MFANYABISHARA MAARUFU DAR MBARONI KWA TUHUMA ZA KUJIHUSISHA NA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA

  Masama Blog      
  Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya  James Kaji (wanne kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 1,mwaka 2020 kuhusu kukamatwa kwa watu wawili akiwemo mfanyabishara mkubwa jijini Dar es Salaam Abuu Kimboko ambao wanatuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
 Kaimu Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya  James Kaji(katikati) akizungumza leo Januari 1, mwaka 2020 jijini Dar es Salaam kuhusu hatua wanazochukua kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya nchini.Pia ameeleza mikakati yao ya kukomesha biashara hiyo haramu nchini
 Kamishna wa Sheria wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Burhani Kishenyi(katikati) akifafanua masuala ya kisheria katika utendaji wao wa kazi za kukabiliana na dawa za kulevya nchini.
 Kamishna wa Kinga na Tiba Dk.Peter Mfisi (katikati) akielezea jitihada zinazochukuliwa na Mamlaka hiyo katika kuwasadia walioathirika kwa matumizi ya dawa za kulevya.
Kaimu Kamishana Jenerali James Kaji(aliyesimama) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari na hasa umuhimu wa kuandika habari sahihi zinazohusu dawa za kulevya.


*Mamlaka yaelezea hatua kwa hatua namna walivyomfuatilia hadi kumtia mikononi
*Akutwa Mbagala akiwa na gramu 400 za Heroin, Bastola moja na risasi za moto 15


Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii

MAFANYABISHARA mkubwa jijini Dar es Salaam ambaye pia anamiliki magari ya biashara yaliyoandikwa Mashallah anashikiliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini kwa tuhuma za kujihusisha na kusafirisha  dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa Mamlaka hiyo, ni kwamba mfanyabishara huyo aliyetambuliwa kwa jina la Abuu Kimboko amekuwa akitafutwa na nchi mbalimbali kutokana na tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo na hatimate amenazwa na sasa anashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama wakati taratibu za kupelekwa mahakamani zikiandaliwa ili sheria ichukue mkondo wake.

Kaimu Kamshna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya nchini James Kaji amewaambia waandishi wa habari leo Januari 1 mwaka 2020 amesema kuwa mtuhumiwa huyo wa biashara hiyo amekamatwa Desemba 29 mwaka 2019 akiwa maeneo ya Mbagala Zakiem/ Mpakani,  jijini Dar es Salaam tena akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin gramu 400 pamoja na bastola moja na risasi za moto 15 na vyote amekutwa navyo aiwa kwenye gari namba T568 DKC aina ya Toyota Spacioal aliyokuwa akiendesha.

"Huyu jamaaa alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu sana, na sio Tanzania tu bali hata nchi nyingine nako walikuwa wanamtafuta kutokana na kujihusisha na bishara hii haramu.Kwa namna ambavyo Mamlaka na vyombo vya ulinzi na usalama kujipanga vema katika mapambano ya dawa za kulevya, tumemnasa na sasa tunamshikilia.Kwa wanamfahamu huyu Abuu kwa jina lingine la mjini Kipusa ndio anamiliki magari yaliyoandikwa Mashallah,"amesema Kamishna Kaji.

Mbali ya mtuhumiwa huyo Mamlaka hiyo pia imesema inamshikilia Pascal Lufunga ambaye naye anatuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo ya dawa za kulevya .Mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa eneo la Bwilingu Kibaha akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 133.33.

Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo amesema kuwa watuhumiwa hao wote wako ndani na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Pia amesema kwa mwaka 2019, Mamlaka hiyo walifanikiwa kufanya operesheni mbalimbali na kufanikiwa kukamata dawa za kulevya kiasi cha kilo 325.69 za bangi zikiwahusisha watuhumiwa wawili, kilo 892.24 za mirungi zikiwahusisha watuhumiwa tisa  na kilo 34 .47 za heroin zikiwahusisha watuhumiwa watano.

Kuhusu kesi za dawa za kulevya, amesema kuwa kesi 35 zimemalizika katika Mahakama Kuu na dawa zilizohusika na kesi hizo zilishateketezwa na kwamba  ifahamike kuwa pale ambapo Jamhuri haikuridhika na maamuzi au adhabu iliyotolewa kwa washitakiwa wa dawa za kulevya haikusita kukata rufaa.

Ametoa mfano kuwa Jamhuri ilikata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga faini ya Sh.milioni moja aliyopewa Mustafa Juma Kahamis na  Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin gram 40. 16 ndani ya chumba chake.Kamishna Kaji amesema kuwa msingi wa rufaa ya Jamhuri ni kwamba kiasi cha fini alichotozwa mtuhumiwa hakiendani na adhabu mbadala ya kifungo Cha miaka 30 jela.

Wakati huo huo amesema kuwa Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na ofisi ya Mashitaka ya Taifa imefanikiwa kushinda mashauri kadhaa makubwa ya dawa za kulevya  na miongoni mwa mashauri hayo ni lile lilihusu kilo 63 za heroin ambalo iliendeshwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya  Mtwara ambapo watuhumiwa Mwinyi Kitwana Rajabu na Ally Hamduni Hamad walihukumiwa kifungo Cha miaka 20 jela na kutaifishwa gari iliyohusika kusafirisha dawa za kulevya.

Kaimu kamishina wa Mamlaka hiyo ametoa onyo kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara hizo kuacha Mara moja kwani tayari lisiti yao wanayo na muda ukifika watakamatwa na wanaendelea kukamatwa na kwamba wanajua baada ya kuwadhibiti katika njia mbalimbali wanazotumia kusafirishia na kuuza wamebuni njia mpya.

"Ndugu waandishi wa habari nataka niwaambie vijana wetu wameharibika na kuathiriwa kwa kiwango kikubwa sana endapo mkiwaona mnaweza kulia kwa uchungu.Wakati Serikali inahimiza vijana kujikita kujenga nchi yetu lakini kundi kubwa la vijana hao linaharibiwa na dawa za kulevya.Ni jukumu letu kukomesha biashara hiyo ndani ya nchi yetu,"amesema.

Kwa upande wake Kamishna wa Sheria wa Mamlaka hiyo Buruhani Kishenyi amesema wanafahamu kuna changamoto ya sheria hasa zinazotumika kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya lakini wataendelea kufanya maboresho ili ziwe kali zaidi.

Wakati huo huo Kamishna wa Kinga na Tiba Dk.Peter Mfisi amesema wanatambua kuwa watumiaji wa dawa za kulevya baada ya kuona upatikanaji wa dawa nchini umekuwa mgumu, wanabuni mbinu nyingine ikiwemo ya kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya ambapo nazo madhara yake ni makubwa na Mamlaka imekuwa ikichukua hatua ya kukomesha utumiwaji huyo wa dawa hizo.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/39FmNdE
via
logoblog

Thanks for reading MFANYABISHARA MAARUFU DAR MBARONI KWA TUHUMA ZA KUJIHUSISHA NA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA

Previous
« Prev Post