Ticker

10/recent/ticker-posts

BENKI YA KILIMO YATOA BILIONI 2.8 KUSAIDIA VYAMA VYA MSINGI VINAVYOLIMA MAHINDI RUVUMA


BENKI ya maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) katika msimu wa kilimo 2019, imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 2.8 kwa vyama sita vya msingi vya Ushirika vyenye wanachama 922 vinavyojihusisha na kilimo cha mahindi mkoani Ruvuma.


Mkurugenzi Mtendaji wa TADB  Japhet Justine amesema hayo jana alipokuwa akielezea mikakati ya Benki hiyo kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme  wakati wa ziara yake kukagua shughuli za kilimo cha zao hilo  zinazofanywa na wanachama wa vyama  vya msingi vya Ushirika mkoani Ruvuma vinavyopata mkopo kutoka Benki hiyo.



Aidha Justine alisema,  Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania  msimu wa kilimo 2020 itaongeza idadi ya vyama  kutoka 6 vya sasa hadi kufikia  18  na imeshatoa bilioni 1.6 kama mkakati wake wa  kuongeza uzalishaji  na kuinua uchumi wa wakulima wa mahindi mkoani Ruvuma.



Alisema,huu ni mwaka wa pili kwa  TADB Tanzania kuwapatia  mbegu,mbolea pamoja  kuwatafutia soko wakulima wa mahindi  ili kuongeza mnyororo wa thamani ambao umewasaidia kuongeza uzalishaji na kupunguza umaskini katika familia zao.



Kwa mujibu wa Japhet, katika msimu huu tayari wakulima wa vyama hivyo  wameshapata mkopo wa Mbegu  na mbolea kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa kilimo wa 2019/2020.



Pia alisema,  baada ya kufanya vizuri katika zao la mahindi Benki hiyo inakusudia kuwafikia  wakulima wa zao la kahawa  wa wilaya ya Mbinga ili nao waweze kunufaika na Benki hiyo ambayo ni kiungo muhimu kwa wakulima  na taasisi nyingine za fedha.



Alisema mbali na kusaidia kuongeza  mnyororo wa thamani  kwenye zao la mahindi,  TADB inawaunganisha wenye viwanda  na wakulima kwa ajili ya kupata bidhaa jambo lililo saidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo  na kuondoa tatizo la soko la mahindi kwa wakulima.



Ametoa wito kwa wafanya biashara  mkoani Ruvuma ,kuchangamkia fursa  hiyo kwa kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao na Benki hiyo iko tayari kushirikiana nao kwa kutoa ushauri na mitaji kwa kushirikiana na Benki nyingine zilizopo hapa nchini.



Aidha,ameipongeza Serikali ya mkoa wa Ruvuma kutokana na juhudi kubwa inazofanya  ya kushauri na kusimamia suala zima la kilimo,  na kuufanya mkoa huo  kuongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biasahara hapa Nchini.



Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameishukuru Benki ya maendeleo ya kilimo  kwa kazi nzuri inayofanya kusaidia mnyororo wa thamani kwa zao la mahindi  jambo lililosaidia kuongeza  uzalishaji wa mazao kutoka tani milioni 1.4 mwaka 2018 hadi kufikia tani milioni 1.6 mwaka 2019.



Alisema, Serikali ya mkoa itaendelea kuwasaidia wakulima kwa ushauri ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao ili kuinua hali zao za maisha, ambapo  ameiomba Benki hiyo kufungua tawi lake mkoani hapa ili wakulima wengi waweze kufikiwa kwa karibu na huduma zake  na Serikali  ya mkoa  itatoa ushirikiano katika mchakato mzima wa uanzishwaji wake ikiwemo kutoa ofisi.



Alisema, asilimia 96  ya wakazi wa mkoa wa Ruvuma ni wakulima na wanategemea sana kuendesha maisha yao kupitia shughuli za kilimo,kwa hiyo mkoa huo unahitaji sana  Benki ya TADB kuwaunga mkono kwa hali na mali ili waendelee kuzalisha.



Mndeme, ameiomba Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania kuuangalia mkoa huo kwa jicho la huruma  kutokana na kazi nzuri inayofanya  katika uzalishaji wa zao la mahindi na mazao mengine kama mbaazi,ufuta,korosho,soya,maharage kwa  TADB kufungua tawi  ili kusaidia shughuli za kilimo.



Mkuu wa mkoa alibainisha kuwa,kipaumbele cha mkoa huo ni uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na samaki ambao wanapatikana kwa wingi katika ziwa nyasa ambapo mwaka 2019 mkoa ulitenga hekta milioni 1.6 kati ya hekta milioni 3.3 zinazofaa kwa shughuli za kilimo.



Pia Mndeme ameiomba Benki hiyo kusaidia kufufua kiwanda cha kusindika zao maarufu la Tumbaku kwani kama kitarudi katika hali yake na kufanya kazi, zao la Tumbaku litapata soko la uhakika sambamba na kutoa ajira kwa watu wapatao 350 na hivyo kuinua maisha ya wananchi na uchumi wa mkoa huo.



Mmoja wa watu walinufaika na mkopo wa Benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania John Mgogo anayemiliki kiwanda cha Real World Ltd kinachozalisha bidhaa za Ample ameishukuru Benki hiyo kwani imesaidia sana kutimiza yake ya kumiliki kiwanda.
Alisema,  kwa sasa kiwanda hicho kinachakata chakula cha mifugo kama kuku,nguruwe na samaki na kina uwezo wa kuzalisha tani kumi kwa siku.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania Japhet Justine katikati, akiangalia mahindi yaliyoletwa katika  kiwanda cha Real World Ltd kilichopo Lilambo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na baadhi ya vyama vya msingi vya Ushirika wilayani Songea vinavyopata mkopo kutoka Benki hiyo kwa ajili ya kazi ya kuchakata,kulia Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme na kushoto Meneja wa kiwanda hicho John Mgogo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme kulia akimuonesha jana Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya maendeleo ya Kilimo Nchini Japhet Justine unga  wa mahindi uliochakatwa katika kiwanda cha Real World Ltd Lilambo mkoani Ruvuma,wakati wa ziara ya Mkurugenzi wa Benki ya maendeleo ya kilimo kutembelea vyama vya msingi vya ushirika vinavyopata mkopo kutoka kwa Benki hiyo ambapo mwaka 2019 TADB ilitoa zaidi ya shilingi Bilioni 2.8 kusaidia vyama sita vya msingi katika mkoa wa Ruvuma.kushoto meneja wa kiwanda hicho John Mgogo.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2ZYojmL
via

Post a Comment

0 Comments