Ticker

10/recent/ticker-posts

MAPENZI:SHOGA KATIKA MAHUSIANO YAKO USITAFUTE MCHAWI, UMEJIROGA MWENYEWE..SOMA HAPA UELEWE

Jamani hamjambo? naona viroho vinawadunda baada ya kuufunua ukurasa huu na kujiuliza leo kombora linaangukia kwa nani? Narudia, sipo kwa ajili ya kuwarusha roho bali mtajirusha wenyewe kutokana na tabia zenu mbaya.  Nia yangu ni kumuona mwanamke mwenzangu mambo ya kike hayampiti kando.
Jamani kuna mambo mengine yanasikitisha, hivi kwa nini umuogope mwanamke mwenzio mwenye viungo kama wewe. Wiki iliyokwisha nilielezea makosa ya nyuki kukimbia mzinga wake kwa sababu tu mtu katia mkono na kulamba asali yako.

Ukiona mtu katia mkono kwenye mzinga wako ujue asali yako ni  tamu unatakiwa kuilinda na siyo kuukimbia mzinga kuwaruhusu watu wajilambie kwa raha zao, haipendezi. Hizo ni hasira za mkizi na kutoa kafara kwa mvuvi. Nimeliongelea hili kwa vile makavu ya leo yanafanana na hilo.

Juzi nilikutana na mtoto wa shoga yangu akiwa anatoka sokoni, katika mazungumzo yetu si unajua mimi mtu wa utani. Sijui kukasirika kijinga,  mtoto wa kike niliumbwa siku Mungu akitabasamu nami nikawa na umbile la tabasamu, siyo wewe uliumbwa Mungu amechoka kila wakati uso kama ndimu ,unacheka hujulikani, umenuna hujulikani!

Si kwamba nazungumzia wenye sura mbaya, bali wenye sura zilizokosa tabasamu, siwezi kumhukumu mtu kwa maumbile kwa vile mimi sijawahi kuumba. Ila nazungumza na tabia za watu, Mungu kawaumba na sura nzuri lakini imeharibika kwa kukunja uso na kupinda midomo.

Hebu tuachane na hayo tuendelee na yetu, basi katika kutaniana si ndiyo aliponieleza kaamua kurudi kwao baada ya mumewe kuoa mwanamke mwingine. Nilimuuliza kipi kikubwa kilichomuondoa kwa mumewe ikiwa dini yake inamruhusu. Alinijibu jibu la kitoto ambalo lipo katika vichwa vya wanawake wengi.

Eti ameondoka kwa vile hawezi kushea mwanaume na mwanamke mwenzake. Jibu lake lilinifanya nimwangalie chini mpaka juu hadi akashtuka na kuniuliza kulikoni kumuangalia vile.  Nilichomueleza nataka nikae na wewe chini nikueleze uache ujinga wa kijinga!

Jamani  ni kweli wanawake tupo kama mdudu wa sikio tusiotaka mshirika, lakini kutokana na hali ya sasa hivi kuwa na wako wa peke yako ni kazi. Afadhali dini nyingine zinaruhusu mpaka wake wanne, lakini dini zilizokataa tunaona jinsi gani viongozi wao wanavyoingia kwenye kashfa ya kuwa na wanawake wengi tofauti na muongozo wa dini yake.

Siyo kwamba nahalalisha lakini ukweli ndiyo ulivyo asilimia kubwa ya nyumba, waume zetu wana wanawake zaidi ya mmoja. Wengine tunawakamata na wasichana wetu wa kazi, imefikia hata kuwapa ujauzito.

Hii yote inatokana pengine na udhaifu wetu ndani ya ndoa kwani wengi baada ya kuolewa hujisahau na kuamini ukishaolewa umemaliza.Tumekuwa hatuzithamini ndoa zetu kwa kuamini baada ya kuolewa hakuna kingine zaidi kwa mumeo kama umemvulia nguo ya ndani ndiyo baaaasi. Tunasahau mwanaume unatakiwa kumtunza kama mtoto kwani wewe ndiye kila kitu kwake, siyo kasoro zitolewe na mwanamke wa pembeni.

Pengine mumeo hakuwa na wazo la kuongeza mwanamke mwingine, lakini mwenzako aliona mapungufu yako na  kuyafanyia kazi ndiyo yakamfanya mumeo aingie kichwakichwa baada ya kunasa, aliendelea kumpa vitu adimu ambavyo kwako hapati. Ili afaidi vizuri anamuoa kabisa ili asile kwa kujificha.

Unaletewa mke mwenza unakimbia kumbe sababu ni wewe. Kaingia ndani hutakiwi kukimbia, jirekebishe pigana  kuhakikisha unairudisha namba moja yako.

Nina imani nimesomeka vizuri, basi kwa leo inatosha tukutane wiki ijayo, ni mimi Anti Nasra, Shangingi Mstaafu.