Ticker

10/recent/ticker-posts

CUF na CCM Watuhumiana Kwa Ubaguzi Pemba

Wakati hali ikionekana si shwari visiwani Zanzibar baada ya kuwapo kwa madai ya kutengana, kubaguana na kuharibiana mali, vyama vya CUF na CCM vimetupiana mpira kwa kila kimoja kikimtuhumu mwenzake.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria (CUF) Wilaya ya Wete, Mwinyi Juma Ali amesema kuwa chama hicho kinaheshimu misingi ya utawala bora na haki za binadamu na kauli hizo hazina ukweli wowote.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana ofisini kwake, Wete , Mwinyi alisema chama hicho kinasikitishwa na vitendo hivyo hasa vya kufyekwa mashamba na kusababisha hali ya umaskini kwa wananchi .

“Kusema kuwa kitendo cha hujuma hizi kinasababishwa na CUF siyo kweli, kwani chama chetu kinathamini na kuheshimu misingi ya utwala wa sheria na haki za binadamu na hujuma hizi zinatuathiri hata sisi, ” alisema Mwinyi.

Hata hivyo, jana Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman alisema hujuma hizo zinapangwa na kuratibiwa na wafuasi wa CUF.

Othman aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kutembelea shamba la mihogo na migomba, lenye ukubwa wa eka tano lililofyekwa.

Othman alivitaka vyombo vya ulinzi kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwani vitendo hivyo vinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Akizungumzia hayo, Mkurugenzi wa CUF, Mwinyi alisema kwamba tangu tuhuma hizo zianze kuelekezwa kwa wanachama wa CUF, hakuna hata mwananchama mmoja ambaye amefikishwa mahakamani wala kutiwa hatiani na kuongeza huo ni msamiati wa propaganda za kisiasa.

Kuhusu migomo inayoendelea, alisema CUF haihusiki na masuala hayo, bali imekuja baada ya viongozi wa Serikali kuwakatisha tamaa wananchi kutokana na chuki zao binafsi