Ticker

10/recent/ticker-posts

WANANCHI HOMBOLO MAKULU-DODOMA WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI

Wananchi wa Kata ya Hombolo Makulu wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma ambayo imesaidia kuwapunguzia mwendo wanafunzi wa Shule waliokuwa wanatembea umbali mrefu kufuata Sekondari Hombolo Bwawani.

Shukrani hizo zimetolewa leo katika mkutano wa wazazi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma ambao umehudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh.Anthony Mavunde ambaye pia alitumia fursa hiyo kukabidhi vitabu  1667 kwa ajili ya Shule alivyoviomba kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania.

“Shule hii ni moja kati ya shule zilizojengwa


kila kata nchini chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye tunamshukuru kwa maono yake makubwa kwenye sekta ya elimu.

Watoto wa hapa walikuwa wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya 19 kufuata Shule kata ya Hombolo Bwawani lakini sasa wanasomea hapa hapa,haya ni maendeleo makubwa.

Nimesikia changamoto zenu za nguzo za umeme kufika hapa eneo la shule hili nitalishughulikia na tutawasha umeme,pia kuhusu vifaa vya michezo kesho nitawaletea magoli ya chuma,jezi na mipira na pia nitachangia Tsh 2,400,000 kwa ajili ya malipo ya walimu wanaojitolea”Alisema Mavunde

Akitoa taarifa ya awali Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Livinus Tanganyika amesema shule hiyo ambayo imeanza Oktoba,mwaka 2022 imejipanga kuhakikisha inatoa elimu bora ili kuwaandaa wanafunzi kutoa mchango wao kwa ustawi wa Taifa Tanzania.

Naye Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Hombolo Mh. Janeth Kutonha ameishukuru serikali kwa ujenzi wa shuke hiyo pamoja na Mbunge Mavunde kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele kwenye shughuli za maendeleo.

Post a Comment

0 Comments