JAFO AWAHIMIZA WAGOMBEA KUCHANGAMKIA ZOEZI LA KUCHUKUA NA KURUDISHA FOMU

  Masama Blog      

Charles James, Michuzi TV

WAGOMBEA wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu wametakiwa kuhakikisha wanakamilisha zoezi la kuchukua na kurudisha fomu leo.

Akizungumza jijini Dodoma leo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amesema zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu lilikua la siku saba na linakamilika leo na hivyo kuwataka wagombea kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote leo.

Jafo amesema licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto kwenye maeneo kadhaa nchini lakini zoezi hilo limeenda vizuri kwa asilimia 80 jambo ambalo anaamini litachangia wananchi kupata wagombea kwenye maeneo yao na hivyo kuchagua viongozi walio bora.

Amesema tayari alishatoa maelekezo toka jana kwa wasimamizi wa uchaguzi huo kufungua vituo vya uchukuliaji fomu Nchi nzima kwa muda unaotakiwa ili kuwawezesha wagombea hao kupata haki yao ya msingi ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu.

" Ni kweli tumesikia malalamiko kwa baadhi ya maeneo kuwa wasimamizi wasaidizi wamekuwa wakifunga vituo lakini tayari nishatoa maelekezo yangu kwao kwamba wahakikishe wanafungua vituo ili watu wapate haki zao.

Zaidi ya asilimia 80 ya wagombea waliochukua fomu washazirejesha hii inamaanisha kwamba zoezi letu linakwenda vizuri na muitikio umekua mkubwa. Hatua inayofuata hivi sasa ni ya uteuzi kabla ya kwenda kwenye uchaguzi wenyewe," Amesema Waziri Jafo.

Amesema kati ya Kata 3659 ni asilimia 1.8 ya Kata hizo tu ndio ambapo kumekua na changamoto ya wagombea kuchukua na kurejesha fomu na kuwataka kutumia siku ya leo kumaliza changamoto hiyo.

" Kiukweli nimefarijika sana na namna zoezi hili linavyoenda, changamoto zimekua ni chache kulinganisha na mafanikio ambayo yamejitokeza toka hatua ya kwanza ya uandikishaji, ninaamini mwaka huu tutaweka rekodi ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kuhusu vyama vya Siasa kulalamika kuwepo kwa vitendo vya uvunjifu na vurugu kwenye baadhi ya maeneo niwasihi viongozi wao waweze kutoa taarifa kwa vyombo vyetu vya usalama ili kuweza kuchukua hatua zaidi," Amesema Mhe Jafo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo akizungumzia zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wagombea wa uchaguzi  wa Serikali Mitaa.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/32dZaE7
via
logoblog

Thanks for reading JAFO AWAHIMIZA WAGOMBEA KUCHANGAMKIA ZOEZI LA KUCHUKUA NA KURUDISHA FOMU

Previous
« Prev Post