Ticker

10/recent/ticker-posts

Pinda Aeleza Hali ilivyokuwa Lowassa Akijiuzulu...Asema 'Hakuna Aliyetegemea'

 


Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema hakupata nafasi ya kukutana ana kwa ana na Edward Lowassa kuzungumza naye kitu chochote baada ya kutangaza kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu bungeni Jijini Dodoma.


 Pinda amesema hiyo ilitokana na hali ilivyokuwa baada ya Lowassa kutangaza uamuzi huo bungeni, kwani hakuna mtu aliyetegemea.


Ameeleza haya jana Jumanne, Februari 13, 2024 nyumbani kwake Zuzu jijini Dodoma, alipotembelewa na Mwananchi Digital kuzungumzia namna alivyoguswa na kifo cha Lowassa.


Amesema pia hakutegemea kuwa angeteuliwa kurithi nafasi ya Lowassa, hivyo ilikuwa ngumu kidogo kupokea taarifa za uteuzi huo.


“Sikupata nafasi ya kuongea naye tangu ile taarifa ya kujiuzulu nilipoiskia. Nilishtuka kwa sababu nilikuwa nimemzoea alikuwa kiongozi wangu kwa mda mrefu, sikujua vilevile kama mimi ndio nitakuja kuvaa viatu vyake,” amesema Pinda.


Hata hivyo, amesema baada ya uamuzi huo alilazimika kushika kijiti alichoachiwa na kwamba haikuwa ngumu kwake kutokana na ukaribu wao wa kiuongozi na alikuwa akifahamu vitu vingi, hivyo ilikuwa rahisi kuendeleza mengi aliyoyaacha.


Pamoja na hayo, Pinda alimsifu Lowassa kwa kutoa wazo na kulisimamia la kujenga ofisi na makazi ya waziri mkuu kwenye eneo la Mlimwa C, jijini Dodoma.


“Yeye ndiye alikuwa mwanzilishi wa jambo lile, kwanza kinadharia lakini pia baadaye katika kutekeleza na hata alipofikia hatua ya yeye kujiuzulu alilitetea wazo lake,” amesema.


Aidha, Pinda amesema msiba wa Lowassa umemkumbusha mengi aliyoyafanya hususan kuimarisha na kuijenga CCM, kwani alikuwa mfano bora kwa wanasiasa wengi hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments