Ticker

10/recent/ticker-posts

Rais Samia Ataka Malipo ya Gesi yawe Kama Luku

 Rais Samia Ataka Malipo ya Gesi yawe Kama Luku

 Wizara ya Nishati imetakiwa kuwatafuta Watanzania Wabunifu wa teknolojia, ili waweze kufanikisha mpango wa matumizi ya gesi ya kupikia kwa kulipia kadri unavyotumia.

Wito huo umetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akiuzindua Mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024 Jijini Dar es salaam.

Amesema, "watuletee pia teknolojia rahisi itakayowezesha Wananchi kupata nishati safi kadri ya uwezo wao kwa mfano kulipia kadri anavyotumia kama inavyofanyika kwa umeme na maji, zile pre paid meters.”

Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa, "tunalo jukumu la kuongeza uelewa kwa Wananchi kuhusu nishati safi ya kupikia na kutunga sera nzuri na wezeshi, ili kufikia malengo ya mkakati huu, katika hili wenzetu wa Wizara ya Nishati watatuongoza kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa uhakika na kwa bei inayohimilika kwa Wananchi.”

Hata hivyo ameongeza kuwa moja kati ya maonesho ya mazingira aliyowahi kutembelea aliwahi kuikuta teknolojia hiyo ambapo Watanzania walitengeneza mitungi ambayo unatumia gesi jinsi unavyolipa.

"Unachukua mtungi mzima kama umelipa elfu 10 utatumia gesi yako ya elfu 10 ikimalizika mtungi unakata hata kama gesi ipo mpaka uwasiliane nao tena ulipe tena wakufungulie utumie tena naomba sana watafute au kama wapo wajitokeze tufanye nao kazi,” alisisitiza Rais