Ticker

10/recent/ticker-posts

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA



Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu na ajali za barabarani ili kuhakikisha kuwa wageni na wakazi wa mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa usalama hali inayopelekea kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu, ajali za barabarani na kukamatwa kwa watuhumiwa mbalimbali wa uhalifu.


Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na misako na doria ni kama ifuatavyo:-


KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kupatikana na Nyara za Serikali vipande kumi na moja [11] vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilo 21.5 sawa na Tembo 4 wenye thamani ya Tshs 137,970,000/=. Watuhumiwa hao ni:-

ABDULMARIK UPETE [41] mkazi wa Uyole
MOHAMED OMARY [50] mkazi wa Kilosa Mkoani Morogoro na
AYOUB KIDUMBA [49] mkazi wa Ilembula Mkoani Njombe.
LAWI KALONGA [50] mkazi wa Mkoani Dodoma.
Watuhumiwa walikamatwa Disemba 21, 2019 majira ya saa 18:30 jioni huko eneo la Soweto lililopo Kata ya Ruanda, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya baada ya Jeshi la Polisi kuweka mtego. Nyara hizo zilisafirishwa kutoka Mkoani Njombe kwa lengo la kutafuta wateja na zilikuwa zimehifadhiwa kwenye duka la kuuza vipuri vya magari mali ya ABDULMARIK UPETE. Taratibu za kisheria zinafanywa ili watuhumiwa wafikishwe Mahakamani.

KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KULIPIA USHURU.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili [02] kwa tuhuma za kuingiza nchini bidhaa aina ya vitenge belo 24 kila belo moja likiwa na doti 50 za vitenge sawa na doti 1,200 kutoka nchini Zambia bila kulipia ushuru. Mzigo huo ulikuwa unasafirishwa kwenye gari T.471 BJJ aina ya Toyota Hiace. Watuhumiwa waliokamatwa ni:-

1.ELIA MWAKAGILE [30] mkazi wa Mwakibete na

2.FURAHA LUTENGANO MWAKALENGELA [35] mkazi wa Mwakibete.


Watuhumiwa wamekamatwa Disemba 22, 2019 majira ya saa 03:00 usiku huko eneo la Ituta lililopo Kata na Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya – Tunduma.

Taratibu zinafanywa ili watuhumiwa pamoja na mzigo huo kukabidhiwa Mamlaka ya Mapato [TRA] kwa hatua za kiforodha.


iii. KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KULIPIA USHURU.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtuhumiwa mmoja [01] MARIAM JAPHET [35] Mkazi wa Ilembo – Mbeya kwa tuhuma za kuingiza nchini bidhaa aina ya vitenge doti 42 kutoka nchini Malawi bila kulipia ushuru.
Mtuhumiwa amekamatwa Disemba 22, 2019 majira ya saa 06:30 alfajiri huko eneo la stendi ya mabasi Kyela, iliyopo Kata ya Kyela – Kati, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. Taratibu zinafanywa ili mtuhumiwa pamoja na mzigo huo kukabidhiwa Mamlaka ya Mapato [TRA] kwa hatua za kiforodha.

KUKAMATWA WATUHUMIWA WANAOJIHUSISHA NA
MTANDAO WA WIZI WA PIKIPIKI NA MATUKIO MENGINE
YA UHALIFU.

Katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka – 2019 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya msako maeneo mbalimbali Mkoani Mbeya dhidi ya wahalifu wa matukio mbalimbali ikiwemo mtandao wa wizi wa Pikipiki.

Katika misako iliyofanyika jumla ya watuhumiwa wanne [04] wamekamatwa, wamehojiwa na wamekiri kufanya matukio kadhaa ya uporaji wa Pikipiki na kuziuza nchi jirani ya Malawi na Zambia.

Watuhumiwa waliokamatwa katika misako ya hivi karibuni ni pamoja:-
ADAM BRAYSON SANGA [27] Bodaboda, mkazi wa Iyunga
OSCAR ELIAS MWAKABIKI [25] mkazi wa Utengule – Mbalizi na
BENJAMIN SILVESTER MWANDATA [26] Bodaboda na mkazi wa Utengule – Mbalizi.

4: RAMADHAN BAKARI [25] mkazi wa Lupa – Chunya.


KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA WIZI KWENYE MAGARI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya litaendelea kufanya misako na doria katika maeneo yote ili kuhakikisha linasambaratisha mtandao wa wizi wa Pikipiki na wahalifu wengine kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama ndani ya Mkoa wa Mbeya.

Kutokana na kuibuka kwa wizi wa vifaa vya magari katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya misako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne [04] kuhusiana na matukio ya wizi kwenye magari, kuvunja vioo vya magari na kuiba betri za magari, kufungua milango ya magari na kuiba vitu vya thamani.

Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na matukio hayo ni:-
JOSEPH SIMON @ MBOGOLO @ WHITE [40] Mkazi wa Mwananyamala D’Salaam.FAIDHA NSAJIGWA @ MWASEBA [44] Mkazi wa Isanga.
GABRIEL MWANDWANGA [48] Mkazi wa Manga – VETA.
AYOUB EMANUEL KISUNGA [22] Mkazi wa Iyela

Watuhumiwa hao walikutwa na vifaa vya kuvunjia magari na baada ya kuhojiwa wamekiri kuhusika na matukio kadhaa ya wizi kwenye magari katika maeneo ya Forest, Kabwe, Isanga, Uyole, Sokomatola na Mwanjelwa Jijini Mbeya. Pia wamekiri kufanya matukio kama hao katika mikoa ya Arusha na Tanga.

Misako na ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu Mkoani Mbeya inaendelea vizuri.

MAUAJI


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wawili mke na mume ambao ni ALLY MBAVU [23] na SABINA ALEX [19], wakazi wa Pambogo kufuatia kifo cha mtoto wao ISMAIL ALLY MBAVU [mwaka 1 na miezi 11]

Tukio hilo limetokea Disemba 22, 2019 majira ya saa 06:30 alfajiri huko mtaa wa Pambogo, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya. Marehemu alitoweka nyumbani kwao tangu Disemba 21, 2019 jioni na hakuonekana mpaka alipokutwa amefariki dunia.

Uchunguzi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika, watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.


vii. KUELEKEA SIKUKUU ZA KRISMAS NA MWAKA MPYA.

Katika kuelekea sikukuu za Mwisho wa Mwaka [Krismas] na Mwanzo wa Mwaka [Mwaka Mpya] Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga kikamilifu kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa Mbeya, wageni na wakazi wa mikoa jirani wanasherehekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu.


Kwa kutambua kuwa Mkoa wetu unapakana na nchi jirani ya Malawi pia barabara kuu inayounganisha nchi yetu na nchi jirani pamoja na mikoa jirani imepita hapa, tumejipanga vizuri kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa barabara wakiwemo madereva na watembea kwa miguu. Wito wangu kwa watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Kuelekea kipindi hiki cha sikukuu, waumini wa madhehebu mbalimbali ushiriki katika ibada/misa kwa nyakati tofauti kulingana na ratiba zao, Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama katika makanisa pamoja na misikiti hasa katika misa au ibada za mkesha. Aidha ninatoa wito kwa viongozi katika makanisa na misikiti kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri hasa katika suala la ulinzi kwa kuunda kamati za ulinzi na usalama ili kuhakikisha ulinzi unakuwepo maeneo ya ndani na nje ya Makanisa na Misikiti.

Pia rai kwa wamiliki wa Kumbi za starehe kufuata sheria hasa kuzingatia Leseni zao za biashara zinavyowaelekeza ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda wa kufungua na kufunga sehemu zao za biashara, wenye kumbi za muziki kuhakikisha kambi zao zinaingiza idadi ya watu inayohitajika [capacity] pamoja na kuweka walinzi katika maeneo yanayowazunguka.

Kuelekea msimu huu wa sikukuu, ni wito wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuzingatia ulinzi wa mtoto, na pia kuwasaidia watoto hasa kuwavusha katika maeneo tete kama vile barabarani au maeneo yenye mito ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata. Pia ili kuepuka watoto kupotea katika kipindi cha sikukuu, wazazi na walezi wanapaswa kuongeza umakini, uangalizi wa watoto wao kila mahali wanapokwenda iwe ni makanisani, misikitini au katika maeneo yenye michezo ya watoto ikiwemo fukwe za ziwa nyasa Matema na Ngonga Wilayani Kyela.

Mwisho, nitumie fursa hii kuwatakia wananchi wote wa mkoa wa Mbeya na Watanzania kwa ujumla Kheri ya Krismas na Mwaka Mpya 2020 tukumbuke kufanya vitu kwa kiasi, tusivuke viwango/mipaka.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2QjxXvJ
via

Post a Comment

0 Comments