Ticker

10/recent/ticker-posts

Msikilize Kocha Gamondi Kuhusu kutimka Yanga Licha ya Mafanikio Makubwa

Kocha Gamondi Kutimka Yanga Licha ya Mafanikio Makubwa

Huku mashabiki na wanachama wa Yanga wakifurahia namna timu yao ilivyocheza vizuri michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifika hatua ya makundi baada ya

miaka 25, lakini pia ikitinga robo fainali kwa mara ya kwanza, kocha aliyefanya kazi hiyo, Miguel Gamondi, amesema hana uhakika wa kuendelea kubaki katika klabu hiyo kwa msimu ujao.

Gamondi, ambaye ni kocha mkuu wa timu hiyo, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili wakitokea Afrika Kusini ambapo walitolewa na Mamelodi Sundowns kwa mikwaju ya penalti 3-2 kutokana na dakika 90 za pili kumalizika kwa suluhu kama zile za awali katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Alipoulizwa kuhusu mipango yake ya msimu ujao baada ya kuichukua Yanga msimu wa kwanza na kuiingiza makundi baada ya miaka 25 kupita, huku akiifikisha robo fainali kwa mara ya kwanza tangu mfumo mpya wa michuano hiyo kuendeshwa kwa mtindo wa ligi ulipoanzishwa mwaka 1997, Gamondi alikataa kuelezea kwa madai hana uhakika wa kuendelea kuwapo na ataelezea kama atakuwapo kipindi hicho.

"Siwezi kuelezea hilo kwa sababu sina uhakika kama nitakuwapo kwa hivyo siwezi kuelezea mipango yoyote ya baadaye," alisema.

Lakini kuhusu mbinu alizotumia kuweza kuisumbua Mamelodi inayosifika kwa kucheza soka la kuvutia Afrika, alisema ana furaha kubwa kwa kiwango walichoonyesha, akiwapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa maelekezo yake na kwa usahihi zaidi, wakiongeza na juhudi, upambanaji na kujituma.

"Nina furaha kwa kiwango tulichocheza na pia uwezo wa wachezaji wangu, walichofanya ni kucheza kwa maelekezo na kwa usahihi, kujituma, nidhamu na kupambana, usisahau tulikuwa tunacheza na Mamelodi Sundowns. Tulizuia mianya yao yote ambayo walikuwa wanatumia ili kufanya mashambulizi, wametengeneza nafasi chache sana za kufunga kitu ambacho si kawaida, hii si sifa kwa Yanga tu bali ni kwa Tanzania nzima," alisema Gamondi.

Kocha huyo alikiri kuwa si kazi rahisi kucheza na timu hiyo kwani kila mtu anafahamu kuwa ni moja kati ya timu kubwa barani Afrika, huku pia akikumbushia bao walilonyimwa.

Katika hatua nyingine ya mzunguko wa pili ya watani wa jadi, Simba na Yanga imepangwa kuchezwa Aprili 20, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa jana na Bodi ya Ligi, imeeleza kuwa mchezo huo namba 180, awali haukupangwa kwenye ratiba iliyofanyiwa maboresho na kutangazwa Februari mwaka huu, ambapo sasa utachezwa saa 11:00 jioni, Yanga ikiwa mwenyeji.

"Klabu za Simba na Yanga pamoja na wadau wengine wa Ligi Kuu wamepatiwa taarifa zote zinazohusiana na mchezo huo na maandalizi yake yanaanza mara moja ili hakikisha unafanyika katika kiwango cha juu kinachoendana na michezo mikubwa ya ligi ya sita kwa ubora Afrika," ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na ldara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi nchini, TPLB.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa kwenye uwanja huo, Novemba 5, mwaka jana, Simba ikiwa mwenyeji, ilikutana na kipigo cha mabao 5-1. 

Post a Comment

0 Comments