Katika mahojiano maalum na mtangazaji Millard Ayo, Jesca Magufuli, mtoto wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli — Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania — ameweka wazi msimamo wa baba yao kuhusu elimu, akieleza kuwa Hayati Magufuli alikuwa muumini mkubwa wa elimu ya ndani ya nchi.
Jesca amesema kuwa kati ya watoto wa Hayati Magufuli, ni mmoja tu aliyebahatika kusoma nje ya nchi, na hata hivyo ilikuwa kwa ajili ya shahada ya pili (Masters), si shahada ya kwanza. Akiendelea kufafanua, Jesca alieleza kuwa alipokuwa anaingia mwaka wa kwanza wa chuo kikuu, baba yake alimwahidi kwamba endapo atahitimu shahada ya kwanza vizuri, atapewa nafasi ya kuendelea na shahada ya pili nje ya nchi.
“Nilifurahi sana wakati huo, nikasubiri kwa hamu hiyo nafasi," Jesca alisema katika mahojiano hayo. "Niliona kama ndoto kubwa inaningojea."
Hata hivyo, mambo yalibadilika baada ya Jesca kuhitimu shahada ya kwanza. Hayati Magufuli alimwambia kuwa ataendelea na masomo ya shahada ya pili hapa hapa nchini, katika chuo kikuu alichohitimu shahada yake ya kwanza. Jesca alisema kuwa ingawa alikuwa ametamani sana kusoma nje ya nchi, aliheshimu maamuzi ya baba yake na kuyaelewa, hasa ikizingatiwa imani kubwa aliyokuwa nayo katika ubora wa elimu ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Jesca, Hayati Magufuli aliamini kuwa Tanzania ina vyuo vikuu na walimu wa viwango vya juu vya kimataifa, hivyo hakuwaona watoto wake wakihitaji kwenda nje ili kupata elimu bora.
Mahojiano haya yameibua hisia miongoni mwa Watanzania wengi, hasa wale waliomfahamu Hayati Magufuli kama kiongozi aliyesisitiza uzalendo na kuwekeza katika maendeleo ya ndani ya nchi, ikiwemo sekta ya elimu.
Chanzo: Amplifaya/Clouds FM