Ticker

10/recent/ticker-posts

Tanzania yashinda nafasi ya tatu kuogelea Afrika

Timu ya Taifa ya mchezo wa kuogelea (The Tanzanite) wakiwa katika pozi baada ya kushinda nafasi ya tatu katika mashindano ya Afrika ya Kanda ya Tatu yaliyomalizika Jumapili mjini, Nairobi, Kenya.

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam.  Timu ya Taifa ya mchezo wa kuogelea ya Tanzania (The Tanzanite) imeshinda kombe la Shaba katika mashindano ya Kanda ya Tatu Afrika yaliyomalizika jijini Nairobi, Jumapili jioni.

Tanzania iliyowakilishwa na waogeleaji  25 imemaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano hayo yaliyoshirikisha nchi tisa za Afrika kwa kukusanya jumla ya pointi 2, 044.50.

Wenyeji, Kenya ilimaliza katika nafasi ya kwanza kwa kupata pointi 2, 447.50 na kufuatiwa na Uganda iliyopata pointi  2, 392.

Mbali ya kushinda nafasi hiyo, waogeleaji watatu wa Tanzania, Sydney Hardeman, Romeo Mihaly na Sylvia Caloiaro walishinda vikombe kwa kushika nafasi ya kwanza kwa waogeleaji wa wenye miaka yao.

Sydney alipata pointi 130  kwa waogeleaji wenye miaka kati ya 11-12 wakati Romeo alikusanya pointi 118 katika umri huo huo na Sylvia alipata pointi 126.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, waogeleaji wa kike wa Tanzania waling’ara zaidi kwa kumaliza katika nafasi ya pili kwa kukusanya pointi 1,083 huku wenyeji, Kenya wakishika nafasi ya kwanza kwa kupata pointi 1,180  na Uganda katika nafasi ya tatu kwa kupata pointi 851.

Kwa upande wa wanaume, Tanzania ilikusanya pointi 865.5  na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Kenya iliyomaliza ya pili kwa kupata pointi 1, 143.50 na Uganda iliyokuwa ya kwanza kwa kupata pointi  1, 421.

 Matokeo yanaonyesha kuwa Afrika Kusini imeshika nafasi ya nne kwa kupata pointi 1, 540 wakati nafasi ya tano imekwenda kwa Zambia kwa kupata pointi  1,386 na Burundi ya sita kwa kupata pointi 866.

Waliokuwa mabingwa watetezi, Sudan imeshindwa kufukuta baada ya kushika nafasi ya saba kwa kupata pointi 812 huku Djibouti ikipata pointi 105 na  Malawi ikipata pointi  88.

Timu ya Tanzania iliundwa na waoegeleaji Maria Bachmann, Sylvia Caloiaro, Kayla Temba, Sydney Hardeman, Linnet Laiser, Sophia Latiff, Sarah Shariff, Avalon Fischer, Nawal Shebe, Roos Nevelsteen, Eunike Mathayo na Lissa Stanley.

Wengine ni Mischa Ngoashani,  Augustino Lucas, Romeo Mihaly, Delhem Rashid, Terry Tarimo, Aaron Akwenda, Singko Steiner, Ethan Alimanya, Sil Kleinveld, Ezra Miller,  Augustino Lucas,  Ashraf Moez, Nathan Kagoro, na Peter Itatiro.

Meneja wa timu hiyo  Hadija Shebe aliwapongeza waogeleaji hao kwa matokeo hayo mazuri pamoja na changamoto mbalimbali abazo zilisababisha baadhi ya waogeleaji kushindwa kushiriki.

Hadija alisema kuwa walipanga kuwa na waogeleaji 27, lakini waogeleaji wawili, Collins Saliboko anayesoma nchini Uingereza na Hilal Hilal anayesoma Dubai wameshindwa kushiriki kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wao.

 “Matokeo yanaonyesha jinsi gani Tanzania inafanya vyema katika mchezo huo na tunawaomba wadau watusaidie kwani bila wafadhiri, mchezo hauwezi kufikia hatua ya juu kabisa ya maendeleo,” alisema Hadija.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2rbVjuu
via

Post a Comment

0 Comments