Ticker

10/recent/ticker-posts

Waziri Jerry Silaa Aanza Kutekeleza Maagizo Haya ya Mwenezi CCM Paul Makonda



Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa ameanza utekelezaji wa maagizo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yaliyotolewa na Katibu wa Nec Itikadi, Uenezi na mafunzo, Paul Makonda ambaye alisema chama hicho kinampa miezi miwili awe amemaliza migogoro ya ardhi mkoani Dodoma.

Novemba Mosi mwaka huu, alipokuwa akipokelewa Jiji Dodoma, Makonda alisema dhuluma ya ardhi imewafanya baadhi ya watu kutamani kujiua na wengine wakijilaumu kwa nini walizaliwa jijini humo.

“Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa nakupenda na nakuheshimu lakini hapa nilipo sio heshima yangu, si matakwa yangu tena, chama kinakupa miezi miwili hadi Desemba mwaka huu, tusisikie mwananchi wa Dodoma wanalia juu ya ardhi,” amesema.

Amesema itakapofika Januari Mosi mwakani, watu wawe wanakula sikukuu ya mwaka mpya hawana migogoro tena migogoro ya ardhi.

Akizungumza leo Jumamosi Novemba 4, 2023, Silaa amesema kuwa ofisi yake imeanzisha kliniki ya ardhi ambayo itawawezesha wananchi kupata huduma mahali pamoja.

“Namwelekeza Katibu Mkuu, mikoa yote watoke maofisini wakasilikize wananchi. Mimi mwenyewe Jumatatu baada ya vikao vya Bunge mchana nitakuwa hapa ili wale wananchi wenye matatizo ambao wanasema kuwa lazima nimuone waziri wamuone bila kuweka ahadi,” amesema.

Silaa amesema wamejipanga kuhakikisha kuwa matatizo ya ardhi ya nchi nzima yanamalizika na kwamba wanatekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kufanyika kwa mabadiliko ya kiutendaji katika maeneo yao.

Amesema moja ya hayo ni kuanzisha eneo ambalo mwananchi ataweza kupata huduma zake za ardhi mahili pamoja na ofisi zao zitakuwa za kisasa.

“Pale ambapo hatuhitaji kuwa na vyumba vingi vingi kutakuwa wazi ili kuweka uwazi katika huduma zetu. Usije ukajifungia ofisini ukamwambia mteja naomba fedha ili ushughulikie tatizo lake,” amesema.

Amesema kuongeza uwazi watafunga kamera katika ofisi zao zote ili kila kinachofanyika katika maeneo hayo kiweze kuonekana kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Antony Sanga.

“Tunafanya hivi kuhakikisha kuwa maelekezo mahususi anayoyatoa Rais Samia Suluhu Hassan lakini na maelekezo yanayotolewa kwa wizara yanatekelezwa,” amesema.

Aidha, Silaa amesema kuwa Jiji la Dodoma limepokea Sh4.5 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia katika maeneo ambayo wameyatwaa kupima viwanja.

Mmoja wa watu waliofika kupatiwa huduma katika kliniki hiyo, Asha Abdalla ameshauri huduma hiyo iwepo kila mwezi ili kuondoa usumbufu kwa wananchi ambao wamekuwa wakisumbuka sana kutafuta haki.

“Sisi wananchi tumekuwa tukisumbuka sana kama mimi nimezunguka sana kufuatilia suala langu la kuingia katika mfumo wa ulipaji wa kodi ya ardhi. Mara nenda huku nenda huku,” amesema.

Post a Comment

0 Comments