Ticker

10/recent/ticker-posts

Naibu Waziri Mavunde: Serikali ya Rais Samia itaongeza uzalishaji wa Miche ya Mkonge kufikia Milioni Moja.

Serikali imepanga kuzalisha miche milioni kumi kwa njia ya teknolojia ya chupa (Tissue  Culture) kupitia maabara ya kisasa inayojengwa katika Kituo cha Utafiti TARI Mlingano,Wilaya ya Muheza,Tanga.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde alipotembelea Kituo cha TARI Mlingano wilayani Muheza na kukagua maendeleo ya ujenzi wa maabara hiyo.

"Mahitaji ya miche ya mkonge ni takribani milioni 11 kwa mwaka, wakati uwezo wetu kwa sasa ni kuzalisha kupitia TARI ni wastani wa miche milioni 5 tu kupitia njia zote yaani ya vikonyo na chupa. Wakulima wengi waliokuwa wameacha kulima mkonge wamehamasika kurudi kupanda zao hili la kimakati.

Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija. Na ndiyo maana mnaweza kuona kipindi cha miaka 2 hii, bajeti ya utafiti imeongezeka kutoka wastani wa bilioni 11.7 hadi bilioni 43 ili kuwezesha kufanya utafiti wa mbegu bora zitakazoleta manufaa kwa wakulima.

 Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuwajengea uwezo watafiti ili waweze kufanya tafiti ambazo zitakuwa na tija na zinazoendana na wakati uliopo sasa ambazo zitakuwa na manufaa kwa wakulima na taifa kwa ujumla.


Msimu uliopita uzalishaji wa mkonge ulifikia tani 48,513. Kwa msimu huu, kwa kipindi cha Januari-Julai, 2023 takribani tani 34,000 zimezalishwa, ambazo zimetuletea fedha za kigeni Dola za Kimarekani Milioni 41 na fedha za ndani shilingi Bilioni 23, mtaweza kuona ambavyo mkonge unaendelea kufanya vizuri”Alisema Mavunde

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Mlingano, Dkt. Catherine Senkoro alieleza kuwa hapo nyuma walikuwa wakizalisha miche 500,000 pekee ambapo baada ya kuboresha kwa sasa wanazalisha miche milioni 5 ambayo bado haikidhi. Aliongeza kwamba ujio wa maabara hiyo ni mkombozi kwa wakulima ambao wamekuwa wakihitaji sana miche bora ya mkonge.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Bw. Sadi Kambona alibainisha kuwa tija ya uzalishaji kwenye zao la mkonge ndiyo changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwani mkonge hauna changamoto ya masoko. Aliishukuru Serikali kwa kuipa Bodi ya mkonge fedha za kununua Korona 3 ambazo taratibu za manunuzi zinaendelea ili kurahisisha uchakataji wa mkonge wa wakulima wadogo ambao mwingi umekuwa ukiozea mashambani.

Naye Katibu wa Wilaya ya Muheza Ndg. Mohamed Mfaki amesema kwamba serikali wilayani Muheza itaendelea kuhakikisha kwamba inashirikiana na TARI Mlingano ili wakulima wa Mkonge wanufaike na uwepo wa kituo hichi kwa kuzalisha kwa tija zao la mkonge




Post a Comment

0 Comments