Ticker

10/recent/ticker-posts

MHANDISI ROGATUS MATIVILA AKAGUA BARABARA ZA TARURA MKOANI IRINGA, AMSHUKURU RAIS SAMIA


Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Miundombinu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Reagatus Mativila amefanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa barabara zilizo chini ya TARURA zilizopo mkoani Iringa ambazo ni Mtili-Ifwagi Km 14, Wenda-Mgama Km 19, Sawala-Lulanda Km 10.4 zinazojengwa kwa kiwango cha lami.

Akiwa katika ziara hiyo, Mhandisi Mativila ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Mtili-Ifwagi utagharimu Shilingi Bilioni 21.7 na utachukua muda wa miezi 15 kukamilika, barabara ya Wenda-Mgama gharama yake ni Shilingi Bilioni 29.9 utachukua miezi 18 kukamilika na barabara ya Sawala-Lulanda itagharimu takribani Shilingi Billioni 9 na itakamilika mapema mwaka 2024.


Mhandisi Mativila amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa barabara za vijijini ili kuchochea uchumi katika maeneo ya uzalishaji wa vyakula na mazao ya kibiashara.

"Nimekuja kutembelea na kujionea ujenzi wa barabara hizi, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo ambao ni Benki ya Dunia kwa kutoa mkopo wa masharti nafuu kwa Serikali ya Tanzania kwaajili ya ujenzi wa barabara hizi muhimu ambazo zinaingia kwenye maeneo ya uzalishaji mkubwa wa mazao ya misitu na mazao ya vyakula", alisema Mhandisi Mativila.

Aidha Mhandisi Mativila aliongeza kuwa barabara hizo zitanufaisha wananchi wa maeneo hayo na taifa kwa ujumla kwani itasaidia kukuza uchumi.


Naye Meneja wa TARURA Mkoa wa Iringa Mhandisi Makori Kisare alisema kama Mkoa wanamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha kwa ujenzi wa barabara zilizo chini ya TARURA na kuahidi kuendelea kusimamia vizuri fedha za Serikali zinazotumika katika ujenzi wa barabara.

Pia Mhandisi Makori amewashukuru wananchi katika maeneo ambayo mradi unapita kwa kuwa tayari kutoa maeneo yao ili kupisha ujenzi wa barabara.

Nao baadhi ya wananchi ambao ni wanufaika wa mradi huo wameipongeza serikali kwa kuwaona na wamesema kuwa wameupokea vizuri mradi huo.

Post a Comment

0 Comments