Ticker

10/recent/ticker-posts

SERIKALI YAVUNJA MKATABA NA KAMPUNI YA NICOL KUENDESHA MACHINJIO YA DODOMA


Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imevunja mkataba wake na Kampuni ya Uwekezaji wa Taifa (NICOL) ambayo kupitia kampuni ya TMCL ilikua ikiendesha kiwanda cha nyama jijini Dodoma.

Uamuzi huo umefikiwa hii leo baada ya Serikali kugundua kuwepo kwa udanganyifu kwenye mkataba wao ambao umeisababishia hasara Taifa ya Shilingi Bilioni 9.7.

Akizungumza leo jijini Dodoma na wafanyakazi wa kiwanda hicho na wadau wa nyama, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina amesema tangu waikabidhi kampuni ya NICOL uendeshaji wa kiwanda hiko hakuna faida yoyote ambayo Serikali imeipata zaidi ya hasara.

Waziri Mpina amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua za kisheria watendaji wote wa NICOL, TMCL na viongozi wa Ranchi ya Taifa (NARCO) ambao wameisababishia serikali hasara hiyo tangu mwaka 2008.

Pia ameipa siku 60 NARCO kujiondoa kwenye ubia na kampuni hiyo ya TMCL kwani ni jambo la aibu kwa kampuni ya Umma kuendelea kushirikiana na watu ambao wamekua wakiipa hasara serikali.

" Hatuwezi kuvumilia hii hali, kuna harufu kubwa ya ufisadi hapa na ndio maana nimevitaka vyombo vyetu vya ulinzi kuhakikisha wanawachukulia hatua wale wote waliokula fedha hapa. Rais Magufuli alishasema ni heri ukala sumu kuliko kula hela ya wananchi wanyonge.

Ni jambo lisiloingia akilini kwamba walikua wakiendesha machinjio haya kwa hasara. Kuna fedha nyingi zinaonekana kampuni iliingiza, mfano kuna fedha Bilioni 1.2 lakini hawakuingiza kwenye mapato. Kuna Bilioni tano iliingia lakini pia haikwenda Benki jambo ambalo ni kinyume na sheria. Lazima tuchukue hatua," Amesem Mhe Mpina.

Akijibu malalamiko ya baadhi ya wafanyakazi waliowahi kusimamishwa na ambao wako kazini, Waziri Mpina pia ameitaka NICOL kuwalipa watumishi wote ambao wamekua wakidai stahiki zao, pamoja na madeni yote zaidi ya Bilioni tano ambayo kampuni ya TMCL ilikua ikidaiwa.

Mhe Mpina amesema baada ya kuvunja mkataba baina yao na NICOL kwa sasa huduma ndani ya kiwanda hicho zitaendelea kama kawaida zikiwa chini ya serikali.

" Serikali itaendesha kiwanda hichi kwa mpito wakati huu ambao tunatafuta mwekezaji ambaye ataweza kuendana na Sera zetu, mahitaji ya sasa, kutafuta masoko nje na ambaye atakua tayari kutoa ajira bila ubabaishaji wa mishahara.

Na kwa kuanzia nimemteua ndugu Victor Mwita kuwa Kaimu Meneja wa kiwanda hiki na uteuzi wake umeanza mara moja baada ya kufanyika kwa makabidhiano chini ya Katibu Mkuu wa Wizara, Prof Elisante Ole Gabriel, " Amesem Mhe Mpina.

Waziri Mpina amesema kwa kipindi chote ambapo machinjio hayo yalikua chini ya kampeni hiyo wameua masoko yote ya kuuza nyama katika Nchi za Kiarabu ambao kwa muda mrefu wamekua wakichukua nyama nchini jambo ambalo limesababisha serikali kukosa mapato ya fedha za kigeni.

Amesema kutokana na uongozi dhaifu wa kiwanda hicho kumesababisha pia wafanyakazi wengi kupoteza ajira kwa makosa yasiyoeleweka lakini pia kushindwa kulipa mishahara wafanyakazi walioko kazini.

Mhe Waziri amewataka wafanyakazi wote wanaodai fedha zao kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho serikali inatafuta njia bora za kuhakikisha wanapata stahiki zao na baada ya siku 60 atatoa taarifa rasmi ambayo itakua yenye matumaini kwa wale wote ambao wamekua wakidai kwa muda mrefu.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akizungumza na wafanyakazi wa machinjio ya Dodoma leo ambapo ameagiza machinjio hiyo kurudi mikononi mwa Serikali.
 Kaimu Meneja wa Machinjio ya Dodoma akizungumza na wafanyakazi wa machinjio hayo baada ya kuteuliwa leo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina ikiwa ni baada ya Serikali kuyachukua machinjio hayo kutoka mikononi mwa Kampuni ya Uwekezaji ya Taifa, NICOL.

 Mmoja wa wafanyakazi ambao wanadai mishahara yao kutoka kiwanda cha nyama cha TMCL, Bw Charles Hema akitoa malalamiko yake kwa niaba ya wenzake mbele ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina (hayupo pichani) alipofika katika kiwanda hicho leo jijini Dodoma.
Wafanyakazi wa kiwanda cha nyama Dodoma wakimsiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina alipofika katika machinjio hayo leo.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2QvtBS3
via

Post a Comment

0 Comments