Ticker

10/recent/ticker-posts

Nick wa Pili: Hatumminyi Lord Eyez, Bado Amesimamishwa

Nick wa Pili amekanusha madai yaliyowahi kutolewa na rapper Lord Eyez dhidi ya member wengine wa Weusi kuwa wamekuwa wakimminya.

Akizungumza na mtangazaji wa Jembe FM, JJ, Nick ambaye ni msemaji wa kundi/kampuni hiyo, amesema Lord Eyez bado amepigwa benchi. “Kama umesimamishwa unawezaje kusema unaminywa? Yaani mwanafunzi kama umepewa suspension utasemaje tena shule inakuminya wakati wewe uko suspended?” amehoji Nick.

“Kila kitu kinaendeshwa kisheria, kwahiyo unaposema unaminywa kuna watu wanavunja sheria na yeye anaelewa kabisa kanuni na taratibu za kampuni, hakuna hata mtu mmoja aliyepo kwenye nafasi ya kuvunja sharia kumkandamiza mtu mwingine, kitu kama hicho hakiwezekani,” ameongeza rapper huyo.

Akiongea kwenye kipindi cha XXL cha Clouds FM, mwanzoni mwa October, 2016, Lord Eyez alisema akiwa mmoja wa waasisi wa kampuni hiyo, atakuja kueleza zaidi ya ndani yanayoendelea. Alidai kuwa makubaliano ya kampuni hiyo ni kuwa member asiyepanda kutumbuiza hapati mkate wake, na yeye kwakuwa hahusiki sana na show zao amekuwa akiambulia patupu.

“Kimuziki uhusiano wetu na Weusi mimi Joh Makini Gnako na Nick wa Pili tupo vizuri ila kwenye maslahi kuna kuminywa sana,” alisema. Rapper huyo aliyewahi kung’ara enzi za Nako 2 Nako, alipanda kwenye show ya Fiesta jijini Arusha baada ya kualikwa na Barakah Da Prince. 4

“Nilipanda na Barakah Da Prince kwasababu Barakah ndiye aliyeona umuhimu wangu mimi kuwepo Arusha. Alinifata nikiwa bado sijapokea simu ya mtu yeyote,” alisema.

“Kuna watu waliingilia kati kuweka zengwe nisitumbuize na Barakah lakini nilifanikisha kwa kishindo.”

December mwaka jana hata hivyo alipohojiwa kwenye kipindi cha Planet Bongo cha EATV, Lord Eyez alikuwa na hadithi tofauti. Alisema bado yupo fresh na kundi hilo na anatarajia kuachia ngoma mbili, ‘Hardcore’ na ‘Shida Mpya’ alizomshirikisha member wa kundi hilo G -Nako.

“Lord Eyez bado nipo na nilikuwa na napikapika vitu,” alisema. “Juzi kati nilikuwa na G-Nako tukiwakilisha Weusi kampuni na sasa hivi tayari tumeandaa kazi mbili, moja inaitwa Hardcore na nyingine Shida Mpya,” aliongeza.

“Kwahiyo nawaambia mashabiki wangu wakae mkao wa kula, nataka nifunge mwaka halafu nifungue kwa kasi kwa sababu nataka mwaka 2016 uwe mwaka wangu.”