Ticker

10/recent/ticker-posts

RC SENYAMULE: RAIS SAMIA AMETOA BILIONI 5.6 KUKAMILISHA SKIMU YA UMWAGILIAJI BAHI

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule (mwenye kofia) akimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bahi Mhe. Donald Simango Mejiti akifafanua jambo katika eneo la bwawa katika Kijiji cha Kagongo, ambapo ujenzi wa skimu ya umwagiliaji unaendelea.

Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 5.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Kongogo, Kata ya Babayu, Tarafa ya Mundemu yenye ukubwa wa hekta 220.

Hayo yamebainishwa leo na Bw. Raphael Laizer Meneja wa Mradi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya utekelezaji wa ujenzi wa bwawa hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, katika eneo la mradi.

Bw. Laizer amesema ujenzi wa skimu hiyo unaendelea na uko katika hatua za awali chini ya mkandarasi wa Kampuni ya M/S CRJE (EA) kutoka China.

Akizungumza na wakazi wa eneo hilo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa skimu hiyo ya umwagiliaji, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha nchi inakuwa na kilimo cha kisasa kwa kulima mara mbili mpaka tatu kwa mwaka, kuhamasisha shughuli za uvuvi na mifugo bila kuathiri mazingira.

“Kilimo cha uhakika duniani kote ni kilimo cha umwagiliaji, kilimo kinachowezesha wananchi kulima mara mbili hadi tatu kwa mwaka” Senyamule amesisitiza.

Amesema maono ya Serikali ni kuhakikisha nchi ya Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi nyingine duniani katika kulisha dunia kwa kusambaza chakula ndani na nje ya nchi. Amesema sababu za Serikali kuajiri maafisa ugani, kununua vitendea kazi ikiwa ni pamoja na ununuzi wa pikipiki, kuimarisha vitalu vya mbegu zote ni nyenzo za kuimarisha usalama wa chakula na kuimarisha sekta ya kilimo.

Nae Bi. Francisca Ntizi amesema kukamilika kwa skimu hiyo ya umwagiliaji itakuwa ni fursa hususan ya kuimarisha vyanzo mbadala vya mapato ikiwa ni pamoja kujihusisha na kilimo zaidi ya mara mbili kwa mwaka, uvuvi na kilimo cha mbogamboga.

Ujenzi huu wa skimu ya umwagiliaji umeanza Aprili 2023 na utakamilika baada ya miezi 18 ambapo pia rambo litajengwa kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Picha ikionyesha ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Bahi-Misheni ulipofikia unaogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 493.4 fedha za boost. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi Katika Wilaya ya Bahi jana Mei 18,2023 ambapo Ujenzi wa mradi huo unaendelea .
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiongea na kusikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Kongogo wakati wa ziara yake ya kikazi Katika wilaya ya Bahi Mei 18,2023 Mkoa wa Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Rosemary Senyamule akikagua mradi wa bwawa la Umwagiliaji la Kongogo wakati wa ziara yake Katika wilaya ya Bahi Mei 18,2023. Mradi huo unagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 5.6 na bwawa hilo linauwezo wa kuhifadhi maji ya kumwagilia ekari 1000 kwa msimu na linatarajia kukamilika Aprili, 2024.
Wanakijiji wa Kongogo wakimsikiliza Mheshimiwa Rosemary Senyamule Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati akizungumza nao kupitia mkutano wa hadhara, Mei 18,2023 Mkoani Dodoma

Post a Comment

0 Comments