Ticker

10/recent/ticker-posts

ZITTO KABWE ANG’ANG’ANIA UFISADI BENKI YA STANBIC..SIKIA KAULI ZAKE HAPA


MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo) ameitaka serikali kumwagiza Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kubaini wizi wa Sh. 608 trilioni zilizokopwa kupitia Benki ya Stanbic yenye tawi lake nchini hapa.

Ametoa kauli hiyo leo bungeni wakati akiuliza swali la nyongeza kutaka kujua ni hatua gani ambazo zinachukuliwa kutokana na ufisadi mkubwa wa fedha hizo ambazo ni trilioni 6.8.

“Jumla ya fedha ambazo serikali ilizikopa nje kwa mfumo wa namna hiyo ni shilingi trilioni 6.8 na katika taarifa ya hukumu inaonesha mtindo huo wa kutumia vikampuni kwa ajili ya kupata mikopo imekuwa ikitumika na mabenki mengi ya kibiashara hapa nchini.

“Serikali haioni kwamba umefika wakati CAG aweze kufanya ukaguzi maalum wa mikopo yote ya kibiashara ambayo serikali imechukua katika kipindi hicho ili kuweza kujua kama pia kulikuwa kuna aina za rushwa za namna hiyo ambazo zimekuwa zinafanyika,”amehoji Zitto.

Zitto amesema DFA (Hukumu ya Uingereza) ilikuwa ina lengo la kuilinda Benk ya Uingereza ambayo ndiyo ilitoa hongo kwa maofisa wa Tanzania ili iweze kupata biashara ambapo alihoji, serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa kufungua kesi dhidi ya benki hiyo ya Uingereza ili iwe fundisho kwa kampuni za nje zinazohonga kwa lengo la kupata biashara katika nchi za kiafrika

Akijibu maswali hayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji George Masaju amesema CAG anayo majukumu ya kikatiba na hilo ni jukumu ambalo anaweza kulitekeleza wakati wowote ili kujiridhisha kama mikopo hiyo ambayo imekuwa ikipatikana kwa namna ambayo inaifanya nchi iingie kwenye hasara.

Amesema, kama Zitto anazo taarifa zozote zinazoweza kuisaidia serikali ama kufungua shauti la madai ama jinai ashirikiane na vyombo husika ikiwemo Ofisi ya AG na kuliangalia ili kuona kama linakidhi sifa na sheria na kwa kuzingatia pia uhusiano uliopo kwa nchi ya Uingereza ili kuona kama kesi ya jinai inaweza kufunguliwa.

Aidha amesema serikali imepokea ushauri wa Zitto na itaufanyia kazi kwa kuzingatia sheria za ndani ya nchi na uhusiano wa kisheria katika Jumuiya ya Kimataifa.

Awali katika swali la msingi la Zitto alitaka kujua serikali inaichukulia hatua gani Stanbic Bank ili walipe fidia zaidi.

“Mwaka 2013 serikali ilizuia hatifungani ya thamani ya dola za Kimarekani milioni 600 (USD 600.0 mili) kupitia Benki ya Sdandard yenye tawi hapa nchini (Stabic).

“Shirika la Corrupition Watch la Uingereza kwa kutumia vyombo kama IFM imeonesha kuwa hatifungani hiyo imeipa Serikali ya Tanziania hasara ya Dola za Marekani miliono 80 na serikali imelipwa fidia Dola za Marekani milioni 6.

“Je kwa nini serikali haichukulii hatua Stanbic Bank ili ilipe fidia zaidi?”amehoji Zitto.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashantu Kijaju amesema, serikali imefuatilia taarifa za hasara kwa Serikali ya Tanzania ya Dola za Marekani 80 iliyotajwa na Zitto lakini haikupata ushahidi wake.

Hata hivyo Dk. Kijaju amesema Benki Kuu ya Tanzania imeiandikia Benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya Sh. 3 bilioni kwa kosa la kufanya miamala inayokiuka sheria na kanuni za mabenk na taasisi za fedha.