Ticker

10/recent/ticker-posts

CHONGOLO: CCM IKO MAKINI MJADALA UWEKEZAJI BANDARINI,AKEMEA VIKALI WAPOTOSHAJI

 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo amewatoa hofu wananchi na Watanzania kwa ujumla dhidi ya kile alichokiita ni upotoshaji kuhusu Makubaliano ya Serikali za Tanzania na Dubai, kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uboreshaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar Es Salaam, akiwataka kuwa makini na wanasiasa na wanaharakati ambao wamegeuza suala hilo kuwa ni ‘kete’ ya kisiasa, badala ya kuona ni fursa kubwa ya nchi kunufaika kimkakati dhidi ya washindani wengine.

Ndugu Chongolo amesema kuwa makubaliano hayo yaliyoingiwa na Serikali za pande hizo mbili, ni hatua nyingine mojawapo muhimu katika kufanya Mapinduzi ya Uchumi kwa Maendeleo ya Watu, kama ilivyonadiwa na kuahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, akiongeza kuwa uwekezaji huo unalenga kuboresha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, kuimarisha utendaji kazi wake na pia kuongeza kiwango cha mizigo kinachoingia na kutoka katika bandari hiyo, jambo ambalo litaongeza tija kwa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), mazingira mazuri ya kuongeza mapato ya Serikali, kutengeneza ajira na kuvutia uwekezaji zaidi, nchini. 

Katibu Mkuu Ndugu Chongolo ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari waliotaka maoni yake na msimamo wa CCM kuhusu suala hilo ambalo limeibua mjadala mkubwa siku za hivi karibuni miongoni mwa Watanzania, ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza kuwa ni muhimu wananchi kujadili na kutoa maoni yao kuhusu mambo muhimu yanayohusu mstakabali wa taifa letu, lakini akatahadharisha kuwa wapotoshaji wa makusudi wasitumie nafasi hiyo, kama mwanya wa kuibuka kisiasa na kiharakati.

Ndugu Chongolo amekemea vikali kitendo cha baadhi ya wanasiasa na wanaharakati hao kugeuza mjadala huo kuwa ‘kete’ ya kisiasa, wakiwapotosha Watanzania kuhusu makubaliano hayo, huku wakitumia maneno ya kibaguzi yanayolenga kugawanya watu na kuvuruga umoja wa kitaifa. Akisisitiza, Chongolo amesema kuwa wanachokifanya watu hao ni dalili ya kuishiwa sera, agenda na kukosa uzalendo, hivyo wanahangaika kutafuta kukubalika kwa kutumia ubaguzi wa kidini, kijinsia, rangi na hata kuwabagua watu kwa sababu wanatokea upande mmojawapo wa Muungano wa Tanzania. Akisema ubaguzi wa aina yoyote, kamwe haukubaliki Tanzania.

“Ndugu zangu…ni vyema tukatambua kuwa jambo hili linalokwenda kufanyika la uwekezaji wa bandarini, ni jambo kubwa sana na muhimu, ambalo linahitaji maamuzi muhimu na magumu kufanyika, yakiongozwa na dira na maono ya kiuongozi. Uongozi ni kuwa na maono, kuona fursa kwa ajili ya watu unaowaongoza na kufanya maamuzi kwa ajili yao, kwa ajili ya manufaa na maslahi ya unaowaongoza na kwa niaba yao. Kimsingi, kwa mataifa ambayo yameendelea, suala la uwekezaji wa uboreshaji na uendeshaji wa bandari si geni…na hata kwa mataifa mengine ambayo yana bandari ndogo kuliko sisi. Lakini kwa sababu ya uwekezaji mkubwa wa kuboresha na kuendesha bandari zao, faida na tija wanayopata wao wanaonekana kuwa mbele kuliko sisi katika eneo hili la bandari.

“Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025…kitabu chenye kurasa 303, Chama Cha Mapinduzi tuliweka bayana…kafanye rejea, kuwa tutaisimamia Serikali kutafsiri katika vitendo maelekezo ya Chama kuhusu kufanya Mapinduzi ya Uchumi kwa Maendeleo ya Watu. Huko ndani tulizungumzia mahitaji kadhaa, mojawapo lilihusu kuboresha miundombinu na huduma wezeshi kama uchukuzi kuwa sehemu ya kufanikisha mapinduzi hayo. Na tukasisitiza kuwa tutahakikisha uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati, ikiwemo reli, viwanja vya ndege na bandari,” amesema Ndugu Chongolo.

Katibu Mkuu wa CCM huyo, alisisitiza kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 – 2025, unazingatia Mwelekeo wa Sera za Chama Cha Mapinduzi wa 2020-2030, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020-2050, na iliweka bayana kuwa mabadiliko mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiteknolojia yanayotokea nchini na duniani, yataangaliwa kuwa ni fursa ya kujifunza na kuboresha mazingira ya Tanzania katika nyanja mbalimbali, ili kuendelea kuboresha mikakati na misingi ya kukuza uchumi na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji mali.

“Sisi Chama Cha Mapinduzi, tukiwa na dhamana ya uongozi wa taifa letu Tanzania, hatuwezi kukubaliana na taarifa potofu zenye lengo la kuwagawa wananchi na kuzua taharuki miongoni mwa watu katika jamii, zikiwemo lugha za ubaguzi. Tunaona wazi kuwa uwekezaji huo unaenda kuwa na tija kwa nchi yetu kwa ujumla na tunaomba wananchi na wanasiasa waone jambo hili kuwa ni suala la taifa, ni jambo la nchi,” amesema Chongolo.

Post a Comment

0 Comments