Ticker

10/recent/ticker-posts

Rais Samia na Rais Museveni Wazindua Mradi wa Kimakakati EAC..Ni huu hapa

 

Uganda. Marais wa nchi mbili za Tanzania na Uganda wamezindua mradi kimakakati wa umeme Afrika Mashariki ujulikanao kama Kikagati Murongo Hydropower Plant, wenye uwezo wa kuzalisha megawati 14 ambazo zitanufaisha nchi hizo mbili.

Mradi huo unaotokana na maji ya Mto Kagera, umegharimu dola za Kimarekani milioni 56, na umezinduliwa leo Mei 25, 2023 wilayani Isingiro nchini Uganda na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akishirikiana na Rais wa Uganda, Yoweli Kaguta Museveni.

Akiongea na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotajwa majina yake kwa kuwa yeye siyo msemaji wa mradi huo, mmoja wa viongozi waandamizi katika Wizara zinazosimamia nishati kwenye nchi hizo, amesema mradi ulianza kutekelezwa 2017 na kukamilika 2022 na tayari wananchi wa nchi hizo wananufaika na matunda yake.

Wakati wananchi nchini Tanzania wamenufaika kwa kupata megawati 7, vivyo hivyo wenzao wa Uganda wanapata megawati 7.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kwa upande wa Tanzania mradi umezinufaisha baadhi ya wilaya za Mkoa wa Kagera ambazo ni Kyerwa Karagwe na Misenyi.

Hii ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa kupitia uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kushirikisha nchi wanachama.

Miradi hii inalenga kunufaisha jamii ikiwa ni sehemu ya kuufanya umma kutambua na kuthamini ushirikiano wa kikanda ili hatimaye kufikia lengo la utangamano wa nchi za EAC.

Tayari mradi unaofanana na huu umetekelezwa eneo la Rusumo Wilaya ya Ngara ikizinufaisha nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi.

Huu mradi wa Kikagati pia umeijenga upya Shule ya Msingi Murongo upande wa Tanzania kama sehemu Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Aidha Mkoa wa Kagera unatekelezwa mradi mwingine wa umeme katika maporomoko ya maji Rusumo Wilaya ya Ngara ambao utazinufaisha nchi tatu za Tanzania Rwanda na Burundi wenye megawati 80 na kwa sasa umefikia asilimia 99.

Post a Comment

0 Comments