Ticker

10/recent/ticker-posts

Maskini Wastara! Tazama Mguu Wake Ulivyoharibika, Anaomba Msaada (VIDEO)


AMA kweli hujafa, hujaumbika! Ndivyo unavyoweza kusema endapo utaisoma simulizi ya hali ya sasa ya msanii wa filamu Bongo, Wastara Juma anayesumbuliwa na mguu wake wa kulia aliokatwa baada ya kupata ajali, Risasi limeongea naye na kutoa simulizi ya kukutoa machozi.

Akiongea kwa masikitiko, Wastara ambaye alikuwa akilia kila wakati anapoongelea maumivu anayoyapata, alifikia hatua ya kuonesha mguu wake wenye jeraha kwa mara ya kwanza, kitendo kilichowafanya waandishi na baadhi ya watu waliokuwa karibu naye kutokwa na machozi.

Wastara alisema kuwa, amefikia hatua ya kuuonesha mguu wake huo na maumivu anayopata kutokana na baadhi ya watu kutomuamini pale anapoelezea wakati mgumu anaopitia.




“Jamani ninavyoumwa hivi kiuweli natamani nisingekuwa staa kwa sababu inafikia wakati natamani hata niingie barabarani kuomba, hii ni katika kuonesha ni jinsi gani nataka kwenda kupata matibabu ya mguu huu unaoniuma kila sekunde na dakika. Wapo watu ambao hawanielewi kabisa na sidhani kama watanielewa,” alisema Wastara.
Wastara aliendelea kusema kuwa amelazimika kuomba msaada kutoka kwa watu si kwa kutaka ila ni kwa sababu ameshafanya kazi za kila aina ili atumie jasho lake katika kujitibu lakini amejikuta akiambulia patupu huku watu wengine wakimkimbia.

KAZI ALIZOZIFANYA AKAAMBULIA PATUPU
Wastara alieleza kazi alizozifanya ambazo zimempotezea pesa na mpaka leo anaumia kuwa ni pamoja na mkataba aliosaini na Wachina wa kuwatangazia simu zao za KZG ambao walimkimbia bila kumlipa pesa zake kiasi cha shilingi milioni 80 na anaiomba serikali iingilie kati suala lake.

“Sipendi kuomba kabisa kwani uwezo wa kutafuta kama nikiwa na mguu naweza lakini dah… sijui nianzie wapi lakini hili suala la kudhulumiwa na watu linaniumiza sana (analia…) Wachina na Kampuni yao ya Simu ya KZG wamenikimbia nikiwa nawadai milioni 80, tukio la pili Msumbiji nimepoteza mzigo wa milioni 19 kwenye vurugu za kufukuzwa Watanzania ambapo nilikuwa nafanya biashara zangu nikijikusanyia pesa za kurudi hospitalini.

“Tukio la tatu nimeenda nchini Sweden kufanya filamu, nimerudi mikono mitupu kwani kule sikulipwa kama nilivyotarajia, mwezi wa 4 nimedai pesa yangu Steps, tumeishia mahakamani bila kulipwa nilivyokuwa natarajia, badala yake nikaahidiwa kulipwa milioni mojamoja ambayo haiwezi kunisaidia kwani nahitaji pesa ndefu kwa ajili ya kujitibu.

“Tokea hapo chochote ninachofanya kinachohusu pesa lazima tuishie polisi au mahakamani, silipwi vile tunavyokubaliana na baya zaidi ninaofanya nao kazi hawajui kuwa tangu nimerudi nchini toka Sweden nahaha kutafuta pesa ya matibabu, silali kwa maumivu makali ya mgongo na ninazimia kila muda.
“Hii imetokana na kuchelewa kurudi hospitalini kufanya tiba ya mgongo na kubadilisha ‘Soberly Skoner’ inayowekwa kwenye mguu kama tiba kuu ya kurudisha mgongo wangu ukae sawa,” anaeleza Wastara na kusisitiza kuwa, endapo hatapata matibabu ya haraka, anaweza kuondoka duniani.

SABABU YA MAUMIVU
Wastara ameeleza sababu ya maumivu ya mguu kuwa ni kuvimba na kuchanika kila mara kutokana na mguu wa bandia anaouvaa kupitwa na wakati huku mwingine ambao una afadhali ukisababisha mishipa ya mgongo kuhama.
“Hii hali inanikosesha raha, kwa kusimulia tu huwezi kunielewa msomaji lakini navimba na kuchanika, mara kwa mara mgongo unauma kitu ambacho sasa kinaniathiri kiakili kwani maumivu ni makali na natumia dawa za maumivu kila mara yanapotokea,” alisema Wastara.

AWAANGUKIA JPM, MAMA SAMIA NA MAKONDA
Wastara amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kuliingilia kati suala lake la Wachina wenye Kiwanda cha KZG ambao ‘wamemzima’ pesa hizo alizozitaja ili alipwe na aweze kupata matibabu kuokoa uhai wake.
Mbali na rais, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda ambaye muda mwingi amekuwa karibu na wananchi wake hasa wanapokuwa kwenye matatizo kulifuatilia suala lake na Wachina hao ili alipwe haki zake.
Pia msanii huyo alimuomba Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu kuangalia jinsi anavyoweza kumsaidia katika matibabu yake kwani hata mwanzo wa tatizo lake aliwahi kuwa naye karibu.
“Nimeamua kuwaandikia hata barua viongozi hao watatu wa nchi, huenda barua zangu hazijawafikia lakini kiukweli peke yangu bila mkono wao mimi siwezi, nahitaji pesa nyingi ambazo si familia wala mimi mwenyewe tunaoweza kuzipata kwa ajili ya matibabu yangu,” alisema Wastara.

AOMBA MSAADA KWA WATANZANIA
Mbali na kuomba msaada kwa viongozi hao, staa huyo ambaye maisha yake kwa sasa yanasikitisha amewaomba Watanzania wenye moyo wa huruma wamsaidie ili aweze kwenda kwenye matibabu kwani anajiona anakufa hivihivi.
“Watanzania wenzangu, naomba mnisaidie ninakufa najiona, mficha uchi siku zote hazai. Leo nimeona niweke ustaa pembeni, nimeamua kufunua mguu wangu mnielewe ni maumivu gani nayapata. Mimi nimejaribu kila aina ya biashara ambayo ni halali lakini nimeshindwa kupata pesa za kurudi kwenye matibabu, kwa yeyote aliyeguswa naomba anipigie simu kwa namba yangu hiyo hapo chini,” alisema Wastara.

ANAHITAJI MIL 37
Ili awe sawa, Wastara anahitaji milioni 37 kwa ajili ya kutengenezewa mguu ambao ndiyo dawa ya mgongo pia. Mguu huo pamoja na siku atakazokaa hospitali ndiyo gharama inayohitajika kwani atafikia kwenye Hospitali ya Sifael iliyopo India.

MGUU KUKATWA
Endapo atakosa pesa hiyo, inatakiwa akatwe mguu wake tena jambo ambalo hayuko tayari nalo huku akieleza kuwa hataweza kuendesha maisha yake kwa kutembelea magongo mawili.
Kumsikia Wastara akiongea kwa masikitiko fungua mtandao wa You Tube kisha andika neno Global TV ONLINE halafu bofya kwenye alama nyekundu yenye maandishi SUBSCRIBE, utaona habari yote ya Wastara.

NENO LA MHARIRI
Wastara anahitaji msaada wako, yeyote anayeweza kumsaidia awasiliane naye kwa namba yake 0768666113.

VIDEO:


GPL