Ticker

10/recent/ticker-posts

ML 280 KUMALIZA KERO YA MAJI TUNDURU

Na Mwandishi Wetu,Tunduru

JUMLA ya shilingi milioni 280 zinatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika vijiji vinne vya kata ya Misechela Jimbo la Tunduru Kusini mkoani Ruvuma.

Mbunge wa Jimbo hilo Daimu Mpakate amesema hayo kwa nyakati tofauti wakati akiongea na wakazi wa kijiji cha Misechela na Mkaleka katika ziara yake ya kusikiliza kero na kuongea na wananchi wa vijiji mbalimbali katika jimbo lake.

Kwa mujibu wa Mpakate,Serikali kupitia wakala wa Maji vijijini imetenga kiasi hicho cha fedha ili kutekeleza mradi wa maji ambao mara utakapokamilika utawezesha kumaliza kabisa kero ya maji iliyokuwepo kwa muda mrefu.

Alisema, mbali na fedha hizo Ofisi ya Mbunge kuanzia Mwezi Novemba mwaka huu itaanza kazi ya kuchimba visima vifupi na virefu katika baadhi ya vijiji ambavyo vina tatizo kubwa la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Aidha alisema, wakala wa Bara bara mjini na vijijini(TARURA) wilaya ya Tunduru nayo imetenga shilingi milioni 118 kwa ajili ya ukarabati wa Bara bara ya Tunduru Mjini- Amani,Chiungo, Mea Mtwaro, Misechela na Bara bara ya Liwanga Misechela ambazo zimeharibika kutokana na mvua za masika.

Alisema, kazi hizo zitaanza mara baada ya kupatikana kwa Wakandarasi ambao watapewa dhamana ya kujenga miradi hiyo mikubwa katika kata ya Misechela na kata nyingine katika Jimbo la Tunduru Kusini,ambapo amewaomba wananchi wa vijiji vitakavyopitiwa na miradi hiyo kutoa ushirikiano kwa wakandarasi na kujiepusha na vitendo vya wizi ili iweze kukamilike kwa wakati.

Mpakate alisema, Ofisi ya Mbunge kupitia mfuko wa Jimbo kwa kushirikiana na Serikali ya awamu ya tano,imejipanga kuhakikisha inamaliza kero zote za wananchi ambazo zinakwamisha kuharakisha maendeleo na kuwataka wananchi wa jimbo hilo kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano.

Pia alisema, ili kuhakikisha wanafunzi hawapoteza muda wa masomo kwenda kutafuta huduma, yeye kama Mbunge amefunga mashine za kusaga nafaka kwenye shule za Sekondari 14 ili zitumike kusaga mahindi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi hasa baada ya kubaini kuwa wanafunzi wanatumia muda mwingi na kutembea umbali mrefu kwenda kusaga nafaka.

Alisema, katika utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo michango na nguvu za wananchi ni jambo la muhimu sana kwani fedha zinazotengwa na Serikali ni ndogo,kwa hiyo ni lazima wananchi wenyewe nao waanze kuchukua hatua ili serikali iweze kuwaunga mkono.

Katika hatua nyingine,Mpakate amewataka wenyeviti wa vitongoji,vijiji na watendaji wa vijiji kuwakamata wafugaji wanaoingiza mifugo yao katika maeneo yasioruhusiwa ili kuepusha kutokea migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa kuwa Serikali ya wilaya imeshatenga vitalu maalum kwa kwa ajili ya ufugaji.

Mpakate amewaonya viongozi wa vijiji kuacha tabia ya kuuza Ardhi kwa wageni, kwa lengo la kujipatia fedha badala yake kuwaelekeza wafugaji katika maeneo waliyotengewa.

Alisema, baadhi ya viongozi hao wamejiingiza katika biashara haramu ya kuuza na kutoa Ardhi kwa wageni wakiwemo jamii ya wafugaji ambao wamevamia kwa wingi katika vijiji mbalimbali wilayani Tunduru.

Alisema, Serikali haitawavumilia viongozi wanaojihusisha na suala la kuuza Ardhi kiholela na kuwataka viongozi wa umma kujiepusha na vitendo vya ukiukaji wa Sheria za Ardhi badala yake waendelea kuwahudumia wananchi kwa kutoa huduma Bora.

Alisema, baadhi ya tabia ya viongozi hao wana tabia ya kuwakamata wafugaji hata wakiwa bara barani na kuwatoza fedha ambazo haziendi Serikalini jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya Serikali.

“ ni lazima tufuate sheria hawa wafugaji ni Watanzania wenzetu,viongozi acheni kuwanyanya badala yake mnapo wakuta bara bara wakisafirisha mifugo waelekezeni maeneo yaliyotengwa,mkifanya hivyo wafugaji watakauwa tayari kuchangia shughuli zote za maendeleo katika vitongoji na vijijini vyenu” alisema Mpakate.
 Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini Daimu Mpakate kulia akiwasikiliza baadhi ya wenyeviti wa vitongoji wanaotuhumiwa kukubali kuingiza mifugo na kuuza Ardhi kwa Wageni katika maeneo yao bila kufuata sheria, wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero na kuongea na wananchi katika  jimbo lake,


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2AYdQvD
via

Post a Comment

0 Comments