Ticker

10/recent/ticker-posts

RAI DK.JOHN MAGUFULI KUAPISHWA KESHOKUTWA,NA HIZI NDIZO CHANGAMOTO KUBWA ZINAZO MKABILI

Rais mteule wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Pombe Magufuli anakabiliwa na changamoto nane kubwa ikiwamo ya namna ya kutatua kwa amani mgogoro wa urais wa Zanzibar ambao umeibuka, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kusitisha mchakato wa kumtangaza mshindi.

Wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema mbali na changamoto hiyo inayotishia kuwaingiza wakazi wa visiwa vya Pemba na Unguja katika uhasama wa kisiasa na kijamii, Dk Magufuli ambaye ataapishwa keshokutwa, atakabiliwa na changamoto ya ongezelo la Deni la Taifa, matarajio makubwa kupita kiasi kwake, Katiba Mpya, upinzani wa kisiasa uliokomaa, ‘unafiki’ ndani ya chama tawala, kufumua mfumo wa utendaji serikalini na kurejesha umoja.
Katika mahojiano na gazeti hili jana, baadhi ya wasomi wametoa wito Rais Jakaya Kikwete amalize utata huo wa Zanzibar kabla ya kuondoka ikulu badala ya kumwachia Dk Magufuli kwani itakuwa changamoto kubwa kwake.
Urais Zanzibar
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Des Salaam, Dk Benson Bana amesema ikiwa Rais Kikwete hatashughulikia utata huo, Dk Magufuli atakabiliwa na changamoto kubwa kwani suala hilo linagusa Muungano.
“Mvutano ulioko Zanzibar hauna budi upatiwe ufumbuzi na Rais Jakaya Kikwete na endapo atakuwa hajamaliza Dk Magufuli atalazimika kubeba kijiti hicho,” alisema Bana.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) Hamad Salim alisema, “Kile kinachoendelea Zanzibar bado suluhu haijapatikana, kwa hiyo atakapoingia madarakani ana wajibu wa kuhakikisha anamaliza tatizo hilo ili kulinda Muungano bila kuacha dosari yoyote.”
Mgogoro wa Zanzibar umeibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kuamua kufuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 kwa madai zimegundulika kasoro kadhaa katika baadhi ya vituo na majimbo ya Pemba.
Jumuiya ya Kimataifa; Ubalozi wa Marekani, Umoja wa nchi za Ulaya (EU), waangalizi wa kimataifa, na wanasiasa nchini wameitaka ZEC kuendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi huo ili mshindi atangazwe. Jecha, ambaye hakumshirikisha kamishna yeyote wakati akitoa tangazo hilo, ameshikilia uchaguzi wote urudiwe badala ya maeneo yenye dosari.
Katiba Mpya
Changamoto nyingine inayomkabili Dk Magufuli ni Katiba mpya. Katika kipindi chote cha kampeni Dk Magufuli pamoja na mgombea mwenza wake ambaye ni makamu wa rais mteule, Samia Hassan Suluhu walikwepa kuzungumzia Katiba Mpya.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alisema suala la Katiba Mpya halikwepeki na kwamba akitaka kutekeleza mambo aliyoahidi kwa Watanzania hana budi kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana.
“Ni lazima aachane na Katiba Inayopendekezwa, arejee kwenye Rasimu ya Jaji Warioba (Joseph, Mwanyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) wananchi waipigie kura upya kwa sababu huko ndipo kulikokuwa na mapendekezo yao,”alisema Profesa Mpangala.
Alisema mapendekezo yaliyopo kwenye rasimu hiyo ndiyo yanayoendana na hali ilivyo sasa, hata miiko ya uongozi itafuatwa ikiwa hilo litafanyika.
Katika hilo, Dk Magufuli atakabiliwa na changamoto ya kumaliza mchakato wa Katiba Mpya ambayo imegawanya makundi mawili; kundi linaloiunga mkono (CCM) na lile linaloipinga. “Je, ataamua kuendelea na Katiba iliyoligawa Taifa katika makundi mawili au ataanza upya ili kuleta umoja wa Watanzani?”alihoji Profesa Mpangala.
Rais Kikwete alianzisha mchakato wa kupata Katiba mpya, lakini uliibuka mgawanyiko baada ya Bunge Maalumu la Katiba lililokuwa chini ya Mwenyekiti Samuel Sitta na Makamu wake, Samia kutupa mapendekezo mengi ya wananchi. Malumbano hayo yalisababisha Katiba Pendekezwa kushindwa kupigiwa kura.
Ahadi
Changamoto nyingine inayomkabili Dk Magufuli ni kutekeleza ahadi zake. Kwa mujibu wa Dk Bana ili aweze kuendesha shughuli za Serikali itabidi afanye kazi ya kuwashawishi Watanzania kuwa na utamaduni wa kulipa kodi.
“…Ameahidi mambo mengi ambayo hayataweza kutekelezeka kama wananchi hawatalipa kodi ambazo zitamsaidia kuendesha shughuli mbalimbali katika Serikali yake,”alisema Dk Bana.
Profesa Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), alisema itabidi Dk Magufuli akabiliane na changamoto ya ajira kwa vijana wanaohitimua elimu ngazi mbalimbali, wakulima na ardhi. “Badala ya kujenga viwanda vikubwa, Serikali hiyo mpya inatakiwa ijenge viwanda vidogo vitakavyokamilika mapema ili kutoa fursa ya ajira,” alisema Profesa Gabagambi.
“Michezo pia inatakiwa kupewa kipaumbele kwani ni moja ya sekta inayotoa ajira kwa vijana,’’alisema.
Kuhusu ardhi alisema kama walivyohidi wakati wa kampeni, wanatakiwa kufanya hivyo ili kulinda ardhi ambayo ina rutuba kwa ajili ya kilimo kama hifadhi za Taifa zinavyolindwa.“Wakulima wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu ikifika kwenye suala ya bei ya mazao. Ni vyema kukawa na tume itakayosimamia hilo ili kuhakikisha wakulima wananufaika na bei ya mazao yao na siyo kuwanufaisha wafanyabiashara tu,”alisema.
Katika kipindi chote cha kampeni, Dk Magufuli aliwapa Watanzania matarajio makubwa kwamba atafanya mabadiliko makubwa na ya kweli. Alitoa ahadi hizo wakati ahadi nyingi za Rais Kikwete hazijatekelezwa.
Hayo yakitekelezwa Serikali ya Awamu ya Tano itaweza kutekeleza ahadi ya kuongeza ajira kwa vijana, kuimarisha usafirishaji, kusambaza kwa uhakika na kwa kasi huduma za jamii hasa maji, kuanzisha mahakama maalumu ambayo itashughulika na mafisadi, na kutoa huduma nzuri za afya, elimu, barabara, pamoja na kuvipatia vijiji Sh50 milioni.
Deni la Taifa
Changamoto kubwa ya pili inayomkabili Dk Magufuli ni namna ya kulikabili deni kubwa la taifa linalokadiriwa kufikia Sh30.6 trilioni. Rais Jakaya Kikwete alipokabidhiwa nchi deni la taifa lilikuwa Sh9.3 trilioni lakini katika kipindi cha miaka 10 limeongezeka hadi kufikia kiasi hicho.
Chini ya Mwalimu Nyerere uchumi ulikuwa umestawi hadi ulipoharibiwa na vita dhidi ya nduli Iddi Amini Dada mwaka 1978/9. Baada ya vita kumalizika Mwalimu Nyerere aliwataka Watanzania kufunga mikanda kwa miezi 18, baadaye akasema miaka mitatu, lakini hali haikubadilika.
Nyerere alikataa masharti ya kurekebisha uchumi yaliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, badala yake kazi hiyo ilifanywa na mrithi wake Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Tanzania ikawekwa chini ya Mpango wa Nchi Maskini zenye Madeni Makubwa (HIPC) uliowezesha kufutiwa kiasi kikubwa cha madeni.
Rais Benjamin Mkapa alipoingia madarakani na kutekeleza kwa kasi masharti ya wahisani kwa kubinafsisha taasisi za fedha, viwanda na mashirika ya umma, Tanzania ilifutiwa madeni ya mabilioni ya shilingi, na aliondoka madarakani akiacha Hazina ikiwa na fedha za kutosha na deni la taifa likiwa limedhibitiwa.
Lakini sasa, Rais Kikwete anaondoka akiacha deni kubwa, uchumi unaokua kwa asilimia 7 huku utawala wake ukigubikwa na kashfa za ufisadi kama wa Epa, Richmond na Tegeta Escrow. Ufisadi wa Tegeta Escrow ndiyo ulisababisha Bodi ya Wakurugenzi ya Maendeleo ya Milenia (MCC) kusitisha msaada kwa Tanzania wa Sh992.8 bilioni.
Serikali
Changamoto nyingine ni kufumua mfumo wa uendeshaji wa Serikali. “Hayo waliyoahidi hata hayati Mwalimu Julius Nyerere aliahidi, Tanzania kuwa nchi ya viwanda, yote yaliahidiwa tangu zamani. Suala ni kubadili mfumo wa uchumi na siasa ili Tanzania iwe nchi ya kujitegemea, iwe na vyanzo imara vya kuingiza mapato bila utegemezi kutoka nje,” alisema Profesa Mpangala.
Wakati wa kampeni, Dk Magufuli alisema mbali ya mawaziri wake kuapa watatia saini ili wathibitishe kuwa hawatakuwa watendaji mizigo, wazembe, wasiowajibika pamoja na kugeuza ofisa za Serikali kuwa vijiwe vya ‘kupiga dili.’
Katika awamu ya kwanza ya utawala chini ya Mwalimu Nyerere kulikuwa na uwajibikaji wa kizalendo, utiifu na hofu ya matumizi mabaya ya madaraka. Katika awamu ya pili chini ya Alhaji Ali Hassan Mwinyi wafanyabiashara walithaminiwa zaidi kuliko wafanyakazi, na hapo ndipo udokozi wa mali ya umma na upigaji dili ulikithiri.
Mkapa alifumua vijiwe vingi na ofisi nyingi za mfukoni, lakini hali ya uzembe, upigaji dili vilirejea awamu ya nne jambo ambalo Dk Magufuli amelalamikia kipindi chote cha kampeni.
CCM
Kipindi cha kampeni na baada ya kushinda urais, Dk Magufuli amekuwa akisikitishwa na usaliti wa baadhi ya wanachama. Kauli zake zinaonyesha atapambana na aliowaita “wana CCM wanafiki” ili kukijenga chama katika mwelekeo mpya.
Mhadhiri wa UDSM, Richard Mbunda amesema kazi kubwa aliyonayo Dk Magufuli ni kubadilisha mfumo wa chama hicho.“Kama CCM inataka kuendelea kubaki madarakani na isipate ushindi mwembamba kama ilivyopata katika uchaguzi wa mwaka huu, lazima wafanye mabadiliko…chama kimetekwa na baadhi ya makada jambo ambalo siyo zuri,”alisema Mbunda.
Pia alisema utekelezaji wa ahadi nyingi alizotoa ni jambo la msingi bila hivyo Watanzania watamhukumu baada ya miaka mitano.
Upinzani
Tofauti na watangulizi wake, Dk Magufuli atakakabiliwa na upinzani uliokomaa dhidi ya Serikali ya CCM. Mwaka 1992 upinzani uliporuhusiwa rasmi kisheria ilikadiriwa kwamba kulikuwa na asilimia 20 hivi na ulijionyesha katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995.
Upinzani umeendelea kukua mwaka hadi mwaka na mwaka huu ulikuwa na ushindani wa nguvu baada ya mawaziri wakuu wawili wastaafu Frederick Sumaye na Edward Lowassa kujiondoa CCM na kujiunga na upinzani. Katika kampeni Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais wa Chadema na Sumaye akiwa mpambe, walitoa upinzani mkali majimboni.
Dk Magufuli atapaswa kuwa makini katika utekelezaji wa ahadi lukuki alizotoa vinginevyo wana CCM wengi zaidi wanaweza kuwa wamefunguliwa minyororo na kujiunga na vyama vya upinzani ili kutekeleza haki yao kidemokrasia.
Umoja
Kwa mujibu wa Dk Bana, changamoto nyingine ya Dk Magufuli ni kuziba nyufa zilizojitokeza wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu. Alisema wakati wa mchakato huo kulikuwa na makundi mengi yaliyowagawanya Watanzania kikanda hivyo ana jukumu la kuziba nyufa hizo ili kurejesha umoja ikiwa ni pamoja na kuendeleza mambo mazuri ambayo Rais Kikwete aliyaanza katika kipindi cha uongozi wake.
CHANZO MWANANCHI