Ticker

10/recent/ticker-posts

Marehemu ahukumiwa jela miaka mitano

Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemhukumu aliyekuwa Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Godfrey Majuto ambaye ni marehemu sasa, kulipa faini ya Sh milioni 3.6 au kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Hiyo ni baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu ya kupanga ya uhujumu uchumi, baada ya Majuto na wengine wanne kushtakiwa kwa kosa la kuisababishia Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda hasara ya Sh 61,157,342. 

Aidha, mahakama hiyo imeamuru yeyote atakayeteuliwa kuwa msimamizi wa mirath ya marehemu Majuto atalipa faini ya Sh milioni 3.6 ili fedha hiyo iingine serikalini.

Mbali na Majuto, washitakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Naomi Nko ambaye wakati huo alikuwa ni Kaimu   Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Peter Mwanoni, Beatus Bisesa, mkandarasi na Chiyando Matoke.

Ilidaiwa mahakamani hapo na  Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Katavi, Bahati Haule, kuwa  washitakiwa hao walitenda kosa hilo la kuhujumu uchumi kwa nyakati tofauti.

Alidai walitenda kosa hilo Januari 2, 2012 wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Mpanda wakidai kuandaa hati ya malipo ya uongo ya kutaka kuonyesha sehemu ya Barabara ya Kasokola kwenda Mtapenda kuwa imetengenezwa kwa gharama ya Sh 64,376,152 wakati si kweli.

Katika kosa la pili lililowahusu washitakiwa wa kwanza hadi wa tatu,  walishtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi kwa kupitisha malipo hayo kwa Kampuni ya Matoke huku wakijua barabara hiyo haikujengwa kwa gharama hiyo.

Haule alidai kuwa shitaka la tatu  liliwahusu washitakiwa wote watano  walioshitakiwa kwa kosa la kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya Sh 61,157,342.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili za  mashitaka na utetezi, Hakimu Luoga, aliiambia mahakama hiyo kuwa washitakiwa wa kwanza, wa tatu na wa nne wamepatikana na hatia katika kosa la  kwanza huku Majuto naye ametiwa hatiani katika kosa la pili na la tatu.

Pia washtakiwa akiwamo wa pili na wa tano hawakutiwa hatiani kwa kosa lolote lile na waliachiwa huru.

Baada ya maelezo hayo, Haule aliiomba  mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa washitakiwa kwa kuwa wameisababishia  hasara Serikali.

Akisoma hukumu hiyo, Luoga alisema   pamoja na mahakama kupokea hati ya   kifo cha Majuto kilichotokea Desemba 4, mwaka huu huko Songea ambako    alikuwa akifanya kazi kama Meneja wa  Tarura wa Manispaa ya Songea, alikohamia kabla ya mauti hayajamfika alikuwa ameshatoa utetezi wake mahakamani hivyo hakuwa na sababu ya kuifanya mahakama ishindwe kutoa adhabu kwake.

Luoga alisema katika shitaka la kwanza   Majuto akiwa na washitakiwa wa tatu na wa nne wamepatikana na hatia ya kifungu cha Sheria namba 22 ya kupambana na rushwa ya mwaka 2007, hivyo wameadhibiwa kulipa faini ya Sh 600,000 kwa kila mmoja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Katika kosa la pili na la tatu limemtia  hatiani Majuto peke yake na kosa la pili  kwa mujibu wa Sheria namba 31 sura  namba 11 ya mwaka 2007, amehukumiwa kulipa faini ya Sh 1,000,000 au kifungo cha miaka mitatu jela.

Katika kosa la tatu, Majuto chini ya  kifungu cha Sheria namba 57 (1)na kifungu namba 60 (1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, makosa ya kupanga, sura 200, marejeo ya 2002 amehukumiwa kulipa faini ya Sh 2,000,000 au kifungo cha miaka mitano jela.

Hakimu Luoga alisema hukumu hiyo amekukumiwa Majuto na mahakama inaagiza yeyote atakayeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu alipe faini hiyo ili fedha hizo ziende serikalini.


from MPEKUZI http://bit.ly/2VbHQxc

Post a Comment

0 Comments