Ticker

10/recent/ticker-posts

Bilionea Yusuf Manji Atii Sheria Bila Shuruti......Alipewa saa 24 kuondoka kwenye jengo la PSPF (Quality Plaza)

Mfanyabiashara Yusuph Manji jana alitii sheria bila shuruti kwa kuhama kwenye jengo la Quality Plaza akitekeleza amri ya Mahakama ya kumtaka kurejesha jengo hilo ambalo ni mali ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF). 

Mbali na kutekeleza amri ya kuhama baada ya kupewa notisi ya saa 24 iliyomalizika juzi, pia anatakiwa kulipa malimbikizo ya deni la pango la Dola za Marekani 6.1 milioni (zaidi ya Sh13 bilioni), ambazo kama asipozilipa mali zake zitakamatwa. 

Hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama Kitengo cha Ardhi kutoa hukumu ya kumtaka Manji kuondoka kwenye jengo hilo pamoja na kuilipa deni la pango. 

Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Manji ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi. 

Viongozi wa kampuni za Manji waliokuwa wakisimamia uondoaji wa vifaa uliomalizika jana asubuhi, walikataa kuzungumza na waandishi wa habari waliofika kufuatilia tukio hilo. 

Tangu juzi chini ya usimamizi wa kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart, Manji na kampuni zake walikuwa wanaondoa vifaa mbalimbali vilivyopo kwenye jengo hilo na kuhitimisha shughuli hiyo jana.

Meneja Uendeshaji wa Yono Auction Mart, Atukuzwe Mhugo alisema kampuni ambazo walikuwa wakizisimamia kuondoa vifaa ni Quality Group Co Ltd, Gaming Managemeti Ltd, Q Consult Ltd na Quality Logistics Co Ltd.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ya Yono, Scholastica Kenyela alisema tayari wameshaziondoa kampuni za Manji kwenye jengo hilo. 

Kenyela alisema mteja wao ambaye ni PSPF alichukua uamuzi huo baada ya Manji kushindwa kulipa kodi ya pango ya zaidi ya Sh13 bilioni. 

“Sisi tumetimiza wajibu wetu, ukienda pale utaona tayari tumeshafanya kazi yetu kwa sababu alipewa notisi ya saa 24 awe ameondoka,”alisema.

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa PSPF, Abdul Njaidi alisema masuala yote yanayohusiana na jengo hilo kwa sasa yako chini ya Yono Auction Mart. “Sipo Dar es Salaam na sitazung- umzia chochote kuhusu jengo hilo wenye mamlaka ni Yono naomba uwatafute wao,” alisema.