Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 8 wa wahandisi wanawake nchini.
Alisema mchango wa wanawake katika sekta mbalimbali nchini hivi sasa ni mkubwa ambapo msukumo maalumu unahitajika kuona kundi hilo linashiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa na kuleta maendeleo.
Alisema kwa sasa wapo jumla ya wahandisi 40 wanawake katika taasisi hiyo wakifanya kazi katika mikoa 26 ya Tanzania Bara ambapo wote kwa ujumla wameonesha ufanisi mzuri wa utekelezaji wa majukumu yao.
Alizitaja hatua wanazozichukuwa kwa sasa ni pamoja na kuwahamasisha kuwapa moyo zaidi ya kujiendeleza katika kozi mbalimbali ili waweze kwenda kufanya kazi na kuchukuwa nafasi katika maeneo mbalimbali ikiwemo mikoani.
"Kwa mfano bado nafasi nyingi za ngazi za umeneja katika mikoa mbalimbali zinashikiliwa na wanaume ambapo kwa sasa wamejipanga vizuri kutoa msukumo unaostahiki kwao", alisema.
Mapema Mhandisi Seff alisema TARURA inaendelea na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuzifanyia matengenezo barabara zilizopo vijijini ili kupitika na wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo.
Alisema kwa kushirikiana na wadau katika ujenzi wa barabara wamefanikiwa kujenga zaidi ya barabara zenye urefu wa kilomita 144,000 zikijumuisha barabara za wilaya kuweza kutumiwa na wananchi na kurahisisha shughuli za maendeleo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila ambaye pia ameshiriki katika mkutano huo amesema wao kama Wizara wanaipongeza TARURA kwa kuwa na nia ya dhati ya kuhakikisha wanawapa nafasi na kuwajengea uwezo zaidi wahandisi wanawake ili waweze kuwa katika nafasi muhimu za maamuzi hivyo wizara itatoa ushirikiano kwa ajili ya kuisaidia TARURA katika kufikia lengo hilo.
Katika maonesho hayo Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi akifuatana na viongozi wa serikali alipata nafasi ya kutembelea banda la Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kupata maelezo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala.
0 Comments