Ticker

10/recent/ticker-posts

MDH WAZINDUA UPIMAJI WA TB KWA WATOTO KWA NJIA YA MPIRA Inbox x

SHIRIKA la Usimamizi na Uboreshaji wa Huduma za Afya ngazi ya Jamii(MDH) kwa kushirikiana na Serikali,limezindua mpango wa uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa TB kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwa njia ya mpira(mrija).

Uzinduzi huo umefanyika katika zahanati mbili za Ligoma,Misechela na Hospitali ya Misheni Mbesa na Hospitali ya wilaya Tunduru ambao ulikwenda sambamba na mafunzo kwa vitendo ya kuwajengea uwezo baadhi ya wauguzi na Madaktari kutumia njia hiyo mpya kubaini vimelea vya ugonjwa huo kwa watoto.

Mkuu wa Program na mafunzo wa MDH Dkt John Lymo alisema,baada ya uzinduzi kufanyika katika wilaya ya Tunduru wataendelea na wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuwabaini na kuwaanzishia dawa watoto wote watakaobainika kupatwa na maradhi ya kifua kikuu.

Dkt Lymo ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya watoto hapa nchini alisema, lengo la MDH ni kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutokomeza kabisa ugonjwa wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2030 na wapo katika mikoa minane hapa nchini ya Kagera,Mbeya,Dodoma,Tanga,Mara,Shinyanga na Simiyu.

Kwa mujibu wa Dkt Lymo,mpango huo ambao ni mpya hapa nchini utaleta tija kubwa na utasaidia kuokoa maisha ya watoto wengi walio na umri chini ya miaka mitano kwani uzoefu unaonesha kuwa,watoto wadogo kila wanapokohoa umeza makohozi,kwa hiyo inakuwa vigumu kwa wataalam kupata makohozi kwa ajili ya kufanyia vipimo.

Alisema,uchunguzi wa vimelea vya TB kwa kutumia mpira ndiyo njia muafaka kwani mpira uingia moja kwa moja tumboni ambako makohozi hayo yamejificha na kusisitiza kuwa,njia hiyo ni salama na sahihi kuibua ugonjwa huo kwa watoto ikilinganisha na watu wazima.

Alisema, ugonjwa wa kifua kikuu unatibika kwa mtu aliyepata kuwahi Hospitali na kuanzishiwa dawa ambazo zinatolewa bure katika zahanati,vituo vya Afya na Hospitali zote hapa nchini.

Dkt Lymo, amewataka wazazi na walezi pindi wanapoona mabadiliko ya Afya kwa watoto wao ni vema kuwahi katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya uchunguzi.

Alisema, MDH inashirikiana na Serikali kupitia wizara ya Afya katika kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali hususani malaria,kifua kikuu,VVU na ukimwi,huduma bora za maabara na rasilimali watu katika sekta ya Afya.

Kwa upande wake mratibu wa kifua kiku katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, mwanzoni ilikuwa vigumu kuwatambua watoto wenye ugonjwa huo kwa kuwa walitumia njia ya kuwauliza maswali wazazi,hata hivyo haikuwa njia sahihi ya kubaini vimelea vya kifua kikuu kwa watoto.

Aidha, ameishukuru MDH kutuma wataalam wake kwenda kufundisha wauguzi na madaktari ambao wamepatiwa uwezo wa kufanya hunguzi wa TB kwa watoto kwa njia ya mpira, mpango ambao utakwenda kumaliza kabisa tatizo la maradhi ya ugonjwa huo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano katika wilaya hiyo.

Dkt Kihongole alisema, wahudumu waliopata mafunzo watapelekwa katika maeneo yote ili kutoa huduma kwa watoto, na litamaliza kasumba ya wazazi na walezi kupeleka watoto kwa Waganga wa Tiba asili na tiba mabadala pindi wanapoona mabadiliko ya afya kwa watoto wao.

Baadhi ya wazazi wamelishukuru shirika hilo kwa kupeleka huduma hiyo ambayo inakwenda kuokoa maisha ya watoto wengi hasa wale wanaopa maradhi ya kifua kikuu.

Wamepongeza mpango huo kwani utawezesha sana kuibua ugonjwa wa TB kwa watoto,kwani kila wanapokwenda Hospitali wakati mwingine wataalam walishindwa kutambua kwa vile walishindwa kupata makohozi kwa ajii ya vipimo.

Rukia Omari na Mwanahawa Musa wa Kijiji cha Misechela wameomba wataalam hao wafike kila kijiji kutoa huduma ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu na magonjwa mengine ambayo ni chanzo cha kupoteza maisha ya watoto wengi katika wilaya ya Tunduru.
 Mwezeshaji wa mafunzo ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kutoka shirika la MDH  Maliwaza Maganga kushoto akimchunguza  mtoto Afizuna Esabu(5)  vimelea vya kifua kikuu kwa kutumia njia mpya ya mpira wakati wa ufunguzi wa mpango wa matumizi ya mpira kwa watoto kubaini ugonjwa wa  kifua kikuu,uzinduzi uliofanyika katika zahanati ya Misechela wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,
 Mwezeshaji wa mafunzo kazini ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa watoto walio na umri  chini ya miaka mitano Malizawa Maganga kushoto na mganga Mkuu wa Zahanati ya Misechela Wilaya ya Tunduru Dkt Kingodom John wakimfanya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu mmoja wa watoto waliopimwa ugonjwa huo kwa njia ya mpira jana katika zahanati ya Misechela.
 Mwezeshaji wa mafunzo ya kifua kikuu kwa vitendo kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano Maliwaza Maganga kushoto akionesha mpira maalum unaotumika kupima vimelea vya ugonjwa huo  wakati wa ufunguzi wa mpango wa kupima na uchunguzi wa kifua kikuu kwa watoto uliofanyika katika zahanati ya Misechela Halmashauri ya wilaya ya Tunduru,wa pili kushoto Mganga mkuu wa Zahanati ya Misechela Dkt Kingdom John, katikati Meneja Progam na mafunzo wa MDH Dkt John Lymo na mratibu wa kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole.
 Meneja Program wa Shirika Usimamizi na Uboreshaji wa Huduma za Afya ngazi ya jamii(MDH) Dkt John Lymo kushoto na mratibu wa kifua kikuu na Ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole kulia wakimfanyia uchunguzi  Zanifa Omari(4)wakati wa kampeni ya Uchunguzi wa vimelea vya kifua kikuu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kwa njia ya mpira iliyoendeshwa na MDH kwa jushirikianao na Serikali ikiwa ni mara ya kwanza kupima ugonjwa huo kwa njia ya mpira,
Picha na Muhidin Amri


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2RZjo2P
via

Post a Comment

0 Comments