Ticker

10/recent/ticker-posts

Makutano ya Barabara za Kongwa na Mpwapwa Kujengwa,RC Senyamule Aongoza kikao cha utekelezaji

Bodi ya Barabara Mkoa wa Dodoma leo Desemba 20, 2023 imefanya kikao chake cha kwanza mwaka 2023/24 kuwasilisha, kujadili na kushauri juu ya utekelezaji wa miradi ya Barabara za Mkoa kwa kipindi cha Julai hadi Novemba. Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, kimefanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkoa jengo la Mkapa Jijini Dodoma

Katika kikao hicho, Mwenyekiti amewasilisha taarifa ya bajeti ya jumla ya Mkoa kwenye ujenzi wa miundombinu ya Barabara na kuwataka wajumbe kwa niaba ya wananchi kufanya maendeleo ili kuinua Uchumi kulingana na maendeleo yaliyopatikana.
"Mkoa umepata jumla ya shilingi Bilioni 230.29 kutekeleza miradi ya Barabara kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo TANROADS wamewezeshwa kutengeneza Barabara zenye jumla ya urefu wa Km 9248.12, TARURA wamewezeshwa kutengeneza Barabara zenye urefu wa jumla ya Km 7540.9 ambapo jumla wote wamepatiwa kiasi cha Shilingi Bilioni 593 na Milioni 69.

" Utekelezaji huu wa miradi ya Barabara pamoja na miradi mingine ya Kimkakati inayotekelezwa hapa Dodoma tuifanye ifanane na matokeo yanayotarajiwa, uwepo wa barabara hizi uendane kukua kwa Uchumi wa wananchi kwani Serikali imewekeza ili kuwainua wananchi wake" Amesema Mhe. Senyamule
Awali akifungua kikao hicho, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu, amezungumzia lengo na kazi za bodi ya Barabara ya Mkoa.

"Bodi ya Barabara ya Mkoa ina kazi ya kushauri na kutoa maelekezo juu ya maendeleo ya Barabara, kutekeleza miradi ya Barabara inayoletwa na Serikali, kupokea ushauri kuhusu miradi ya Barabara za Mkoa na Halmashauri pamoja na kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Waziri mwenye dhamana" Amesema Bw. Gugu.
Kikao kimefikia maazimio kadhaa yakiwemo TANROADS, TARURA kwa kushirikiana na Halmashauri waendelee kuchukua tahadhari juu ya mvua zinazoendelea kunyesha ili kuepuka madhara kwa Barabara, TANROADS na TARURA ziwasilishe jumla ya fidia zinazodaiwa na wananchi wanaopitiwa na miradi ya Barabara na ujenzi wa Barabara ya makutano ya Kongwa- Mpwapwa ukamilike huku ahadi ya kuanzia Mpwapwa itekelezwe.

 

Post a Comment

0 Comments