Ticker

10/recent/ticker-posts

Mabehewa ya treni kuanza kutengenezwa nchini chini ya kiwanda cha wazawa

Mabehewa ya treni kuanza kutengenezwa nchini chini ya kiwanda cha wazawa
WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, ikidhamiria kuinua uchumi kwa kutumia miundombinu ya usafirishaji, wadau wa maendeleo wamekuwa wakitumia fursa zilizopo kunufaisha watanzania.


Mkurugenzi wa Makampuni ya Kiluwa Group, Mohamed Kiluwa (kulia) akikabidhiana mkataba na Mkurugenzi wa Kampuni ya Africa Jambo Group
Miongoni mwao ni Mkurugenzi wa Makampuni ya Kiluwa Group, Mohamed Kiluwa ambaye amedhamiria kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mabehewa ya treni yaliyochakaa kwa kutumia reli ya kisasa na ya zamani.

Akiwa katika hafla ya kubadilishana nyaraka za makubaliano hayo aliyoingia na Kampuni ya Africa Jambo Group ya nchini Afrika Kusini, katika Jiji la Johannesburg hivi karibuni Kiluwa alisema anataka kufanya kitu cha kipekee katika ardhi ya Tanzania kinyume na matarajio ya wengi.

“Hiki tunachotaka kukifanya hakijawahi kufikiriwa na wengi lakini kitaleta tija katika uchumi wa nchi, tunafahamu tunapoelekea ni Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati. Tutahitaji mbinu bora za usafirishaji malighafi na bidhaa, reli ni njia rahisi na salama kusafirishia mizigo,” alisema Kilua.


Alibainisha, kiwanda hicho kitakuwepo katika eneo la uwekezaji Kiluwa Free Processing Zone mkoani Pwani, ambapo taarifa ya awali ya utekelezaji wa mradi huo inabainisha utakuwa katika awamu tatu.

Kila awamu itatoa ajira kwa watu wapatao 980, mradi huo unalenga katika soko la ndani ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Vilevile wakazi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki watakuwa sehemu ya wanufaika kwa kuwa baadhi ya mizigo itakwenda katika nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika.

“Ifahamike tumetenga kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 150, kwa ajili ya kukamilisha mradi huu ambao utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda nchini pamoja na usafirishaji,” alisema Kiluwa.

Naye, mwakilishi wa Kampuni ya Africa Jambo Group, Marthinus Christian Landman alisema wameamua kuwekeza Tanzania kwa sababu wanajua ni eneo muhimu linalokua kwa kasi kiuchumi kutokana na malengo makubwa yaliyowekwa na serikali iliyopo madarakani.

“Siku zote mfanyabiashara anaangalia eneo ambalo atanufaika, tunaangalia zaidi faida kabla ya kukamilisha mikataba, tumejiridhisha kwa sasa Tanzania ni sehemu sahihi na salama kiuewekezaji kwa sababu Rais Dk. John Magufuli amedhamiria kuona watu wanafanya kazi, hakuna kona kona wala rushwa,” alisema Landman

from UDAKU SPECIAL BLOG https://ift.tt/2GXtU5c
via

Post a Comment

0 Comments