DOWNLOAD APP YETU HAPA

TUZO YA AMANI YA NOBEL YA DKT. ABIY AHMED KATIKA TASWIRA YA AUNG SAN SUU KYI WA BURMA

  Masama Blog      
Ijumaa tarehe 11/10/2019 ilikuwa ni siku yenye furaha kwa waethiopia na waafrika kwa ujumla kufuatia ushindi wa tuzo ya Amani ya Nobel aliyopata Waziri Mkuu wa Ethiopia Dkt. Abiy Ahmed.

Tangu ameingia madarakani mwezi Aprili, 2018, ndani ya miezi sita Dkt. Abiy Ahmed alifanikiwa kuanzisha makubaliano ya amani na Eritrea, alitia saini kuachiwa kwa wafungwa mbalimbali waliofungwa kisiasa na kuomba radhi kwa umma  kwa ukatili uliokuwa ukifanywa na serikali ya Ethiopia hapo awali.

Mbali na hayo aliruhusu kurejea nyumbani kwa makundi mbalimbali ya waasi ambayo yalikuwa yakitambulika kama makundi ya kigaidi likiwemo kundi kubwa la waasi la Ginbot 7 lililokuwa limejificha Kusini mwa nchi hiyo.

Na hatimaye tarehe 9 Julai, 2018 Dkt. Abiy Ahmed na mwenzake Isias Afwerki wa Eritrea walitiliana saini mkataba wa kumaliza vita vya kugombea mpaka wa eneo la Kusini mwa nchi hiyo la Badme vilivyodumu kwa miaka 20 kuanzia miaka ya 1998-2000 mpaka 2018 mkataba ambao ulianza kutekelezwa rasmi mwezi Septemba, 2018.

Dkt. Abiy ameshiriki pia katika usuluhishi wa migogoro nchini Sudani na Sudani Kusini ingawa kushiriki kwake kunaonekana kama kunatokana ushawishi kutoka kwa mataifa ya Magharibi.

Tangu kuanguka kwa utawala wa Mengitsu Derg mwezi May mwaka 1991 Ethiopia imekuwa ikihangaika sana kurejesha Umoja wa Kitaifa.

Chama kinachotawala nchini Ethiopia cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF) ambacho ni muunganiko wa vyama vinne vya makabila ya Oromo, Ahmara, Tigri na wale wa kusini (OPDO, ANDM, TPLF na SEPDM)  kimekuwa na changamoto za kiuongozi kutokana na mgawanyiko wa makabila nchini humo.

Kwa mujibu wa mtandao wa indexmundi ni kwama kabila la Oromo ndilo lenye idadi kubwa ya watu katika nchi ya Ethiopia likiwa na asilimia 34.4%-36% ya idadi yote ya watu huku kabila la Ahmara likifuatia kwa asilimia 27%.

Makabila kama wasomali lina asilimia 6.2% ya idadi ya watu huku watigray (Tigrinya) wakiwa asilimia 6.1% na Sidama 4%.

Makabila yaliyobaki ambayo yanapatikana zaidi sehemu za Kusini mwa Ethiopia yana idadi ya watu chini wa asilimia mbili; Gurage (2.5%), Welaita (2.3%), Hadiya (1.7%), Afar (1.7%), Gamo (1.5%), Gedeo (1.3), Silte (1.3%), Kefficho (1.2%) na makabila mengine madogo zaidi yakijenga asilimia 8.8% ya watu wote.

Kutokana na mgawanyiko huo wa kimakabila na kisiasa ndani ya chama cha EPRDF ni wazi kuwa tuzo hii inaweza kuwa mwiba kwa baadhi ya wapinzani wake kisiasa na makabila kinzani.

Je ni nini anapaswa kufanya?

Dkt. Abiy Ahmed ana kazi kubwa ya kuitisha mjadala wa maridhiano ya kitaifa yatakayopelekea kuundwa kwa kamisheni ya ukweli ya kudumu na maridhiano ya kitaifa (NTRC)

Pili, ni muhimu kwake kuendelea kufanya mabadiliko katika serikali  yake kujumuisha makundi yote ya jamii yaliyoonekana kutengwa katika ngazi mbalimbali za uongozi nchini humo.

Kufanya haya ni muhimu kwake ili asije kujikuta anaingia kwenye kivuli cha kiongozi wa Myanmar au Burma bi Aung San Suu Kyi ambaye alishinda tuzo ya  Amani ya Nobel mwaka 1991 kwa harakati za kudai demokrasia na haki za binadamu  zisizoambatana na vurugu nchini Myanmar.

Lakini mara baada ya kufanikiwa kuwa kiongozi wa nchi hiyo bi Aung San Suu Kyi alijikuta katika shinikizo la jamii ya kimataifa kufuatia mauaji ya watu zaidi ya elfu kumi wa jamii ya Rohingya kutoka jimbo la Rakhine huku wengine zaidi ya laki saba wakikimbilia nchi jirani ya Bangladesh.

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) liliunda Tume Huru ya Kuchunguza Mauaji hayo (Fact Finding Mission) iliyoongozwa na Marzuki Darusman wa Indonesia ambayo ilitoa taarifa yake mwezi Septemba, 2018 na kushauri  viongozi watano wa juu wa jeshi (Tatmadaw) la Myanmar akiwemo Amiri Jeshi Mkuu Jenerali Mkuu Min Aung Hlaing na wenzake  walitakiwa kushitakiwa kwa makosa ya mauaji ya kimbari kwa mujibu wa Mkataba wa Rome wa mwaka 1998.

Ingawa ripoti ile haikumtaja bi Aung San Suu Kyi, mtu aliyekuwa akipigiwa chapuo sana na Marekani lakini bado jamii ya kimataifa iliendelea kumuhusisha na mauaji yale akiwemo Askofu Desmond Tutu aliyemshauri kuirejesha tuzo ile kwa kuwa nikono yake ilijaa damu ya warohingya.

Lakini mwenyekiti wa kamati ya tuzo ya Amani ya Nobel Berit Reiss-Andersen alimtetea bi Kyi kuwa tuzo yake haihusiani na mauaji ya kimbari ya 2017 kwa sababu aliipata mwaka 1991 kwa harakati za kudai demokrasia na haki za binadamu.

Haitapendeza kuona Dkt. Abiy Ahmed akiingia katika kivuli hiki ikiwa anaweza kujenga jamii inayopendana na kuheshimiana kwa misingi ya udugu na umoja wa kitaifa na si kama makabila ya Ethiopia.

Abbas Mwalimu (Facebook, Instagram & YouTube)

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook & WhatsApp)


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2nFTLar
via
logoblog

Thanks for reading TUZO YA AMANI YA NOBEL YA DKT. ABIY AHMED KATIKA TASWIRA YA AUNG SAN SUU KYI WA BURMA

Previous
« Prev Post