MAHAKAMA KISUTU YAMHUKUMU ALIYEKUWA MHASIBU CHUO KIKUU HURIA KWENDA JELA MIAKA MITANO AU KULIPA FAINI YA SHILINGI MILIONI 700

  Masama Blog      
Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.

ALIYEKUWA Mhasibu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Engels Mrikaria amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani au kulipa faini ya Sh milioni 700 baada ya kukutwa na hatia  katika makosa ya kughushi na utakatishaji fedha zaidi ya sh. Milioni 500.

Pia mahakama imeamuru mshitakiwa huyo kulipa fidia ya Sh milioni 566.4 kama hasara aliyoisabisha  kwa chuo hicho. Pia Mahakama umeamuru kutaifishwa  kwa ardhi iliyopo mkoani Morogoro.

Kwa upande mwingine,  mahakama hiyo imewaachia huru mke wa Mrikaria, Lucy Mrikaria  Boniface Msofe, Stanley Msofe na Rose Maungu baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.


Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile amesema amezingatia ushahidi wa mashahidi 35 pamoja na vielelezo 48 amba uliletwa na upande wa mashtaka ambapo walimeweza kuthibitisha mashitaka dhidi ya Mrikaria ambaye ndie alikuwa akilipa mshahara kwa wafanyakazi wa OUT.

Amesema mshitakiwa amekutwa na hatia katika mashitaka 53 ya kughushi, saba ya utakatishaji fedha na moja la kuisababishia chuo hicho hasara ya Sh 566,446,500.

Hakimu Rwizile alisema katika mashitaka ya kwanza hadi ya 53, mahakama inamuachia huru mshitakiwa huyo kwa sababu amekaa rumande kwa miaka saba na kwa mujibu wa sheria  mashitaka ya kughushi kifungo cha juu ni kifungo cha miaka saba.

Akifafanua adhabu hiyo, Hakimu Rwizile amesema katika shtaka la utakatishaji fedha kila moja mshitakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 100 au kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Pia katika shtaka la kusababisha hasara mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitano jela na kulipa hasara ya Sh 566,446,500 alizosababisha kwa chuo hicho na kwamba adhabu za vifungo zitakwenda kwa pamoja. Hivyo atakaa jela miaka saba. "Pia mahakama inataifisha ardhi iliyopo mkoani Morogoro na kuhusu kiwanja kilichopo Arumeru mkoani Arusha mahakama haiwezi kukitaifisha kwa sababu bado haijajulikana kama kiliingia mikononi mwa mshitakiwa," amefafanua Hakimu Rwizile.

Ameongeza kuwa, kama upande wa mashitaka utataka mali hiyo itaifishwe basi ipeleke maombi ikiwa ni pamoja  na kuorodhesha mali zote wanazotaka zitaifishwe.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Theophil Mutakyawa ameiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine kwa sababu makosa aliyoyafanya ni makubwa.

Pia ameiomba mahakama kutoa amri y kuamuru mshitakiwa kulipa fidia ya hasara aliyosababisha na kutaifisha mali hizo.

Katika utetezi wake, mshitakiwa kupitia wakili wa Utetezi, Peter Kibatala ameiomba mahakama impunguzie adhabu mshitakiwa kwa sababu ni kosa lake la kwanza na kwamba tayari amekaa gerezani kwa miaka saba hivyo, asitengwe na familia yake.

Katika kesi hiyo inadaiwa kati ya Julai 2009 na Aprili 2011 mshitakiwa Mkaria alighushi nyaraka ya malipo ya mshahara na kuwatumia fedha watu mbalimbali kupitia akaunti za CRDB na NBC ambao hawakuwa wafanyakazi wa OUT.

Inadaiwa kati ya Julai 15 na 31, 2009 makao Makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), jijini Dar es Salaam, alighushi  nyaraka ya malipo ya mshahara (payroll) lengo kuonesha S. M January alilipwa mshahara wa Sh milioni mbili, B. J Msoffe (1,983,000) na A. Mrakari (1,603,000) wakati akijua sio wafanyakazi wa chuo hicho.

Katika mashtaka ya utakatishaji fedha, inadaiwa Julai 2009 na Aprili  Mrikaria na mke wake, walijipatia  28,776,750 zilizoingia kwenye akaunti ya familia kama mshahara.

Pia inadaiwa mshitakiwa aliingiza fedha kwenye akaunti ya Kampuni ya Kyungu Hill kama mshahara.

Aidha, Aprili 2011 maeneo ya Dar es Salaam na Dodoma mshtakiwa alijipatia shamba lenye ekari 130 katika Kijiji cha Muungano kilichopo Kongwa mkoani Dodoma fedha ambazo zililipwa na chuo hicho kama mshahara kupitia akaunti zake. Anadaiwa kununua kiwanja Kijiji cha Kiharaka kilichopo Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, pia alinunua kiwanja kilichopo Kijiji cha Meru wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Kati ya Julai 2009 na Aprili 2011 maeneo ya jiji la Dar es Salaam, Mrikaria alisababisha hasara ya 566,446,500 kwa chuo Kikuu huria (OUT).


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2ppKmoo
via
logoblog

Thanks for reading MAHAKAMA KISUTU YAMHUKUMU ALIYEKUWA MHASIBU CHUO KIKUU HURIA KWENDA JELA MIAKA MITANO AU KULIPA FAINI YA SHILINGI MILIONI 700

Previous
« Prev Post