Ticker

10/recent/ticker-posts

KAMATI YA UKAGUZI YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA TARURA MKOA WA TANGA

Kamati ya Ukaguzi ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imeridhishwa na utekelezaji wa miradi katika Mkoa wa Tanga baada ya kufanya ukaguzi na kuona maendeleo ya miradi mkoani humo.Kamati hiyo imempongeza Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff  kwa kuendelea kusimamia vizuri Miradi inayotelkelezwa na fedha za Serikali.

Hayo yameelezwa na wajumbe wa Kamati hiyo katika kikao cha majumuisho kilichofanyika mkoani Tanga kati ya Kamati ya Ukaguzi pamoja na Meneja wa TARURA Mkoa wa Tanga Mhandisi George Tarimo.

Kamati ilitembelea ujenzi wa daraja la Mkomazi lenye urefu wa mita 40.6 katika barabara ya Kwasunga – Mswaha, ujenzi wa barabara ya Hosana – Lutheran – Mount view kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Km 0.73 Km katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, matengenezo ya barabara ya Mkumbi – Muheza Estate kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Km 0.675 Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, pamoja na barabara ya Sahare Phase II kiwango cha lami yenye urefu wa Km 0.60 katika Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati CPA. Ally Rashid Ally alisema, Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa miradi inayoendelea kutekelezwa na wametoa ushauri kwenye mapungufu waliyoyaona katika miradi waliyoitembelea na kusisitiza katika suala la usimamizi wa miradi kwa ukaribu.

“Tumetembelea miradi katika Halmashauri ya Jiji laTanga, Wilaya ya Muheza, Wilaya ya Korogwe pamoja na mradi mkubwa wa kimkakati wa ujenzi wa daraja la Mkomazi utakaotumia shilingi bilioni 3.8 mpaka kukamilika kwake, tumejionea kazi kubwa iliyofanyika katika Mkoa huu’’, alisema

Mwenyekiti wa Kamati aliendelea kusisitiza kuwa jukumu lao kubwa ni kutoa ushauri kwa yale wanayoyaona ili miradi iweze kuwanufaisha wananchi.

Pia Kamati imeishauri TARURA Mkoa wa Tanga kuendelea kusimamia miradi kwa ukaribu, kufanya usafi katika mitaro, uwekaji wa alama na taa za barabarani pamoja na kuongeza sehemu za watembea kwa miguu katika miradi ya barabara waliyotembelea.

Post a Comment

0 Comments