Ticker

10/recent/ticker-posts

NANDY ALIPEWA ‘SHAVU’ NIGERIA AKAKATAA.


Anyakua tunzo Marekani

Na: Moshy Kiyungi,Tabora

Novemba, 2019.

Kama Nandy angelikuwa limbukeni katika maisha, leo hii asingelikuwepo katika ardhi ya Tanzania. Alikataa ofa ya kubakia nchini Nigeria ambako aliahidiwa kuingia mkataba katika lebo ya Chocolate City na kufanya kazi nchini humo.

Tukio hilo lilijiri baada ya kuwa mshindi wa pili katika Shindano la Karaoke Barani Afrika la Tecno Own The Stage, lililofanyika Februari 2016 Lagos nchini Nigeria.

Katika shindano hilo Nandy, alijizolea shilingi milioni 36, pia kuahidiwa kuingia katika lebo kubwa nchini Nigeria ya Chocolate City na kufanya kazi huko lakini alikataa.

Kwa Uzalendo wake uliotukuka, aliamua kurudi nyumbani na kwenda kujiunga katika Jumba la Vipaji Tanzania House of Talents (THT) ambako yupo nao hadi sasa.

Nandy amedhihirisha kuwa kipaji chake siyo cha kubahatisha, Oktoba 2019 ameshinda tena tuzo nyingine kupitia kipengele cha The Best Female in East, South and North Africa, iliyotolewa Oktoba 20, 2019 na African Entertainment Awards USA (AEAUSA) nchini Marekani.

Nandy anaendelea kufanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva pamoja na uigizaji, ambapo yaelezwa kuwa ni miongoni mwa wasanii wa kike waliopo kwenye chati kwa sasa.

Mara baada ya kuzaliwa mjini Moshi, wazazi wake Bi. Mary Charles, ambaye ni fundi wa kushona na Mzee Charles Mfinanga, ambaye ni fundi makenika, walimpa jina la Faustina.

Lakini kwa mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva, wanamtambua kama Nandy a.k.a African Princess.Jina la Nandy ni kifupi cha jina lake halisi Nandera.

Alianza kutumbuiza muziki akiwa na umri mdogo kabisa wa miaka mitano.
Nandy alikuwa mwanachama hai wa kwaya ya mafunzo ya Jumapili ya Kanisa la KKKT huko Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alimaliza elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Mawenzi, baadaye kajiunga Lomwe High School ambako huko alikuwa mwanakwaya mkuu katika shule hiyo.Baada ya kumaliza elimu ya juu alijiunga na Chuo cha Biashara (CBE), jijini Dar es Salaam.

Ngoma iliyomtambulisha mapema ilikuwa ni ya ‘Nagusa Gusa’ ambayo remix yake alimshirikisha msanii Mr. Blue.Msanii huyo licha ya kuimba, ni mwigizaji anayekuja juu katika anga za filamu.

Hivi sasa anaonekana akiigiza katika tamthiria ya Huba, inayooneshwa katika kituo kimojawapo cha luninga nchini.Licha ya kufanya muziki na kuigiza, Nandy ni bonge la dizaina. Ameweza kuwavalisha mastaa wengi wa Bongo Movie.

Yaelezwa kuwa mavazi yake yote anayoonekana amevaa ya asili, huwa anayabuni mwenyewe na kushona.Miongoni mwa watu maarufu aliyewahi kupata ofa ya kubuniwa mavazi ni Naibu Spika Dk. Tulia Ackson.


Milioni 36 zamtoa.

Kati ya vitu anavyojivunia kupitia kipaji chake ni pale alipokuwa mshindi wa pili katika shindano la Karaoke, akajipatia shilingi milioni 36.

Nusu ya pesa hizo zilimuwezesha kumiliki kampuni yake ya kubuni na kutengeneza mavazi ya asili na magauni ya harusi, iitwayo Nandy African Print.

Ilikuwa atoke kwa Akili the Brain?

Kipaji chake kilikuwa kitoke kwa mara ya kwanza katika kampuni ya Akili Records, chini ya Akili The Brain.

Nandy alisema katika kuhangaika kwake kutoka kimuziki, alishawahi kufika kwenye studio ya Akili Records na kutengeneza ngoma nne.

Lakini hazikufanikiwa kutoka mpaka alipopata nafasi ya kwenda Nigeria kwenye Karaoke ya Tecno.

Mwaka wa 2017 alishinda tuzo ya All Africa Music Awards, katika kundi la wasanii bora wa kike kutoka Afrika Mashariki.
Maisha ya awali

Nandy kazi zake zilianza kujulikana baada ya rafiki yake kumtambulisha kwa Ruge Mutahaba, aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania House of Talent (THT), sasa ni marehemu.

Hako ndiko alikokutana na Ema the Boy, ambaye alimtayarishia kibao chake maarufu cha ‘Nagusagusa’, kilichotamba mno wiki tu tangu kutolewa kwake.

Mwanzoni mwa mwaka wa 2016, Nandy alishiriki kwenye mashindano ya kuimba yaliyoandaliwa na Tecno.

Shindano lilishirikisha washiriki wengine kutoka nchi nyingi za Afrika. Kipindi cha fainali kilichofanyika huko Lagos, Nigeria, Nandy aliibuka kama mshindi wa pili.

Shindano hilo lilimkuza kimuziki, hasa katika suala zima la utumbuizaji jukwaani, alipata maarifa ya muhimu kutoka kwa magwiji wa muziki kama vile akina M.I Abaga, Yemi Alade na Bien wa Sauti Sol.

Mwaka wa 2017 alitoa kibao cha ‘One Day’ ambacho kilisukuma kazi yake na hatimaye kumpa nafasi kadhaa zilizomfanya kushiriki kwenye Coke Studio Africa 2017.

Mwaka huohuo Nandy akachaguliwa kwenye Tuzo za All Africa Music Awards, katika kundi la wanamuziki bora wa kike kutoka Afrika Mashariki, ambapo aliibuka mshindi.

Aidha Nandy alishirikishwa na Willy Paul kutoka Kenya kutengeneza wimbo wa mwingine wa ‘Hallelujah’, ambao unapendwa na idadi kubwa ya wapenzi wa muziki wa Bongo Fleva.

Mwaka 2018 alitoa albam ya African Princess, akafuatia kuporomosha singo zake za I'm Confident ya mwaka 2013, Nagusa gusa ya 2017, One Day ya mwaka 2017, Wasikudanye ya mwaka 2017, Kivuruge ya 2017 na Ninogeshe ya mwaka 2018.

Aidha mwanadada huyo alishirikishwa vilivyo na Nassor Isihaka a.k.a Aslay katika wimbo wa Subalkheri Mpenzi ambao ni remix.

Msanii huyo alishinda tuzo ya AFRIMA za nchini Nigeria, ambako yeye na Ali Kiba walitia fora.



Matarajio yake

Hivi karibu alitoa kibao kinanachokwenda kwa jina Mahabuba, ambacho amemshirikisha msanii mwenzake Isihaka Nassor ‘Aslay’.

Msanii huyo wa Bongo Fleva, mtunzi wa wimbo One Day, amemtaja mshindi wa tuzo ya BET kutoka label ya WCB, Rayvanny kama msanii anayetamani kufanya naye kazi kutoka ndani ya label hiyo.

Mwimbaji huyo ameeleza kuwa kwa namna anavyotazama aina ya muziki anaofanya Rayvanny na wake anaona unaendana.

“Nawaelewa wote lakini kwa haraka haraka nikipewa chance kwa mtu wa WCB kufanya naye ngoma nitafanya na Rayvanny.

Nahisi kama tuna Chemistry ile, ambayo tunaweza tukaendana, yaani ukiwasikiliza mashairi yao wewe ndio unajua unafiti wapi, kwa hiyo mimi naona kwa Rayvanny nafiti,” alitamka Nandy.

Msanii huyo Nandy ambaye kwa sasa anafanya vizuri kwa wimbo wake mpya ‘Wasikudanganye’, hajawahi kumshrikisha msanii yeyote katika nyimbo zake tangu alipotoka na ngoma yake ‘Nagusagusa’ kisha kufuatiwa na One Day.


Kwa upande wa Saida Karoli, amemtaja kuwa ni miongoni mwa wasanii wa kike ambao pia anatamani kurudia nyimbo zao.

Kuhusu kufanya kazi na Saida Karoli, Nandy amesema, “natamani sana hata anipe ngoma yake ya zamani niifanyie remix na sijui ni ipi kwa sababu kafumua!, sijui nitaimbaje.

Natamani anipe nifanye verse na kama alifanya chorus ibaki pale pale, halafu mimi nirudie zile verse, I hope atakubali” amesisitiza.

Iwapo utapata kuiona Baadhi ya nyimbo za Saida Karoli ni pamoja na Kasimile Katonda, Nsenene, Karibatano na Mapenzi Kizunguzungu uliouachia Juni 2003.


Saida alitoka na albamu nyingine nzuri iliyokwenda kwa jina la Salome Maria.


Nandy alitarajia kuolewa na Ruge Mutahaba wa Clouds FM. Mpaka sasa anamkumbuka sana kwani alimtolea mahari kabla hajafa. Pole sana Nandy, Mungu atakujaalia kumpata mume mwingine.

Mwisho.

Makala hii imeandaliwa toka vyanzo mbalimbali vya habari.

Mwandaaji anapatikana kwa namba:

0784331200, 0767331200, 0736331200 na 0713331200.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2NfivjO
via

Post a Comment

0 Comments