Na
Mwandishi Wetu, Addis Ababa
Bomba la Mafuta:
WIKI hii nchi tatu za
Afrika Mashariki zipo katika kile kinachoweza kufananishwa na sintofahamu kuhusu
ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Pwani ya Afrika Mashariki. Mradi
huo mkubwa unalenga kuisaidia Uganda kulifikia soko la kimataifa.
Takwimu zinaonesha kuwa
Uganda ina kiasi cha hazina ya mafuta inayofikia mapipa bilioni 2 (na utafutaji
unaendelea) kiasi ambacho Serikali ya nchi hiyo inapanga kukisafirisha kama
mafuta ghafi kwnda nje ya Afrika na sehemu nyingine kusafishwa ndani ya Uganda na
pia katika soko jirani la Rwanda, Kenya na Tanzania.
Kufikia hali ilivyo
sasa kuna mengi yametokea ambapo Kenya ndiyo ilikuwa ya kwanza “kuanza
mazungumzo” na Uganda juu ya ujenzi wa bomba hilo kwa njia ya Kaskazini.
Mazungumzo haya kwa tathmini yangu yalikwama kwa sababu Kenya walileta mazoea
na pia kuegama zaidi katika “biashara” kuliko “ubia” wenye maslahi mapana ya
kikanda.
Katika makala haya
nitajaribu kujenga hoja kwa nini mradi huo sasa umeangukia mikono salama ya
Tanzania baada ya siasa na sanaa za muda mrefu za Kenya katika mradi huu muhimu
kwa ukandi wetu wa Afrika Mashariki. Zipo sababu nyingi lakini hapa nitajadili
mambo matatu: usalama, gharama za mradi na pia mabadiliko ya kisiasa katika
ukanda huu kufuatia ujuo wa Dkt John Pombe Magufuli wa Tanzania.
Usalama
Ukweli wa muhimu katika
uamuzi kuhusu mradi huu ni usalama. Nairobi inapaswa kujua na kuwa na huruma kwa
wananchi wake, Waganda na raia wengine wa Afrika Mashariki kwa sababu kuupeleka
mradi huu njia ya Kaskazini kutoka Bandari ya Lamu ni sawa na kuwapa Al-Shaabab
kisu na kuku wajichinjie wenyewe kitoweo cha mchana.
Huu ni ukweli wenye
uhalisia na sio propaganda kama Kenya wanavyotaka kujaribu kuwapumbaza wananchi
wa Afrika Mashariki kuhusu mradi huu. Tafiti nyingi zimefanyika na kuchapishwa
kuonesha kuwa njia hiyo ya Kaskazini ni hatari kiusalama tena katika Kenya
ambayo mara kadhaa imeshindwa hata kuwalinda raia wake wenyewe.
Ni bahati nzuri pia
kwamba kampuni ya Total iliyo tayari kutoa kiasi cha dola za Marekani bilioni 4 kuufadhili ujenzi huo kwa njia ya
Kusini (kuanzia Bandari ya Tanga) nayo inaguswa sana na suala hili la usalama.
Total sio watu wa kuambia
kuhusu ubaya wa usalama dhaifu katika sekta ya mafuta na gesi na wala sio watu
wa kuhakikishia usalama kupitia makaratasi na “power point presentations” kama
wanavyofanya Kenya.
Kampuni hiyo
inayosimamia sehemu kubwa ya mafuta ya Uganda imepata kukumbana na matukio
mengi kwingineko duniani ya wafanyakazi wake kushambuliwa na hata kuuawa wakiwa
katika ujenzi au usimamizi wa miradi kama hiyo.
Mwaka huu wafanyakazi 11 wa Total waliuawa katika moja ya visima vya mafuta
wanavyovisimamia nchini Libya katika shambulio linaloaminika kutekelezwa na
wafuasi wa kundi linaloungwa mkono na Islamic State.
Kampuni hiyo pia ina uzoefu mwingine kwa kuwa inamiliki visima katika eneo
lililo katikati ya vita la Yemen na Algeria ambako mwaka 2013 wapiganaji
wanaoaminika kuwa wenye uhusiano na Al-Qaeda waliwaua wafanyakazi 40 waliokuwa
wakiwashikilia mateka katika kisima kimoja cha gesi
Kwa uzoefu huu wa Total lakini pia kwa manufaa ya Uganda na ukanda mzima wa
Afrika Mashariki, Nairobi inapaswa kukubali kuwa ingawa mradi huu kwao ulikuwa
na malengo mengi na ya kibiashara kwao lakini Uganda na EAC hatupaswi
kujiingiza katika hatari iliyo wazi ya kiusalama.
Ripoti moja ya taasisi ya Practical Action inaonesha eneo la Kaskazini mwa
Kenya lilivyosheheni usafirishaji haramu wa silaha, somo kutoka shambulizi
dhidi ya Chuo Kikuu cha Garissa na ukweli kwamba sehemu ya bomba itapita ukanda
mrefu usio na makazi ya wala wa vijiji vya karibu, vyote vinaashiria urahisi
kwa Al-Shaabab.
Katika hili, Rais Kenyatta
anapaswa kuwa muungwana tu kuruhusu mradi huo uendelee kwa njia ya Tanzania
huku yeye akiangalia zaidi biashara na Sudani Kusini au kama walivyopendekeza
Wakenya wengi katika mtandao wa gazeti la The Daily Nation wengi wameshauri “Serikali
ya Kenya iangalie zaidi namna ya kusafirisha hazina ya mafuta waliyo nayo.”
Gharama za Mradi
Jambo la pili ambalo
harakati za Kenya zinashangaza ni ukweli huu wa, ukiacha lile la gharama ya
usalama, lakini pia ukweli kwamba kwa jiografia ya njia ya Kaskazini, mradi huu
utakuwa na gharama kubwa.
Hali hiyo inaweza kuwa
na madhara makubwa kwa uchumi wa Uganda na majirani zake kwani mafuta ya nchi
hiyo yatakuwa ya gharama kubwa zaidi ya inavyotarajiwa. Takwimu za wataalamu
zinaonesha kuwa kwa njia ya Kaskazini itakayoanzia katika Bandari “ambayo
haipo” ya Lamu, mradi wa bomba hilo utakuwa wa gharama kubwa kwa namna nne.
Mosi, ujenzi wa mradi
kwa njia ya bandari ya Lamu utakuwa ni takribani kilometa 1,300 lakini kwa
sababu nyingine pia nitakazozieleza hapa punde ujenzi wake utapanda hadi kufikia
dola za Marekani bilioni 4.5. Huu ni mzigo usio na sababu.
Kwa njia ya Bandari ya
Tanga ambayo urefu wake utakuwa takribani kilometa 1,400 ujenzi wake unaelezwa
utakuwa ni dola za Marekani bilioni 4.0 tu. Hii ni nafuu kwa kiwango cha
trilioni moja na ushee lakini pia bado kuna gaharama nyingi nyingine pia
zitapungua.
Tatu, wataalamu wa
sekta ya mafuta wanasema kwa aina ya mafuta ya Uganda ambayo ni mazito hali ya
hewa ya Ukanda wa Juu wa Kaskazini mwa Kenya itasababisha mafuta hayo kuganda
na hivyo kuhitajika gharama zaidi za kulipasha moto mara kwa mara bomba hilo.
“Ujenzi wa mradi huu
unahitaji teknolojia tofauti kidogo kama utachukua njia ya Kenya. Kwa aina ya
mafuta mazito yaliyogundulika Uganda ambayo ni kama nta hivi hali ya baridi
katika maeneo walikopanga lipite bomba itasababisha gharama zaidi ya kulipasha
moto bomba mara kadhaa ili mafuta yaweze kusukumwa,” anasema mtaalamu mmoja
aliyesimamia miradi mingi ya ujenzi wa mabomba ya gesi na mafuta Ulaya na
Afrika.
Nne, gharama nyingine
ambayo wataalamu wa Kenya wanataka kuzificha ni uasili wa Bandari ya Lamu
ambayo haipo kwa sasa (ndio inajengwa). Bandari hii sio ya kama ile ya Tanga
hivyo inachangamoto zake katika meli kupakia na kupakua mafuta.
Mtaalamu mmoja anasema
wakati Bandari ya Tanga ni ya asili na iliyozungukwa na visiwa vya karibu
vinavyopunguza mawimbi na hivyo kuzipa meli urahisi wa kupakia au kupakua, kwa
Bandari “inayolazimishwa” ya Lamu Serikali ya Uganda itaingia tena gharama
nyingine ya kulazimika kujenga matenki mengi ya kuhifadhi kwanza mafuta hayo
nje ya Bandari.
Naironi inapaswa
kufahamu kuwa mradi huu ni limbuko la kiuchumi kwa Waganda na kama gharama hizi
zisizo na tija zitakwamisha wananchi wa Uganda kunufaika na mafuta, Kenya
itakuwa imefanya jinai ya kihistoria.
Dkt
JPM
Kitu kimoja kilicho
dhahiri sasa ukiacha suala la usalama na gharama ni kwamba siasa na uchumi wa
Afrika Mashariki kwa sasa zimepata msukumu mpya: ujio wa mtu huyu, Dkt. John
Pombe Magufuli, kiongozi anayeamini katika sayansi badala ya siasa katika
maendeleo.
Huyu ndiye kiungo mpya
katika suala hili ambalo limeshalipotezea muda mrefu Taifa la Uganda na Afrika
Mashariki kwa ujumla na kuzuia kufaidika na raslimali hiyo iliyopo jirani. Hii
ni kwa sababu ukifuatilia mazungumzo ya njia ya Kenya yalivyochukua muda mrefu,
mtu hawezi kukosea kushukuru ujio wa JPM.
Akitumia staili yake ya
utambuzi wa haraka, nia njema na kutaka mambo yaende, imemchukua kikao kimoja
tu na Rais mwenzake Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda na kisha kikao kimoja tu
na Rais wa Total, Afrika Mashariki kwa Rais Magufuli kufanya uamuzi kuwa
Tanzania itakuwa mwenyewe wa ujenzi wa bomba hilo.
Fundisho kwa Kenya ambao
sasa wanaanza upya kuleta siasa za kuhaha kujaribu kuurejesha mradi huo katika
njia ya Kaskazini mwa Kenya ni kwamba siasa za ukanda huu zimebadilika sana na
ama wanapaswa wao nao kubadilika au kubaki wakiyatazama mabadiliko yakitokea.
Mafuta ya Afrika
Mashariki yawe Uganda, Kenya au Tanzania au kwingineo kwa namna moja hayapaswi
kuingiziwa siasa zitakazokwamisha wananchi wa kawaida kufaidika na raslimali
hizo.
Nafahamu kwamba hakuna
kitu kingine muhimu katika ujenzi huo kama muda na hili ndilo limewaliza
Waganda kwa kipindi kirefu. Mradi huu ulipaswa kuwa umeanza jana kuliko kubakia
katika “power point presentation” za Wakenya.
Katika mazingira kama
haya na hali ilivyokuwa inakwenda kwa kusuasua nimefurahishwa na uamuzi wa Rais
Museveni wa kujiuliza WhatWouldMagufuliDo?Jibu la swali hili limekuwa na
kuibukia kwa mradi huo nchini Tanzania na naamini utaanza na kukamilika haraka.
Ushauri kwa Nairobi, na
kama walivyosema wananchi wengi wa Kenya katika mtandao wa Daily Nation, huu
sio wakati tena wa kuendekeza siasa bali watumie muda huu kuimarisha usalama
kwanza katika eneo lake la Pwani na Kaskazini kasha ikamilishe ujenzi wa
Bandari ya Lamu kwanza.
Kwa
leo alamsiki.