Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Angellah J. Kairuki akizungumza na wafanyakazi wa TAMISEMI na TARURA kabla ya uzinduzi wa Magari 43 ya Makatibu tawala wasaidizi (Miundombinu) pamoja na Mameneja wa TARURA Mikoa na Wilaya leo Makao Makuu ya TARURA eneo la Mtumba Jijini Dodoma.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) unatarajia kutumia Shilingi Trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2023/24
katika kuboresha barabara za vijijini na mijini zenye urefu wa Km 144,429.77
ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya usafiri na usafirishaji kwa
urahisi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki wakati wa hafla
ya kukabidhi magari kwa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)
iliyofanyika katika Ofisi za TARURA Makao Makuu katika Mji wa Serikali Mtumba
jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Tarura Mhandisi Victore H. Seff akizungumza na wafanyakazi wa TAMISEMI na TARURA kabla ya uzinduzi wa Magari 43 ya Makatibu tawala wasaidizi (Miundombinu) pamoja na Mameneja wa TARURA Mikoa na Wilaya leo Makao Makuu ya TARURA eneo la Mtumba Jijini Dodoma.
Mhe. Kairuki amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini na mijini kupitia TARURA ili kuhakikisha wananchi wanasafiri kwa urahisi.
’’Serikali ya awamu ya sita imedhamiria
kuwezesha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo na kuimarisha ubia baina ya
wananchi na Serikali, katika ngazi ya msingi kwa kuimarisha miundombinu ya
barabara kupitia TARURA na kwa kufanya hivyo, Bajeti ya TARURA imeongezeka hadi
kufikia tilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo pia leo tunakabidhi
magari yatakayosaidia katika usimamizi wa miradi ili kuhakikisha inakamilika
kwa wakati’’, amesema Mhe. Kairuki .
Aidha, Mhe. Kairuki ametoa pongezi kwa
Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor H. Seff pamoja na watumishi wote wa
TARURA kwa usimamizi bora wa miradi katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi
za ujenzi na matengenezo ya barabara za Wilaya hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023
Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor H. Seff ameeleza kuwa utekelezaji wa
kazi umefikia asilimia 85 ambapo jumla ya Shillingi Bilioni 621 zimetumika kati
ya Shillingi Billioni 653 zilizopokelewa.
Akiongea katika hafla hiyo Naibu katibu
Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu Mhandisi Rogatus Hussein Mativila
amesema pamoja na kazi nzuri inayofanywa na TARURA na watumishi wake pia kuna kila sababu ya kumshukuru Mhe Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kuamua kuiongezea Bajeti TARURA lengo likiwa ni kuhakikisha
inatekeleza kazi zake kwa ukubwa hadi ngazi ya chini ili kumfanya mwananchi
hasa mkulima aweze kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa haraka na kwa gharama
nafuu kwani ukishajenga au kuboresha barabara unakua umeshaboresha thamani ya
mazao yao na kazi zao za kujenga uchumi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Dennis Londo (Mb)ameipongeza TARURA kwa kazi zinazofanyika katika kuimarisha miundombinu ya barabara na kwamba kazi hizo zinaonekana katika maeneo mbalimbali ya nchi.
0 Comments