Ticker

10/recent/ticker-posts

CBE YAPONGEZWA KWA USIMAMIZI BORA WA MAPATO NA UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
CHUO cha Elimu ya Biashara nchini (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam kimepongezwa kwa usimamizi bora wa mapato pamoja na uanzishaji wa kampasi mpya na uboreshaji wa miundombinu ya elimu.

Akihutubia katika mahafali ya 54 ya Chuo hicho Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi. Stellah Manyanya amesema kuwa Chuo hicho kimeendelea kupiga hatua mwaka hadi mwaka na hiyo ni pamoja na kuanzisha na kuboresha Kampasi mbalimbali na kubwa ni kwa kuwapokea wanafunzi wa ngazi za astashahada kwa kushirikiana na TAMISEMI.

Aidha Mhandisi Manyanya amekipongeza Chuo hicho kusimamia vyema mapato ya Chuo hicho.

"Nimefurahi kuwa Chuo changu hakiendekezi ufisadi na kwa mwaka huu mmepata hati safi kutoka ofisi ya CAG na mmeshika nafasi ya pili katika taasisi zinazosimamia manunuzi, hili ni jambo jema sana na ninawaomba muendelee ivyo ivyo" amesema.

Amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano inatambua mchango na mafanikio ya Chuo hicho na kuhusiana na Changamoto za miundombinu Serikali ipo tayari na tatizo hilo litatatuliwa.

Pia amekipongeza Chuo hicho kwa kutoa elimu ya biashara na ujasiriamali jambo ambalo litawasaidia wahitimu hao na amewashauri wahitimu hao kuvuka mipaka na kutumia vyema mitandao kwa kupenya katika masoko ya nje.

Pia Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema amesema kuwa maarifa yanayotolewa na Chuo hicho yameendelea kuleta na tija kwa watanzania na hadi kufikia sasa kuna wanafunzi wapatao 80000 katika Kampasi zote nchini.

Amesema kuwa katika mahafali hayo ya 54 asilimia 50.1 ya wahitimu hao ni wanawake waliohitimu katika ngazi za Astashahada, Shahada  na Shahada za Uzamili.

Prof. Mjema amesema kuwa wanaendelea kuboresha miundombinu katika kampasi zote na kwa sasa katika kampasi ya Dar es Salaam inajengwa maktaba kubwa ya kisasa yenye vyumba vya mihadhara na ofisi na itabeba wanafunzi 11000 kwa mara moja pamoja na ofisi 30 za walimu.

Pia ameishukuru Serikali kwa kutoa shilingi bilioni 1.5 ambazo zimetumika kununua iliyokuwa Shule ya New Hellen na sasa kuwa Kampasi ya CBE jijini Mwanza na kuahidi kuendelea kusimamia vyema Elimu ya Biashara nchini ili kuweza kujenga uchumi wa viwanda na kulipeleka taifa kwenye uchumi wa kati.

Akieleza Changamoto za Chuo hicho Makamu mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho  Prof. George Shumbusho amesema kuwa miundombinu bado haitoshelezi hasa katika Kampasi ya Mbeya.

"Miundombinu iliyopo iliandaliwa kwa kuwahudumia wanafunzi 600 pekee na hadi sasa tunahudumia wanafunzi zaidi ya elfu sita na licha ya Chuo kutumia mapato ya ndani bado changamoto ya miundombinu bado" ameeleza.

Pia ameishukuru Serikali kwa mchango wao na kuiomba kuendelea kushirikiana nao ili kuweza kuendeleza biashara na hiyo ni pamoja na kupatiwa fungu la maendeleo kutokana na uhitaji mkubwa wa fedha wa kuendeleza elimu ya biashara hatimaye kujenga uchumi wa kati na viwanda.
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi. Stellah Manyanya akizungumza na wahitimu wa chuo cha Elimu ya Biashara nchini (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam wakati wa  mahafali ya 54 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho leo jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara nchini (CBE) tawi la Dar es Salaam, Prof. Emanuel Mjema akisoma hotuba yake kwa mgeni rasmi na wahitimu waliofika kwenye mahafali ya 54 ya chuo hicho yalifanyika katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya wahitimu wakifuatilia hotuba ya  Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi. Stellah Manyanya wakati wa  mahafali ya 54 ya chuo cha Elimu ya Biashara nchini (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho leo.
 Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi. Stellah Manyanya akiwatunuku wahitimu Astashahada, Stashahada na Shahada waliofika kwenye mahafali ya 54 ya chuo cha Elimu ya Biashara nchini (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho leo.
  Baadhi ya wahitimu wakishangilia mara baada ya kutunukuwa Shahada  zao wakati wa  mahafali ya 54 ya chuo cha Elimu ya Biashara nchini (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho leo.

 Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi. Stellah Manyanya akiwatunuku baadhi  ya wahitimu Shahada ya Uzamili waliofika kwenye mahafali ya 54 ya chuo cha Elimu ya Biashara nchini (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho leo.
Picha za pamoja


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2qaSqKe
via

Post a Comment

0 Comments