Ticker

10/recent/ticker-posts

KATAVI YAOMBA UTAFITI MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza nawataalam wa Afya na Maendeleo ya Jamii mkoa wa Katavi wakati wa ziara yake mkaoni humo kujionea shughuli za Afya na Maendeleo ya Jamii.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Lilian Matinga akisoma taarifa ya mkoa kuhusu Sekta ya Afya na Maendeleo ya Jamii kwa Waziri anayesimamia Sekta hizo Ummy Mwalimu wakati wa ziara yake mkaoni humo kujionea shughuli za Afya
na Maendeleo ya Jamii. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

**************************************

Na Mwandishi Wetu Katavi

Mkoa wa Katavi umeiomba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuratibu ufanywaji wa tafiti mpya kuhusu hali ya mimba na ndoa za utotoni mkoani humo ambapo kwa tafiti
zilizopo una asilimia 45 ya mimba na ndoa na mimba za utotoni.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Lilian Matinga ameyasema hayo leo mkoani Katavi wakati wa ziara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alipotembelea mkoani humo kujionea shughuli za Afya na
Maendeleo ya Jamii.

Mhe. Lilian Matinga amesema kuwa tatizo la mimba na ndoa za utotoni bado ni changamoto mkoani humo na limekuwa likichangiwa na wanajamii kwa kuwaozesha watoto wakiwa bado shuleni.

"Niseme bado mkoani kwetu kuna tatizo la ndoa na mimba za utotoni na ukiangalia watoto wengi wanaolewa na wazee wa miaka 50 na zaidi" alisema Mhe. Lilian.

Ameongeza kuwa Mkoani unaendeleza jitihada za Wizara katika kuhakikisha tatizo la ndoa na mimba za utotoni linapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwani limekuwa likikatisha ndoto za watoto wengi wa kike
kupata elimu.

Aidha ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweka msisitizo kwa jamii katika mapambano dhidi ya mimba na ndoa
za utotoni nchini.

Akijibu ombi hilo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa Wizara kwa mwaka 2020 itaratibu tafiti ya jumla kuhusu tatizo la mimba na ndoa za utotoni na kusisitiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuratibu ukusanyaji wa taarifa za mimba na ndoa za utotoni na kupata picha kamili ya mafanikio ya mapambano hayo.

" Tutashirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kufanya tafiti ili tujue tumefikia wapi na kwa asilimia ngapi katika kuondokana na tatizo la ndoa na mimba za utotoni nchini" alisema Waziri Ummy.

Pia Waziri Ummy amewataka wakuu wa shule za Misingi na Sekondari kuhakikisha wanakusanya taarifa za wanafunzi wa kike wanaoacha masomo kwa sababu za mimba na kuolewa na kuhakikisha
zinawasilishwa kwa Kamishna wa elimu.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/35IpzfL
via

Post a Comment

0 Comments