Ticker

10/recent/ticker-posts

TANZANIA MWENYEJI WA MKUTANO WA MAWAZIRI WA SEKTA ZA MAZINGIRA, MALIASILI NA UTALII NCHI ZA SADC

Na Mwandishi wetu, Globu ya Jamii
IKIWA Tanzania ni miongoni mwa nchi 16 wanachama wa SADC wanaotekeleza Mkakati wa SADC kuhusu Usimamizi wa Sheria na Vita Dhidi ya Ujangili wa Wanyamapori, inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). 

Hayo yameelezwa katika taarifa kwa umma ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Constantine Kanyasu iliyotolewa Oktoba 16. 

Taarifa hiyo inaeleza kuwa mkutano huo utafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuanzia tarehe  21 hadi 25 Oktoba, 2019.

"Madhumuni ya mkutano huu ni pamoja na kuangalia mwenendo wa hali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, kubainisha utekelezaji wa mikakati ya hifadhi na usimamizi wa mazingira, kupitia Mkakati wa SADC wa Uchumi wa Bahari (SADC Strategy on Blue Economy); na kutathmini maendeleo katika sekta za misitu, wanyamapori na utalii".

Mkutano huo utahusisha Mawaziri wa sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii utatanguliwa na mikutano ya wataalam wa sekta ya wanyamapori utakaofanyika tarehe 18 hadi19 Oktoba, 2019 na Mkutano  wa Makatibu Wakuu wa sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii utafanyika tarehe 21 hadi 24 Oktoba, 2019.

 Aidha Mikutano hii miwili itajadili na kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa katika kikao cha Mawaziri kitakachofanyika tarehe 25 Oktoba, 2019 kwa maamuzi na maelekezo.

Mkutano wa Mawaziri  unatarajiwa kufunguliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ijumaa Oktoba 25, 2019, ukumbi wa mikutano wa AICC, Arusha na Mkutano wa Makatibu Wakuu unatarajiwa kufunguliwa na Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Oktoba 21, 2019 katika ukumbi wa AICC, Arusha.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa Maeneo mengine yanahusu Programu za uhifadhi yaliyovuka mpaka wa nchi moja hadi nyingine kwenye maeneo ya misitu, uvuvi, mazingira na mabadiliko ya tabianchi, utalii, ukuzaji viumbe maji na Mkakati wa Ubora wa Afya wa wanyama wa majini (SADC Transfontiers Conservation Areas,forestry, fisheries, environment and climate change, tourism,  regional Aqua culture strategy and action plan, and SADC Aquatic Animal Health Strategy) pamoja na Programu ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.

Mapema mwezi Agosti mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Dar es Salaam. Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikabidhiwa na kupokea rasmi jukumu la  uenyekiti wa Jumuiya hiyo. 

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ni moja kati ya jumuiya za  kikanda katika bara la Afrika. Jumuiya hii iliundwa kwa dhumuni la kuimarisha ushirikiano katika nyanja za uchumi,  ulinzi, siasa na usalama.  Jumuiya hii inaundwa na  nchi wanachama 16 ambazo ni Angola, Botswana, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/32oV6S2
via

Post a Comment

0 Comments