Ticker

10/recent/ticker-posts

KUTANA NA ‘PACHA’ WA MAINDA WA BONGO MUVI MWENYE VURUGU KWA MWANAYE

Hamida Hassan na Imelda Mtema
Katika ulimwengu wa sanaa ya maigizo nchini, yupo mwanadada ambaye havumi sana lakini yumo. Wengi wanamfahamu kwa jina la Muna lakini jina lake halisi ni Rose Alfonce.Mwanadada huyo, mama wa mtoto mmoja, Patrick mwenye miaka minne, ni ‘pacha’ wa msanii wa filamu, Ruth Suka ‘Mainda’. Amekuwa akifanya mambo mengi ya kisanii na kijamii lakini si mtu wa kuuza sana nyago kwenye magazeti.
Wiki hii Ijumaa lilimuweka mtu kati, likamtaka azungumzie baadhi ya mambo ambayo watu wangependa kuyajua ikiwemo malezi yasiyofaa anayodaiwa kumpa mwanaye, uhusiano wake na mwanamuziki Kalala Junior pamoja na ukaribu wake na wasanii wenzake Elizebeth Michael ‘Lulu’ na Mainda.
Mjue kwanza kidogo
“Kwenye hili la uigizaji nilianza mwaka 2004 nikiwa ndani ya Kundi la Shirikisho nilipoigiza kwenye tamthiliya zilizokuwa zikirushwa kwenye Televisheni ya ITV ambazo ni Hatia na Siri.
“Ukiacha tamthiliya hizo, nilipata umaarufu sana kwenye filamu za Born to Suffer, Sekeseke, Siri ya Penzi na nyingine kibao.

Ahamia Haki Elimu
“Baada ya kucheza filamu nyingi, nikabahatika kuingia kwenye matangazo mbalimbali na mara ya mwisho niliingia kwenye yale ya Haki Elimu ambapo nilionekana kama mwanafunzi.
Zaidi ya usanii
“Mbali na masuala ya uigizaji, sasa hivi nafanya biashara mbalimbali.

Ana undugu na Mainda?
“Mainda siyo ndugu yangu kama baadhi ya watu wanavyofikiri, ni mtu wangu wa karibu sana ambaye kwenye maisha yangu ya kisanii amechangia kwa kiasi kikubwa. Ndiyo maana tunaitana mapacha.

Amzungumzia Lulu
“Wengi wanakumbuka nilivyomsaidia Lulu alipokuwa gerezani na hata baada ya kutoka nilikaa naye pale kwangu kwa siku kadhaaa. Yule pia ni zaidi ya rafiki yangu na tumekuwa tukisaidiana kwa mengi.

Ni kweli yeye na Kalala Junior ni wapenzi?
“Naomba hili nisilizungumzie kwa leo kwani nahisi ni mapema sana. Watu wanaona tuna ukaribu sana na kila mmoja anahisi kivyake lakini niseme tu kwamba muda ukifika nitaweka wazi kila kitu.

Kuhusu malezi ya mwanaye
“Nampenda sana mwanangu Patrick, nipo tayari kufanya lolote zuri kwa ajili yake na ndiyo maana watu wanasema namlea vibaya, wakumbuke kuwa mwanangu ni staa hivyo kunyoa viduku, kuvaa kistaa siyo tatizo.
“Ameshacheza filamu nyingi na kuonekana kwenye matangazo mengi na amesaini mkataba na kampuni moja ya matangazo ambayo itamlipa dola 1,300 ambazo ni takriban shilingi milioni mbili. “Nimemnunulia gari aina ya Passo na ameshaanza kuiendesha. “Mwanangu napenda aje kuwa rubani,” anasema Muna.