Ticker

10/recent/ticker-posts

MAKAMU WA PILI WA RAIS BALOZI IDDI AWATAHADHARISHA VIJANA KUWA MACHO NA WATU WANAOJIPANGA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI UCHAGUZI MKUU

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewatahadharisha vijana Nchini kuwa macho na Watu walioanza kufanyakazi kinyemela katika mchakato wa kujipanga katika kujiandaa kugombea nafasi za Uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu hapo baadae Mwaka huu.

Alionya kwamba vitendo vinavyoashiria dalili za kufanywa na Watu hao vieleweke kwamba ni kinyume na taratibu zilizowekwa na Taifa na hata Vyama wa Kisiasa kwa vile wakati wa kufanya hivyo haujafika wala kutangazwa rasmi.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa alitoa tahadhari hiyo wakati akizindua Matembezi ya Umoja wa Vijana wa CCM {UVCCM} katika kusherehekea Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoanzia katika Kijiji cha Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema Watu au Wanachama wa Vyama vya Kisiasa wenye nia ya kutaka kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mwishoni mwa Mwaka huu lazima wasubiri kipenga cha mwisho kitakapopulizwa ndipo waanze mchakato huo.

Hata hivyo Balozi Seif  aliwakumbusha Vijana hao wa CCM na hasa wale waliofikia umri wa Miaka 18 kutumia Haki yao ya Kidemokrasia katika kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakati huu uliokwishatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi {NEC} na baadae Tarehe 18 Mwezi huu kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar {ZEC}.

Aliwatanabahisha Vijana hao pamoja na Wanachama wa CCM kwa ujumla kwamba uandikishaji kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ndio msingi pekee unaobainisha ushindi wa Chama hicho ili kiendelee kuongoza Dola la Tanzania kwa Miaka mingi ijayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Vijana hao wa Chama cha Mapinduzi kwa uamuzi wao wa Kizalendo unaopelekea kuendelea kuyalinda, kuyaenzi,  na kuyatetea Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yaliyoleta Haki na Usawa kwa Watu wote.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Waasisi wa Mapinduzi hayo chini ya Jemedari wake Marehemu Mzee Abeid Aman Karume waliamua kufanya kitendo hicho cha Kishujaa kwa lengo la kuwakomboa Wakwezi na Wakulima wa Visiwa vya Unguja na Pemba waliokuwa wakidhululimwa kwa Karne kadhaa zilizopita.

Alielezea faraja yake kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba Mjini na Vijiji katika Kipindi cha Miaka 56 iliyopita ambayo yanaendelea kutoa fursa mbali mbali za upatikanaji wa Rasilmali za Ardhi, Elimu pamoja na Matibabu Bila ya malipo.

Akitoa Taarifa ya matembezi hayo ya Umoja wa Vijana wa CCM, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo Zanzibar Nd. Mussa Haji Mussa alisema Vijana hao wapatao 500 kutoka Mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara na Zanzibar wanatarajiwa kutumia Siku Nane katika Matembezi hayo ya Kilomita 130.7.

Nd. Mussa alisema Kundi hilo la Vijana pamoja na mambo mengine litatembea Wilaya zote za Kisiwa cha Unguja kupitia Vituo vya Mapumziko na kufanya shughuli za Ujenzi wa Taifa kwenyeSekta za Afya, Elimu pamoja na kushiriki Miradi ya Chama cha Mapinduzi.

Mapema akimkaribisha Mgeni Rasmi kuzindua Matembezi hao ya Umoja wa Vijana wa CCM, Mwenyekiti wa Umoja huo Taifa Nd. Kheir James alizipongeza Serikali zote mbili Nchini Tanzania kwa jitihada zinazochukuwa za kuwajengea mazingiura Bora Vijana wa Taifa hili.

Nd. Kheir James alisema Programu ya kuwaendeleza Vijana pamoja na ongezeko la fursa za ajira hasa kwa Vijana ni mfano hai wa jitihada hizo ambazo zimeonyesha kuleta faraja kwa kundi hilo ambalo ndio nguvu kazi ya Taifa.

Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Vijana hao tayari wameshajipanga vyema katika kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kinaendelea kuongoza Dola ya Tanzania katika muda wote.

Alisema Mkakati huo ndio njia sahihi itakayokuwa dira na muelekeo wa kuyalinda, kuyatetea na kuyaendeleza Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yaliyoondoa udhalimu na ubaguzi mkubwa.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM alipofika katika Kijiji cha Kizimkazi Dimbani kuzindua Matembezi ya kuadhimisha Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 Balozi Seif Kati kati akiyaongoza Matembezi ya UVCCM katika Kijiji cha Kizimkazi ikiwa ishara ya kuyazindua rasmi yatakayozunguuka Wilaya zote za Unguja.
  Brass Band ya Chipukizi ya Umoja wa Vijana wa CCM ikiongoza Matembezi ya Vijana hao katika Mitaa ya Kijiji cha Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.
 Vijana wa CCM wakichemka wakati wakipasha moto miili yao kwa ajili ya Matembezi ya kuadhimisha Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

 Balozi Seif akiwakabidhi Vijana hao Picha  ya Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere itakayotumiwa kwenye Matembezi hayo.
 Mmoja miongoni mwa Viongozi wa Matembezi ya Umoja wa Vijana wa CCM akipokea Bendera itakayopeperushwa kwenye Matembezi hayo ya Siku Nane.
 Vijana wa CCM wanaoshiriki Matembezi ya Kuadhimisha Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar wakifuatilia Hotuba ya Mgeni Rasmi Balaozi Seif hayupo pichani kwenye Unjwa wa Michezo wa Kizimkazi Dimbani.
 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Abdulla Juma Saadala {Mabodi Kulia akiwa na Makamu Mwenyekiti wa UWT Tanzania Mh. Thuwaiba Kisasi wakifuatiulia Hotuba ya Mgezni Rasmi.
 Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Nd. Kheir James Kulia akiteta jambo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif huku Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Zanzibar Bibi Tabia Maulid akishuhudia.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dr. Abdulla Juma Saadala akitoa neno la shukrani katika hafla ya uzinduzi wa Matembezi ya UVCCM huko Kizimkazi Dimbani. Picha na – OMPR – ZNZ.



from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2SNMAdp
via

Post a Comment

0 Comments