WASICHANA WAASWA KUTOPOKEA ZAWADI AMBAZO ZITAHATARISHA MAISHA YAO

  Masama Blog      
WASICHANA Mkoani Tabora wametakiwa kuwa na ujasiri wa kusema hapana pindi wanaposhaushiwa na wanaume kupokea zawadi kwa lengo la kuwataka wajiingize katika vitendo vya kujamiana ambavyo vinawaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vinavyosababisha UKIMWI.

Kauli hiyo imetolewa juzi wilayani Igunga  na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu wakati wa maadhimisho ya UKIMWI Duniani ambapo kimkoa yalifanyika wilayani humo ambapo kauli mbiu ilikuwa Jamii ni chachu ya mabadiliko , tuungane kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI.

Alisema wanapochukua  zawadi zenye hila na kupakizwa katika vyombo mbalimbali vya usafiri wanakuwa wamejiingiza katika mtego wa kudaiwa jambo ambalo litawaingiza katika vitendo vinavyo hatarisha maisha yao.

“Ukizoea kupokea zawadi na kupewa ‘rift’ za magari na pikipiki , ipo siku na wewe utaombwa ‘rift’ ndipo kitakuwa chanzo cha kujiweka katika hatari na kupata maambuzi ya UKIMWI na wakati mwingine kupoteza ndoto yako ya kupata elimu” alisisitiza.

Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliitaka jamii kuendelea kuzingatia ushauri na elimu wanayopata ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa ajili ya kujikinga wao na familia zao na kuwa na jamii yenye afya njema.

Alisema maambukizi ya VVU yamekuwa na athari kubwa ya kiuchumi na hata watoto wengine wanalazimika kuacha masomo kwa ajili ya kuwahudumia wazazi wao na wengine kujiingiza katika utumikishwaji kwa sababu ya kutafuta fedha za kuwasaidia wadogo wao waliachwa na wazazi.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo alisema katika kukabiliana na kuenea kwa maambukizi mapya miongoni mwa Wanafunzi wa Shule za Sekondari wilayani humo amepiga marufuku sherehe za wanafunzi ambazo sio rasmi ambazo zinawachochea kufanya vitendo viovu.

Alisema kumezuka utaratibu ambao ni hatari kwa baadhi ya wanafunzi wanaohitimu Kidato cha Nne na Sita kuchangishana fedha na kukodi kumbi na vyumba kwa ajili kuwafanya sherehe ambayo hata walimu na wazazi hawana taarifa.

Mwaipopo alisema katika sherehe hiyo ambayo sio rasmi kuna vitendo hatari vinafanyika humo ambavyo vinaweza kuwasababisha kupata maambukizi ya VVU.
Baadhi ya wakazi wa Igunga mjini wakiwa wamejipanga mstari kwa ajili ya kuchunguza afya zao ikiwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani juzi ambapo kwa Mkoa wa Tabora imefanyika Igunga.
Mratibu wa Kifua Kikuu na UKIMWI wilaya ya Igunga, Dkt. Joachim Kabeya akitoa maelezo kwa Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu (mwenye skafu) juu ya zoezi linaloendelea la upimaji Kifua mjini Igunga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani. Imeandikwa na TIGANYA VINCENT.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2OKu7wb
via
logoblog

Thanks for reading WASICHANA WAASWA KUTOPOKEA ZAWADI AMBAZO ZITAHATARISHA MAISHA YAO

Previous
« Prev Post