Ticker

10/recent/ticker-posts

TRA YAKUSANYA TRILIONI 58.3 MIAKA MINNE

 Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Msafiri Mbibo akizungumza na Waandishi wa Habari (Hawapo Pichani), kuhusu Mafanikio ya TRA katika Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Tano , Mkutano ulifanyika leo Jumatatu (Novemba 25, 2019) Jijini Dar es Salaam.
  Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Msafiri Mbibo akizungumza na Waandishi wa Habari (Pichani), kuhusu Mafanikio ya TRA katika Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mkutano ulifanyika leo Jumatatu (Novemba 25, 2019) Jijini Dar es Salaam.

Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
MAMLAKA ya Mapato Tanzania  (TRA) imefanikiwa kuongeza mapato ya serikali kipindi cha miaka minne toka 2016 hadi 2019 kwa jumla ya sh.trilioni 58.3 ikilinganishwa ni miaka minne iliyopita ambapo ilikuwa shilingi trilioni 34.97.

Kwa miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, TRA imekuwa ikikusanya wastani wa shilingi trilioni1.3 ikilinganishwa na wastani wa shilingi bilioni 850 kabla ya awamu ya tano haijaingia madarakani.

TRA imesema kuwa kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba mwaka huu, wastani wa makusanyo umeweza kupanda  na kufikia kiasi cha shilingi trilioni 1.45 kwa mwezi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Msafiri Mbibo amesema kuwa, mafanikio hayo yametokana na msukumo wa serikali ya awamu ya tano  ya kuboresha mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

"Mafanikio haya yanatokana na msukumo wa serikali kuendelea kuboresha mikakati ya ukusanyaji wa mapato, kuibua vyanzo vipya vya kodi pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano wa TRA wa ukusanyaji wa kodi wenye dhamira ya kuongeza makusanyo  ya kodi za ndani ikiwemo kukuza ulipaji kodi wa hiari kutokana na Mazingira yaliyowekwa kwa wafanyabiashara" amesema Mbibo.

Mbibo amesema kuwa, sababu nyingine ya kuongezeka kwa makusanyo hayo ni pamoja na kuimarika kwa matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFD) baada ya kuondoka katika mfumo wa   stakabadhi zilizokuwa zikiandikwa kwa mkono.

"Mafanikio yametokana pia na uhamasishaji wa Mashine za EFD pamoja na kuboresha mifumo ya makusanyo yanayoendana na mazingira ya sasa ya ukuaji wa sayansi na teknolojia ili kuhakikisha walipa kodi wanalipa kwa urahisi kama ilivyo dhamira ya kurahisisha ulipaji kodi na kufanya mazingira kuwa bora na yanaokoa msongamano pamoja na muda," alibainisha Mbibo. 

Amewapongeza wafanyabiashara wote walioitikia wito wa Serikali kwa kutumia Mashine za Kielektroniki  za EFD bila kuwasahau wananchi ambao wamekuwa wakidai risiti kila wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.

Naibu kamishna Mkuu huyo amezungumzia mafanikio mengine kuwa ni ongezeko la mizigo kutoka nje ya nchi kupitia bandari za Dar es Salaam na udhibiti wa  makusanyo ya bidhaa zinazopaswa kulipiwa kodi na ushuru ziendazo nje ya nchi mfano zao la korosho na mazao ya ngozi na kwato.

Pia, mwezi Juni mwaka 2018 TRA ilianzisha Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki ulioanza kutumika rasmi  Januari 15 mwaka huu. 

Mbibo amesema kuwa, mfumo huo ni mbadala wa stempu za karatasi zakubandika ambazo zilikuwa zikitumika hapo awali.

Amefafanua kwamba,  lengo la kuanzisha mfumo huo mpya ni pamoja na kuongeza mapato ya serikali yanayotokana na ushuru wa bidhaa, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Kodi ya Mapato pamoja na kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ya kutokutendewa haki ya makadirio ya kodi zinazosimamiwa na TRA.

"Kutoka na utekelezaji wa mfumo huo kwenye eneo la pombe kali na mvinyo tu, TRA imekusanya ushuru wa bidhaa sh. bilioni 77.8 kwa kipindi cha mwezi Februari hadi Oktoba, 2019 sawa na ongezeko la sh. bilioni 19.6," alisema Mbibo. 

Mbibo ameongeza kuwa, "Kwa upande wa bidhaa za vinywaji laini yaani soda na vinywaji vingine visivyo vya kilevi ambapo matumizi ya mfumo huo yalianza Agosti, 2019, kwa mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu, TRA ilifanikiwa kukusanya sh bilioni 10 ukilinganisha na sh bilioni 9.2 zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka uliopita". 

Msafiri Mbibo ameeleza kuwa ni matumaini ya TRA kuwa jinsi mfumo huo utakavyoimarika na jamii kutambua unavyofanya kazi na umuhimu wake ndivyo mapato yatakavyoongezeka. 


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2OH45sq
via

Post a Comment

0 Comments