Ticker

10/recent/ticker-posts

MAPENZI:Nani kasema ukiumizwa huwezi kupenda tena?Soma hapa uelewe

Image result for MAPENZI IMAGEHabari yako msomaji wa kona hii! Ni matumaini yangu kwamba uko poa na unaendelea na majukumu yako ya kila siku. Nakukaribisha tena jamvini ili tuzungumze na kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa kimapenzi.
Leo nimeamua kuja na mada hii baada ya kusikia malalamiko kutoka kwa wasomaji wangu kadhaa ambao wanalia baada ya kuumizwa na wenzi wao kiasi cha wengine kufikia hatua ya kujiapiza kwamba hawawezi tena kupenda.
Unapozungumzia suala la maumivu ya mapenzi, japokuwa huumiza sana hasa kama ulikuwa na mapenzi ya dhati na mwenzi wako na baadaye akaamua kukugeuka, siyo suala geni hapa duniani.
Unapolia leo kwa sababu ya mapenzi, elewa kwamba mamilioni ya watu wanalia kama wewe ingawa tunatofautiana namna ya kukabiliana na maumivu. Lakini cha kujiuliza ni je, mpenzi wako akikuumiza sana ni sahihi kujiapiza kwamba hutapenda tena?
Ni sahihi kusema kwamba siku hizi hakuna mapenzi ya ukweli kwa sababu tu amekuumiza? Ni sahihi kusema wanaume wote wako hivyohivyo au wanawake wote ndivyo walivyo?
Ukweli ni kwamba, unapovunjika moyo haimaanishi kwamba huo ndiyo mwisho wako wa kupenda. Unapojiapiza kwamba hutapenda tena au hutamwamini mtu tena ni makosa makubwa kwa sababu kama uliyekuwanaye ameshindwa kuiona thamani ya penzi lako, yupo ambaye atakuthamini na kukuheshimu.
Kuna usemi maarufu usemao kwamba mlango mmoja unapojifunga, mwingine huwa unafunguka muda huohuo lakini wengi wetu hupoteza muda mrefu kuutazama ule uliojifunga badala ya kuufuata uliofunguka.
Msemo huo una maana kubwa kwenye mapenzi kwamba kama mwenzi wako amekutenda, amekuvunja moyo, amekusononesha na kukufanya ulie, jua kwamba hakuwa ridhiki yako. Huwezi kujua Mungu amekuepusha na nini kwa hiyo badala ya kujiapiza na kukufuru, ni bora ukakubaliana na ukweli, japo huwa inauma sana.
Ukishaukubali ukweli, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupona majeraha ndani ya moyo wako na nakuhakikishia, hata kama ulimpenda vipi huyo uliyekuwa naye, kama amefikia hatua ya kukuumiza na kuuvunja moyo wako, hakuwa riziki yako, endelea kumuomba Mungu kwa sababu yupo ambaye ndiye haswa aliyepangwa kuwa wako.
Upo usemi mwingine kwamba watu wengi huwa hawaoni umuhimu wa kitu mpaka wanapokipoteza na wakati huohuo huwezi kujua ulichokuwa unakikosa mpaka pale utakapokipata. Yawezekana ulimpenda sana lakini huwezi kujua ulikuwa unakosa nini mpaka utakapokutana na yule mwenye mapenzi ya dhati, ambaye atakuheshimu na kukutunzia penzi lako.
Kinachowaumiza wengi huwa ni matarajio makubwa wanayokuwa nayo kwa wenzi wao. Unapomuonesha mwenzi wako mapenzi ya dhati, haimaanishi na yeye atakuonesha kama unavyotaka iwe.
Unaweza kupenda sana lakini ukaishia kulipwa mabaya, kitu cha kuzingatia ni kwamba kama umeamua kupenda, penda kwa moyo wako wote na kama unayempenda ni sahihi kwako, utajikuta nafsi yako ikiridhika na utakuwa na furaha. Unapoweka mategemeo makubwa kwamba mwenzi wako naye atakupenda katika kiwango sawa na kile unachompenda, ikitokea ameenda tofauti, maumivu yake huwa makubwa sana.