Ticker

10/recent/ticker-posts

WAZIRI HASUNGA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA MAAFISA UGANI NA CHAMA CHA WAGANI NCHINI.


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka (Annual General Meeting - AGM) wa Chama cha Wagani Tanzania (Tanzania Society of Agricultural Extension and Education - TSAEE) uliofanyika Jijini Dodoma, tarehe 16 Disemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Washiriki wa Mkutano Mkuu wa mwaka (Annual General Meeting - AGM) wa Chama cha Wagani Tanzania (Tanzania Society of Agricultural Extension and Education - TSAEE) wakifatilia hotuba ya mgeni rasmi Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akifungua mkutano huo uliofanyika Jijini Dodoma, tarehe 16 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka (Annual General Meeting - AGM) wa Chama cha Wagani Tanzania (Tanzania Society of Agricultural Extension and Education - TSAEE) uliofanyika Jijini Dodoma, tarehe 16 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano Mkuu wa mwaka (Annual General Meeting - AGM) wa Chama cha Wagani Tanzania (Tanzania Society of Agricultural Extension and Education - TSAEE) uliofanyika Jijini Dodoma, tarehe 16 Disemba 2019.






Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Serikali imekiagiza Chama cha Wagani Tanzania (Tanzania Society of Agricultural Extension and Education - TSAEE) kutumika kama chombo cha kuishauri Serikali katika kuboresha utoaji wa huduma za ugani hapa nchini pamoja na kuwa ni kiungo cha kuwaunganisha watoa huduma za ugani na wadau mbalimbali hapa Nchini.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa kauli hiyo tarehe 16 Disemba 2019 wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka (Annual General Meeting - AGM) wa Chama cha Wagani Tanzania (Tanzania Society of Agricultural Extension and Education - TSAEE) uliofanyika Jijini Dodoma.

Amekitaka chama hicho kusimamia weledi wa Maafisa ugani katika kutekeleza majukumu yao; pia kwa lengo la kuimarisha uhai wa chama amewataka wajumbe wa chama hicho kukutana mara kwa mara ili kujadili mafanikio na changamoto zinazokabili utoaji wa huduma za ugani nchini na kutoa ushauri kwa Serikali namna ya kutatua changamoto hizo.

Pia amewataka Wajumbe, kwa kushirikiana na Viongozi wa Chama hicho kuongeza ubunifu katika kutafuta vyanzo vya mapato kwa ajili ya kuimarisha na kuendesha Chama huku akiwasisitiza kuwa wakati wa uchaguzi wahakikishe wanachagua viongozi makini watakao simamia na kuongoza Chama hicho ili kiwe imara na endelevu.

Kwa upande wa Maafisa Ugani, ili kuweza kuimarisha utendaji wa majukumu yao ya kila siku na hatimaye kuinua sekta ya kilimo nchini, Waziri Hasunga ameagiza kila Afisa Ugani kuwa na Daftari la Kilimo ambalo atalitumia kuweka kumbukumbu zote za muhimu kila atakapoenda kuwahudumia Wakulima.

Amesema kuwa pamoja na taarifa nyingine za msingi, Daftari hilo lioneshe orodha ya wakulima anaowahudumia, ukubwa wa mashamba yao na aina ya mazao wanayolima.

Ameongeza kuwa Afisa Ugani ni lazima awe na Mpango kazi utakaoonesha ni nini hasa amepanga kufanya kwa wakulima, ikiwa ni pamoja na kuainisha ratiba ya kazi kwa kipindi husika huku akitaka kila Afisa Ugani kuwa na mashamba ya mfano au mashamba darasa ambayo atayatumia kuwafundishia Wakulima katika Kata/Kijiji/Mtaa wake.

Kadhalika ameagiza kuwa Afisa Ugani ni lazima awe na Mwongozo wa kusimamia Huduma za ugani na kuhakikisha anausimamia ipasavyo pamoja na kufahamu kanuni au mbinu bora za kilimo cha mazao makuu yote yanayolimwa katika eneo lake.

Waziri Hasunga amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli itaendelea kushughulikia changamoto kwa kutoa msukumo wa kutosha kwa ajili ya uendelezaji wa sekta hizo muhimu hususani kupitia Utekelezaji wa Programu mbalimbali ikiwemo Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II).

Aidha, Amesema kuwa serikali pia itaendelea kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya Nchi ambao wanaonesha dhamira ya dhati ya kuungana na serikali katika kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa kati kupitia shughuli za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2tqFi4R
via

Post a Comment

0 Comments