Ticker

10/recent/ticker-posts

MAKADA WA CCM WAZIDI KUPANDISHA JOTO LA USPIKA DODOMA..SHUHDIA KILA KITU



By Waandishi Wetu
Dodoma/Dar/Arusha. Wakati Kamati Kuu ya CCM ikikutana leo jijini Dar es Salaam kupitisha majina matatu kati ya 23 ya wanaowania uspika, joto la kuwania nafasi hiyo linazidi kupanda .
Kamati Kuu itakayoongozwa na mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete itakuwa na kazi ya kuchuja majina hayo na kubakiza matatu ya wanaowania uspika na mengine matatu ya naibu spika.
Katibu wa oganaizesheni ya Halmashauri Kuu ya CCM, Dk Muhammed Seif Khatib alisema jana kuwa hadi wanafunga uchukuaji fomu ni wanachama 21 tu waliokuwa wamechukua fomu za kuwania uspika, wakati mwanachama mmoja tu ameomba unaibu, huku Profesa Costa Mahalu akishindwa kurudisha fomu yake.
Khatibu alisema majina hayo sita yatapigiwa kura na wabunge wa CCM ili kupata jina moja, la mgombea uspika na naibu wake tayari kupambana na wagombea kutoka vyama vya upinzani.
Kwa upande mwingine, joto hilo linapanda kutokana na mvutano mkali wa kambi mbili, moja ikiongozwa na Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta na nyingine ya Naibu Spika wa Bunge la Kumi, Job Ndugai, ambaye ni mbunge mteule wa Kongwa.
Wapambe wa wagombea hao wamepiga kambi mjini Dodoma, na muda mwingi huonekana kwenye viwanja vya Bunge ambako watunga sheria wamekuwa wakijisajili.
Sitta jana aliibukia mwenyewe kwenye viwanja vya Bunge na alionekana kuzungukia wabunge katika kile kilichoonekana kuwa ni kutengeneza mazingira ya kuungwa mkono.
Mbunge huyo wa zamani wa Urambo Mashariki alifika kwenye viwanja hivyo, saa 5:50 asubuhi na kuzunguka kwa baadhi ya wabunge.
“Niacheni kwanza nikafanye kazi iliyonileta,” alisema Sitta alipofuatwa na waandishi wa habari wakitaka azungumzie uchaguzi huo.
Baadhi ya wabunge waliohojiwa kuhusu harakati za uspika, walikataa kuzungumzia kwa madai kuwa bado vikao vya chama havijafanyika kuteua majina matatu.
“Chama chenyewe hakieleweki. Ngoja tusubiri kwanza CC itakapoteua majina matatu kesho (leo),” alisema mmoja wa wabunge ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini. Hadi jana, Ndugai alikuwa hajaonekana kwenye viwanja vya Bunge, ingawa wapambe wake walikuwa wakimpigia kampeni eneo hilo.
Masaburi ajitoa kuwania uspika
Mmoja wa waliochukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kuwania kiti hicho, Didas Masaburi amejitoa akieleza kuwa atamuunga mkono mgombea atakayepitishwa na chama hicho. Masaburi si mbunge.
“Nimepigiwa simu na rafiki zangu kuwa mbona siko Dodoma, lakini kimsingi, nimeamua kujitoa nikiamini mgombea wa CCM atakayepitishwa atalivusha Bunge na nitamuunga mkono. Wote ni CCM na lengo letu ni kukijenga chama,” alisema Masaburi alipozungumza na Mwananchi kwa simu.
Mbowe aibuka
Wakati kampeni zikiendelea ndani ya CCM, Chadema imesema wanachama wengi wamejitokeza kuwania kiti hicho.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye alikuwa kwenye viwanja vya Bunge jana, alisema mchakato wa kutafuta mgombea unaendelea ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ukawa inaundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.
“Ni watu wengi wamejitokeza kuwania uspika,” alisema Mbowe bila kufafanua idadi ya wanachama waliojitokeza.
Kuhusu baadhi ya wabunge kutaka spika atokane na wabunge, Mbowe alisema kila Mtanzania ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa.
Chief Yemba ndani
Aliyekuwa mgombea wa urais wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Chief Lutalosa Yemba amesema ametuma maombi kwenye chama chake kuomba apitishwe kuwania uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Cheif Yemba alisema amepeleka maombi kupitia chama chake ili kuwania na ana imani atashinda.
Alisema kama chama chake kikimpitisha, ana imani wabunge wengi watamchagua kuwa spika wa Bunge la Kumi na Moja ambalo linahitaji mabadiliko makubwa katika utendaji kazi wake.
Maandalizi ya Bunge
Kwenye ofisi za Bunge, maandalizi ya shughuli za chombo hicho yalikuwa yanaendelea.
Mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel alisema tayari wameongeza viti ili vilingane na idadi ya wabunge waliopo.
“Tumeongeza viti katika meza zile zile zilizokuwepo na hakuna gharama yoyote iliyotumika zaidi ya gharama za kawaida,” alisema Joel alipoulizwa kuhusu gharama zilizotumika kufanya maboresho hayo.
Maisha yapanda Dodoma
Wakati Bunge likijiandaa kuanza shughuli zake, tayari maisha ya baadhi ya wakazi mjini hapa yameanza kubadilika.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wakazi walisema bei za vyakula zimepanda mara mbili ya bei zilivyokuwa kabla ya uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, katibu wa soko kuu la Majengo, Idd Vumba alisema kupanda kwa bei za vyakula mjini hapa kunatokana wakati huu kuwa msimu wa kilimo na si mavuno.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Kalunde Jamal, Mussa Juma na Rachel Chibwete.