Ticker

10/recent/ticker-posts

Juhudi za Kuunga Mkono Tanzania ya Viwanda: VETA yazindua kiwanda cha kisasa cha samani jijini Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichao (Mb), leo tarehe 30 Septemba, 2019 amezindua rasmi kiwanda cha kisasa cha kutengeneza samani cha VETA, kilichopo katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Dodoma (VETA Dodoma RVTSC).

Kiwanda hicho kimegharimu shilingi 3,378,086,721 hadi kukamilika. Gharama hiyo inajumlisha gharama za Mshauri Elekezi, Mkandarasi wa Ujenzi, na Ununuzi wa Mashine na mitambo ya kiwanda hicho. Kiwanda kimeshaanza uzalishaji na kinatoa samani za kiwango cha juu cha ubora kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya kiofisi na majumbani. Hivyo kitapunguza utegemezi wa samani kutoka nje ya nchi pamoja na kusaidia wanafunzi wa fani ya useremala kufanya mazoezi ya vitendo kwenye mashine za kisasa.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri, Mweyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Bw. Peter Maduki alisema VETA itatumia kiwanda hicho pia kuendeleza ubunifu katike eneo la useremala, kwani kina mashine za kisasa zinazoweza kufanya mambo mbalimbali katika shughuli za useremala.

Vilevile, alisema kuwa kiwanda hicho ni fursa kwa mafundi seremala na wafanyabiashara wa samani katika jiji la Dodoma, kwani wanaweza kutumia mashine za kiwanda hicho kuchonga na kukereza mbao zao kwa ajili ya utengenezaji wa samani bora za aina na miundo mbalimbali.

Akiwahutubia wananchi katika uzinduzi wa kiwanda hicho ambao uliambatana na sherehe ya mahafali ya 36 ya Chuo cha VETA Dodoma, Mhe. Prof. Ndalichako, licha ya kuipongeza VETA kwa ujenzi wa kiwanda bora na cha kisasa, aliziomba taasisi za serikali na wananchi kwa ujumla kukitumia kiwanda hicho kujipatia samani bora na kwa bei nafuu. 

Aliwahimiza watendaji wa VETA kuhakikisha kiwanda hicho kinajiendesha kibiashara ili kuleta faida na ikiwezekana kirudishe gharama iliyotumika kukijenga ili itumike kujenga viwanda vingine.

Akitoa maelezo mafupi, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema kuwa mradi wa ujenzi wa Karakana ya Kisasa ya Utengenezaji Samani ni miongoni mwa miradi mbalimbali inayotekelezwa na VETA katika vyuo mbalimbali hapa nchini, kwa lengo la kuboresha mafunzo ya ufundi stadi yanayoendeshwa katika mfumo wa vitendo, ili kutoa wahitimu mahiri wanaohitajika katika soko la ajira na wanaoweza kujiajiri na kuajiri vijana wenzao.

Aliitaja miradi mingine kuwa ni kiwanda cha nyama cha VETA Dodoma; hoteli za VETA za Dodoma, Njiro (VHTTI) Arusha, Mikumi, Tanga na Mtwara, pamoja na miradi ya ujenzi na uboreshaji wa karakana na ununuzi wa vifaa katika vyuo mbalimbali vikiwemo Kihonda, Manyara, Arusha (Oljoro), Lindi, Kibaha, Mbeya na Mwanza.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha VETA Dodoma, Bw. Ramadhani Mataka, akitoa historia kuhusu kiwanda, alizitaja faida zinazotarajiwa katika mradi huo kuwa ni kutengeneza samani bora kwa matumizi ya serikali, mashirika mbalimbali na watu binafsi; kutoa mafunzo ya utengenezaji wa samani zilizo bora kwa wanachuo wa VETA ili kuendana na njia za kisasa za uzalishaji malighafi viwandani; kutoa mafunzo kwa wahitimi wa VETA (incubation) na kuongeza mapato kwa serikali.
 Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kiwanda Cha VETA cha kutengeneza samani.
 Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakiangalia jiwe la uzinduzi wa kiwanda Cha VETA cha kutengeneza samani katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Dodoma.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiterezesha mbao katika kiwanda cha VETA cha kutengeneza Samani katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma Dodoma.


from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2o89jDX
via

Post a Comment

0 Comments