Ticker

10/recent/ticker-posts

HII SASA NI ZAIDI YA HATARI...MEYA JERRY SILAA KAPIGA BILIONI 9 HADI BILIONI 30??APEWA BENDERA TU..ASHUKURU,...SOMA HAPA UONE HELA HIZI

SOKO JIPYA LA KISUTU NI MOJA YA MIRADI ILIYOACHWA NA MEYA JERRY SILAA IKIWA NI JITIHADA NA JUHUDI ZKE ZA KUWAACHIA WANANCHI WA MANISPAA YA ILALA SOKO LA KISASA BAADA YA KUONA SOKO KUU LA KARIAKOO KUWA HALIKIDHI HAJA YA MAHITAJI YA WANANCHI HAO..KWA KIINGEREZA TUNASEMA KIONGOZI BORA ANAACHA KUMBUKUMBU ZA KUONEKEANA NA KUENDELEA KUNUFAISHA WENGINE YAANI ''LEGACY''
MEYA JERRY SILAA AKIWA NA ''TIMU'' YA OFISI YAKE ALIYONENA KWA KINYWA CHAKE KWA KUKIRI KUSEMA MAENDELEO YA MANISPAA YA ILALA YAMECHANGIWA SANA NAO KWA KUANZIA DEREVA WAKE ALIYEKUWA ANAMFIKISHA KATIKA MIHADI NA VIKAO KWA WAKATI NDUGU KASSIM MOTTO, ,MAMA K,JOSEPHINE,JAMAL NA ANTONY WILLIAM.HII NI PICHA YA KUMBUKUMBU JANA BAADA YA MEYA HUYO KUVUNJA RASMI BARAZA HILO LA MADIWANI WA MANISPAA YA ILALA AMBAPO PIA AMEWAOMBA KUMUUNGA MKONO KATIKA HATUA YAKE MPYA YA KUGOMBEA UBUNGE KATIKA JIMBO LA UKONGA AMBAPO AMEWAAHIDI KUWALETEA MAENDELEO ZAIDI ENDAPO ATACHAGULIWA KUWA MBUNGE WA UKONGA
MEYA JERRY SILAA AKIFURAHIA BAADA YA KUPEWA  BENDERA ALIYOKUWA ANITUMIA OFISINI KWAKE KWA MIAKA MITANO IKIWA NI ISHARA YA HESHIMA KUBWA KWA UTUMISHI ULIOTUKUKA KWA WANANCHI WA KATAYA GONGO LAMBOTO NA MANISPAA YA IALA KWA UJUMLA..MASAMA BLOG INAMTAKIA KIL LA KHERI MEYA JERRY SILAA KATIKA NDOTO YAKE MPYA YA KUOMBA RIDHAA YA WANCHI KULIWAKILISHA JIMBO LA UKONGWA KWANI UWEO WAKE HAUNA SHAKA HATA KIDOGO NA TUNAAMINI ATAKUWA MSAADA MKUBWA KWA TAIFA.


HOTUBA YA MSTAHIKI MEYA MHE. JERRY SLAA WAKATI WA KUVUNJA BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA
TAREHE 06/07/2015
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilianzishwa rasmi Mwezi wa Februari 2000, hivyo kufikia mwaka 2015 sasa imetimiza miaka kumi na tano (15).  Katika kipindi chote hicho zimekuwepo awamu  tatu za Uongozi wa Waheshimiwa Madiwani, ambao ni kuanzia mwaka 2000-2005, 2005-2010 na  2010-2015. Nachukua fursa hii kuwapongeza Madiwani na Watendeaji wote ambao kwa pamoja walikaa na kuweka mipango mbalimbali ya kimaendeleo ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Baraza la Madiwani linalomaliza muda wake wa Uongozi leo tarehe 6/07/2015 ni awamu ya tatu ya Uongozi ulioanza kazi mwaka 2010. Naamini kuwa kila mmoja atakubaliana na mimi kuwa yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka mitano (5).  Kupitia miongozo iliyopo ya kuandalia Mipango na Bajeti ikiwemo-Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, MKUKUTA, MKURABITA, Malengo ya malenia na Maelekezo ya Viongozi wa Kitaifa na Baraza la Madiwani, Halmashauri imetekeleza vyema azma ya kupeleka maendeleo kwa wananchi wake na kwa mujibu wa Dira ya Halmashauri isemayo;  
“Kuwa na Jamii yenye maisha bora ifikapo mwaka 2025”.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Manispaa ya Ilala kupitia Idara mbalimbali na Vitengo vyake imeweza kutekeleza Dira yake kwa ufanisi. Mafanikio haya yanaonekana katika maeneo yafuatayo;
UKUSANYAJI WA MAPATO
Ili kuweza kutekeleza majukumu yake, Halmashauri inapaswa kuhahikikisha inakusanya mapato ya kutosha, hususani ya ndani kuwezesha utoaji wa huduma kwa wananchi wake kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.  Kwa kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano (5) Halmashauri ya Manispaa imekuwa ikiongeza juhudi za kukusanya mapato yake ya ndani.   Katika mwaka wa fedha wa 2010/2011  Halmashauri ilikisia kukusanya jumla ya Sh. 16,110,130,000, mapato halisi yaliyokusanywa mwisho wa mwaka yalifikia Sh. 13,059,508,452  sawa na Asilimia 81% ya lengo lake.  Kiwango hicho kimekuwa  kinaongezeka na kufikia mwaka huu wa fedha 2014/2015, makisio yalikuwa ni Sh. 30,450,000,000 hadi kufikia Juni, 2015 makusanyo halisi yamefikia Sh. 30,862,178,729.90 sawa na Asilimia 103 ya lengo la mwaka. Aidha kwa mwaka unaofuata wa 2015/2016 Halmashauri imepanga kukusanya Sh. 54,258,100,000  kutoka mapato ya ndani.  Jambo kubwa linalochangia mafanikio haya ni kuboreshwa kwa zoezi la kukusanya Takwimu za walipa kodi,  mpango unaolenga kubaini idadi ya walipa kodi wa Halmashauri na hivyo kuwa na makadirio halisi ya mapato. Aidha kutokana na kukua kwa Tekinolojia ya mawasiliano Manispaa imeanza kuwasiliana na Walipa kodi wake kwa njia ya simu zao za mkononi kwa ajili ya kuwahimiza na kuwakumbusha ulipaji wa Kodi/Tozo na Ushuru mbalimbali.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Usimamizi mzuri ambao umekuwa ukifanywa na Waheshimiwa Madiwani katika kuhakikisha kuwa kanuni za matumizi ya fedha zinazingatiwa, umeiwezesha  Halmashauri kuendelea kupata Hati safi za Ukaguzi wa Mahesabu. Uthibitisho wa karibu ni taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya mwaka wa fedha wa 2014/15 ambapo Manispaa ya Ilala ni miongoni mwa Halmashauri zilizopata hati safi ya Mahesabu.
MASOKO
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Manispaa ya Ilala ina jumla ya masoko 18, masoko makubwa ni Matano (5), masoko madogomadogo ni 8 na maeneo matano (5) yasiyotumika kikamilifu. Kati ya masoko matano makubwa, masoko matatu (3) ya Kisutu, Ilala na Buguruni ni masoko yaliyojengwa miaka ya 1960 hivyo kwa sasa hayakidhi mahitaji makubwa ya Wafanyabishara walioko katika masoko hayo. Katika kipindi hiki cha miaka mitano Halmashauri ya Manispaa  imeweka mazingira mazuri kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Sekta za Biashara na Masoko kwa lengo la kuzalisha ajira, hususani kwa wafanyabiashara wadogo.  Halmashauri imeweza kuanisha maeneo 17 ya kuendelezwa ikijumuisha shughuli za wafanyabiashara wadogo.  Lengo kuu likiwa kuwafanya wafanyabiashara wadogo  kuondokana na uchuuzi mdogo mdogo na kuwa wajasiriamali. Aidha Halmashauri imesaini Mkataba na Benki ya Rasilimali (Tanzania Investment Bank-TIB) kujenga soko la kisasa la Kisutu, baadaye masoko ya Buguruni na Ilala yataendelezwa. 
ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Manispaa ya Ilala imefanikiwa katika utoaji wa Elimu ya Msingi na Elimu ya Sekondari kwa wananchi wake. Katika kipindi hiki cha miaka mitano jitihada mbalimbali zimefanyika za kukabiliana na changamoto zinazoikabili Sekta ya Elimu.  Pamoja na juhudi za Serikali Kuu na Halmashauri, wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kuboresha Sekta hii. Mashirika ya simu ya Vodacom Foundation, Tigo, Benki  Kuu na KCB ni miongoni mwa waliochangia samani katika shule mbalimbali za Msingi.  Aidha Ofisi yangu kupitia ”Mayors Ball”  na Mpango uliobuniwa na Mhe Diwani wa Kipawa umezipatia baadhi ya shule madawati. Mpango wa Mnazi Mkinda wa kuibua vipaji mbalimbali kwa wanafunzi wa shule ya Msingi nao umechangia kuboresha sekta hii. Kwa takwimu zilizopo katika kipindi husika madawati 32,021 yamenunuliwa katika jitihada za kukabiliana na upungufu wa madawati. Vyumba vya madarasa 111 na Matundu ya vyoo 2109 yamejengwa katika shule za msingi. Watoto 4,876 wa elimu ya awali na 21,798 wa elimu ya msingi waliandikishwa kuanza masomo mwaka 2015,  Hali hiyo imechangia ufaulu wa shule ya msingi kupanda kutoka chini ya Asilimia 58 mwaka 2010 kufikia Asilimia 70.5 mwaka 2014. Aidha ujenzi wa vyumba 76 vya madarasa na maabara 154 katika shule za Sekondari umekamilika kwa asilimia 98. Nachukua nafasi hii kuwapongeza Madiwani wajumbe wa Kamati iliyosimamia masuala ya Elimu, Mkurugenzi wa Manispaa na Wataalam wake kwa kuhakikisha mipango ya elimu inatekelezwa kwa ufanisi.

HUDUMA ZA AFYA
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika eneo la Afya yapo mafanikio makubwa yaliyofikiwa. Kwa mujibu wa Takwimu zilizokuwepo mwaka 2010  kulikuwa na jumla ya zahanati, vituo vya Afya  na Hospital 19 ambapo hadi kufikia  mwaka 2015 vimeongezeka na kufikia 29. Aidha katika kipindi hiki baadhi ya Hospitali na Zahanati zimeingizwa kwenye mchakato wa kupandishwa hadhi.  Hospitali ya Amana imepanda hadhi na sasa ni Hospital ya Mkoa ambapo Kituo cha Afya Mnazi Mmoja kimepandishwa hadhi kuwa Hospital.  Zahanati ya Pugu Kajiungeni inaendelea na mchakato wa kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. Kumekuwa na kuimarika kwa ushirikiano kati ya Idara ya Afya na Wadau wa Afya hususan Taasisi zinazojihusika na utoaji wa Tiba. Utoaji wa Chanjo kwa Watoto na Kina Mama Wajawazito umevuka lengo la Kitaifa la asilimia 90 na kufikia asilimia 100 kwa chanjo karibu zote. Mafanikio haya yote yanaonesha ni jinsi gani Waheshimiwa Madiwani pamoja na Watendaji wameweza kuelekeza jitihada zao katika eneo hili muhimu la huduma linalogusa moja kwa moja maisha ya Wananchi, kwani inaaminika kuwa Mtu mwenye Afya bora anao mchango mkubwa katika familia yake na Taifa lake.

USAFI NA HIFADHI YA MAZINGIRA
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika eneo hili, Halmashauri inaendelea na juhudi za kuliweka Jiji katika hali ya usafi. Takwimu zinaonesha wakazi wa Manispaa ya Ilala wanazalisha tani 1,100 za taka ngumu kila siku wakati uwezo wa kuzoa na kusafirisha hadi dampo la Kigogo Fresh katika Kata ya Pugu ni Tani 676  kufikia Juni, 2015 kiwango hicho ni sawa na Asilimia 61% ya uzalishaji. Mwaka 2010 Halmashauri pamoja na Wakandarasi wengine wa kuzoa taka waliweza kuzoa wastani wa Asilimia 50% za taka ngumu kwa siku.  Aidha Halmashauri ina uwezo wa kufagia Km. 136 za barabara kwa siku dhidi ya Km. 126 za mwaka 2010.  Uwezo huu mdogo wa uzoaji wa taka umechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa vitendea kazi hususani, malori yenye uwezo mkubwa wa kuzoa taka.  Baraza hili la Madiwani linavunjwa likiwa tayari limetoa idhini ya kukopa Sh. 2.55 Bilioni kwa ajili ya kununua malori 17 ya kusafirisha taka ili kuboresha zaidi hali ya usafi Jijini.
Kwa kushirikiana na Sekta binafsi Halmashauri inaendelea kutunza jumla ya Ha. 137.4 za misitu katika bonde la Zingiziwa, Kinyerezi, Kivule dhidi ya majanga ya moto na uvunaji usio endelevu wa mazao ya misitu. Vikundi 7 vinaendelea na ufugaji nyuki kutumia mizinga ya 157 iliyotundikwa katika misitu ya asili, na ya kupandwa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa.  Kupitia Kamati za mazingira za Kata, Wananchi wamekuwa wakielimishwa juu ya umuhimu wa kutunza Vyanzo vya maji na Uoto wa asili hususani kwenye maeneo ya miinuko.
MIPANGOMIJI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kama inavyofahamika Manispaa ya Ilala ndiyo yenye kubeba taswira ya Jiji la Dar es Salaam, hivyo katika kipindi hiki cha miaka mitano (5)  jitihada zimefanyika za kuhakikisha kuwa ujenzi wa nyumba na majengo unazingatia Sheria na kupunguza makazi holela. Kumekuwa na mipango ya kubadilisha taswira ya eneo la Manispaa ambapo mipango ya uendelezaji upya wa maeneo mbalimbali imeidhinishwa.  Jumla ya viwanja 29,243 vimemilikishwa kwa wananchi na viwanja 9,123 vimepimwa katika maeneo ya umma, leseni mpya za makazi 1,568 zimesajiliwa. Aidha wananchi 62,000 wamepata elimu ya sheria za ardhi, Mipango miji na matumizi bora ya ardhi.

UJENZI WA MIUNDOMBINU
Kupitia Idara ya Ujenzi, Halmashauri ya Manispaa imeweza kuboresha zaidi miundombinu yake ya Barabara, ambapo imeweza kuongeza urefu wa Km. 71.31 za barabara za lami kutoka jumla ya Km. 190.32 zilizokuwepo mwaka 2010 kufikia Km. 261.63  mwaka 2015.  Urefu wa barabara za Changarawe umeongezeka kwa Km. 56.77 kutoka Km. 76.6 za mwaka 2010 kufikia Km. 133.37 mwaka 2015 na barabara za udongo zenye urefu wa Km. 638.95. zimetengenezwa. Aidha, makalavati 37 nayo yameweza kujengwa.  Katika kipindi hiki Manispaa imeweza kununua Greda mbili (2) kwa njia ya mkopo ikilenga kuhakikisha kuwa barabara zake zote zinapitika katika vipindi vyote vya mwaka.
HUDUMA ZA MAJI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Sote tunatambua kuwa maji ni rasilimali muhimu.  Katika kipindi hiki cha miaka mitano (5) jitihada za kusambaza maji safi na salama katika Manispaa zimefanyika ambapo Halmashauri imechimba visima virefu 42 na kufanya jumla ya visima vyote vilivyopo kufikia 247. Visima vifupi nane (8) vilichimbwa na kufikia jumla ya visima 69. Vituo vya kuchotea maji 1,239 Mifumo 9 ya kuvuna maji ya mvua imejengwa.  Vikundi vya watumia maji 15 na kamati za maji 50 zimeundwa. Hadi kufikia Juni, 2015 idadi ya wakazi wanaopata maji safi na salama wanaohudumiwa na visima vya Halmashauri wamefikia Asilimia 52% ya wakazi wote wa Manispaa wanaokadiriwa kuwa 1,220,611 (Sensa ya 2012).
MAENDELEO NA USTAWI WA JAMI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2015 Manispaa ya Ilala imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya Ustawi wa Jamii ambapo upo mfumo mzuri wa kuendeleza vikundi vya Wanawake na Vijana. Makundi haya yamekuwa yakinufaika kwa kupatiwa mikopo kutoka Benki yetu ya DCB ambapo Halmashauri ina hisa, pia Mfuko wa Wanawake na Vijana umeendelezwa kwa Halmashauri kutenga fedha kukopesha makundi hayo.  Hadi kufikia Juni 2015 vikundi 37 vilifikia  hatua za mwisho za kukopeshwa mitaji ya biashara. Aidha Manispaa ya Ilala imeweka mfumo mzuri wa kuhudumia Watoto waishio katika mazingira hatarishi kupitia Timu ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto. Dawati la kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu lililofunguliwa Hospital ya Amana limewezesha kuokoa idadi kubwa ya Watoto waliokuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia.
MAHUSIANO NA WADAU
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunapopima mafanikio ya Manispaa ya Ilala hatuwezi kuacha kuzungumzia eneo la mahusiano.  Dhana ya maendeleo kwa njia ya kushirikisha Wadau wakijumuisha Wafadhili imeendelea kutekelezwa ndani ya Manispaa ya Ilala.  Ofisi ya Mstahiki Meya imeweza kushawishi Shirika la KOICA kujenga Hospitali eneo la Chanika. Mkataba wa Makubaliano ya kuanza ujenzi umeshasainiwa. Ujenzi wa Hospital hii utasaidia kusogeza huduma karibu na Wananchi na kupunguza msongamano wa Wagonjwa katika Hospitali ya Amana. Katika kipindi hiki mipango ya Maendeleo inayoibuliwa imekuwa Shirikishi. Kata zote 26 zimeunda Kamati ya wananchi zenye jukumu kuu la kuibua vipaumbele vya ngazi ngazi ya Kata ambavyo baada ya kuidhinishwa na Kamati za Maendeleo za Kata inajumuishwa katika Mipango na Bajeti ya Halmashauri ambako inatengewa fedha.  Aidha Halmashauri imesimamia na kuendeleza mahusiano yaliyopo kati ya Manispaa ya Ilala na Mji wa Kokkola ulioko Finland.


KUTANGAZA SHUGHULI MBALIMBALI ZA HALMASHAURI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeweza kuweka mahusiano mazuri na vyombo vya Habari ambavyo vimekuwa vikiuhabarisha umma masuala mbalimbali yanayotokea na yanayoihusu Manispaa ya Ilala.  Katika kujitangaza huko Halmashauri inalo Jarida lake ambalo limekuwa likitangaza kazi mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa.  Aidha kupitia mitandao ya kijamii Manispaa imeanzisha Blog - Habari ilala.Blogspot.Com ambayo hadi kufikia Juni 2015 jumla ya wanaoingia katika mtandao huo imefikia 30,000 kutoka pande zote za dunia.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Napenda kumalizia hotuba yangu kwa kusema kwamba, Baraza hili la Madiwani la Awamu ya tatu ya Uhai wa Halmashauri  linavunjwa likiwa lina mambo ya kujivunia hususani katika kuandaa mazingira endelevu ya Uwekezaji, Kuongezeka kwa mapato ya ndani, Uboreshaji wa huduma za Kiuchumi, elimu na Afya. Nampongeza Mkurugenzi na timu yake ya wataalam, Waheshimiwa Madiwani wote, Uongozi wa Wilaya, Uongozi wa Mkoa na wataalam wake. Ushirikiano wa karibu wa timu hii umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio tunayoyaona kwa sasa. Naamini Awamu ya nne ya Uongozi unaokuja utaanzia mahali pazuri.
Ahsante sana kwa kunisikiliza.

Jerry Silaa
MEYA WA MANISPAA
HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA