Ticker

10/recent/ticker-posts

DC Chongolo, Msuya Waaga Mwaka 2018 kwa Kueleza Mafanikio ya Serikali

Na. Frank Mvungi

Wakuu wa Wilaya za Kinondoni, Daniel Chongolo na Wilaya ya Uyui, Gift Msuya kwa pamoja wamepongeza Juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha mwaka 2018 ambazo zilizolenga kuboresha huduma za jamii na kuinua maisha ya wananchi.

Akizungumza leo katika mahojiano maalum na Idara ya Habari-MAELEZO, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel Chongolo, amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2018, wananchi wameshuhudia uboreshaji wa miundombinu ya barabara, madaraja, vituo vya afya, Elimu, ujenzi Reli ya kisasa, Zahanati na ujenzi wa Hospitali mpya za Wilaya zipatazo 67.

"Ujenzi wa reli ya kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) hapa nchini utawezesha kufungua sekta mbalimbali ikiwemo uchukuzi, kukuza biashara kati ya Tanzania na mataifa ya jirani, kufungua uwekezaji ambao utachochea kwa kiwango kikubwa kukuza uchumi na ustawi wa wananchi", ameeleza Chongolo.
Akifafanua kuwa katika Wilaya ya Kinondoni, barabara zenye urefu wa kilomita 58.2 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na baadhi zimeshakamilika.

Ametaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa Hospitali ya Wilaya inayojengwa katika eneo la Mabwepande pamoja na ujenzi wa kituo cha afya Kigogo vitaimarisha na kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi wa maeneo hayo.Kwa upande wa maji katika Wilaya ya Kinondoni amebainisha kuwa upatikanaji wa maji unatarajiwa kufikia zaidi ya asilimia 90 kutokana na maboresho na uwekezaji ulifanyika katika miundombinu ya maji.

Akizungumzia Wilaya ya Longido ambayo amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya, Chongolo amesema kuwa kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani Wilaya hiyo ilikuwa na Kituo cha Afya kimoja lakini hivi sasa vimejengwa vituo vya afya vinne vilivyojengwa katika Kata za Kitumbeine, Namanga, Engarenaibor na Olmoti.

Alibainisha kuwa upatikanaji wa huduma ya maji Wilayani humo unatarajiwa kufikia asilimia 130 kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya maji.Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uyui Mhe. Gift Isaya Msuya, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa Shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ambapo tayari maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa na wa kihistoria yameanza.

Akizungumzia mikakati yakuwawezesha wananchi katika Wilaya hiyo, Msuya amesema tayari Serikali imeendelea kuwajengea mazingira wezeshi wananchi wa Uyui na mkoa wa Tabora kwa kuimarisha usafiri wa anga ambapo ndege za ATCL zimekuwa zikifanya safari za mara kwa mara mkoani Tabora jambo linalochochea maendeleo na ustawi wa wananchi kwa kufungua fursa za kukuza uchumi.

Ametaja miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini wa kufua umeme kutoka Mto Rufiji, Barabara, madaraja, vivuko, na ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali hapa nchini kuwa ni mafanikio makubwa kwa ujenzi wa uchumi na utoaji huduma bora kwa wananchi.

Aidha, amepongeza hatua ya Mhe. Rais kuwatambua wajasiriamali wadogo maarufu kama wamachinga kwa kuwapatia vitambulisho maalum vinavyowawezeshakufanya biashara bila kubugudhiwa hali itakayowainua kiuchumi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato.

Wakuu hao wa Wilaya wameeleza kuwa kuwa katika mwaka 2019 wanatarajia kuendelea kutekeleza ahadi za Serikali ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi ikiwemo kuweka mazingira bora ya uwezeshaji kuichumi na utoaji wa huduma za jamii.


from MICHUZI BLOG http://bit.ly/2TmQzLb
via

Post a Comment

0 Comments