Ticker

10/recent/ticker-posts

Mhadhiri wa chuo aliyeomba rushwa ya ngono akiri shtaka, ahukumiwa, baada ya makubaliano na DPP

Na Karama Kenyunko, globu ya jamii
MHADHILI wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samson Mahimbo (69), amehukumiwa kulipa faini ya Sh. Milioni tano au kwenda jela miaka mitatu baada kukiri mashtaka yaliyokuwa yakimkabili likiwemo la kuomba rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi wake.

Hukumu hiyo imesomwa leo Novemba 26,2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya mshtakiwa kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ikiwamo kuomba msamaha na kukiri makosa yake.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema tabia ya rushwa ya ngono imekithili na ni gumzo katika vyuo hapa Nchini na kwamba inapaswa kukemewa.

Amesema, kitendo cha wanafunzi kuonyeshwa nyesha majibu kunapelekea kupata wataalamu wasiokuwa na viwango vinavyostahili hivyo njia sahihi ya watu kama mshtakiwa ni kukomesha vitendo Kama hivyo kwa kuwafikisha mahakamani na kuwapatia adhabu chungu. 
"Utalipa faini ya Sh.milioni tano au kwenda jela miaka mitatu" amesema Hakimu Shaidi.

Hakimu Shaidi ameongeza kuwa, kitendo alichofanya ni mshtakiwa huyo ni cha aibu kwa umri wake kwani mtu wa taaluma yake alipaswa kuwa mfano wa kuigwa lakini akaamua kujiingiza katika mapenzi na watoto wadogo ambao si hadhi yake.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo ameshailipa serikali fidia ya Sh.milioni mbili baada ya makubaliano hayo.

Mapema, Wakili wa Serikali Mkuu, Zakaria Ndasco amedai kuwa Jamhuri haina kumbukumbu ya makosa ya zamani ya mshtakiwa na kwamba tayari ameshalipa fidia ya Sh.milioni mbili.

Akitoa utetezi wake, kabla ya kusomwa  kwa hukumu hiyo, Wakili wa utetezi, Claudia Msando amedai mshtakiwa ana umri mkubwa na kwamba ameshaanza kupata maradhi yaa uzee ikiwamo kutokusikia na kuona vizuri na pia ni mstaafu na ana familia inayomtegemea.

Katika kesi ya msingi inadaiwa mshtakiwa  ambaye alikuwa akifundisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza 2015/16 aliomba rushwa hiyo kutoka kwa mwanafunzi Victoria Faustine.

Mwendesha Mashtaka wa taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukutu), Vera Ndeoya alidai kuwa Januari 12, mwaka 2017 katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Camp David, iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam mshtakiwa aliomba rushwa ya ngono.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo akiwa mwajiriwa wa NIT katika kozi ya Usimamizi wa Barabara na Usafirishaji namba LTU 07101 kwakutumia mamlaka yake alimlazimisha mwanafunzi huyo kutoa rushwa ya ngono.

Ilidaiwa kuwa, aliomba rushwa hiyo ili aweze kumfaulisha katika mtihani  wake wa marudio katika kozi ya Usimamizi wa Barabara na Usafirishaji anayosomea ya Januari 5, mwaka 2017.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2OJMz6G
via

Post a Comment

0 Comments